Uhondo wote wa FA upo Shinyanga leo

Muktasari:

Mbabe wa mchezo huo atasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Singida United na JKT Tanzania kucheza fainali itakayofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha Juni 2.

SHINYANGA nzima itasimama leo Ijumaa pale nusu fainali ya kwanza ya Kombe la FA kati ya Stand United na Mtibwa Sugar itakapopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Mbabe wa mchezo huo atasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Singida United na JKT Tanzania kucheza fainali itakayofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha Juni 2.

Mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu hizo, Stand United iliitandika Mtibwa Sugar mabao 2-1 katika mpambano wa Ligi Kuu uliopigwa Februari 4, kwenye uwanja huo huo.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi katwila alisema wako vizuri kuwavaa Stand United na amesema mipango yao ni kuhakikisha wanatinga fainali. Alisema wataingia kwa tahadhari kubwa katika mpambano huo kwani wapinzani wao si wa kubezwa hivyo wamejipanga vilivyo kupambana nao.

“Tayari tupo hapa Shinyanga, kikosi changu kipo sawa kabisa, sina majeruhi najua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunatinga fainali,” alisema Katwila.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athumani Bilali “Bilo” alisema hakuna kingine wanachokihitaji katika mpambano huo zaidi ya ushindi ambao utawafanya watinge fainali kwa mara ya kwanza.

“Tunajua pa kuwabana Mtibwa kwani hivi karibuni tulicheza nao, kikubwa tunahitaji sana hili kombe msimu huu,” alisema Bilo.