Wema ana kesi ya kujibu

Muktasari:

  • Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kwamba Wema na wenzake wataanza kujitetea Mei 14 na 15, mwaka huu.

Dar es Salaam.Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuona malkia wa Bongo Movie na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili waokabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya, wana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kwamba Wema na wenzake wataanza kujitetea Mei 14 na 15, mwaka huu.

Hakimu Simba alitoa uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watano wa upande wa mashtaka wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula.

Kabla ya uamuzi huo kutolewa na Hakimu Simba, Wakili Kakula aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo jana ilipangwa kwa ajili ya uamuzi kama washtakiwa watakuwa na kesi ya kujibu ama la.

Baada ya Ku tolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Simba alisema kwa kujibu wa sheria iwapo washtakiwa watapatikana kuwa wana kesi ya kujibu wataanza kujitetea na wakionekana hawana kesi ya kujibu wataachiwa huru.

Hakimu Simba alisema baada ya kupitia hoja zote zilizowasilishwa mahakamani hapo, imejitosheleza kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

Wema na washitakiwa wenzake, Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya, wanatetewa na Wakili Alberto Msando.