VIDEO: Saida Karoli kupamba Tamasha la Sauti za Busara

Muktasari:

Baadhi ya wanamuziki wanaotarajiwa kukonga nyoyo za watazamaji katika tamasha hilo ni Zakes Bantwin (Afrika Kusini), Kasai Allstars (DRC), Somi (Uganda/USA), Ribab Fusion (Morocco), Mlimani Park Orchesta (Tanzania), Grace Matata (Tanzania), Segere Original (Tanzania), Saida Karoli (Tanzania).

Wageni kutoka katika kila pembe ya dunia wanatarajiwa kukusanyika kusherehekea utajiri wa muziki wa Kiafrika kwenye Tamasha la Sauti za Busara, huku likitoa kipaumbele kwa wasanii wadogo na wanaochipukia, pamoja na muziki wenye utambulisho.
Tamasha la Sauti za Busara mwaka huu 2018 limebeba kaulimbiu ya ‘Kuunganishwa kwa Muziki’.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mohamed alisema tamasha linazingatia Zanzibar na Tanzania sehemu mbalimbali duniani kwa kuwa linavutia mapromota wa kimataifa na kutoa fursa adhimu kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki kuupeleka duniani kote.
Alisisitiza kuwa, orodha ya mwaka 2018 ni bora kuwahi kutokea kwa miaka yote 15 ya uhai wa tamasha hilo. "Ndani ya majukwaa matatu kwa siku nne, tamasha litakuwa na naonyesho 46 yenye hadhi ya kimataifa ambayo kwa asilimia 100 yatapigwa mubashara.
  "Tamasha litawaleta pamoja wanamuziki wadogo na wakubwa kutoka katika viunga vyetu na hata nje ya nchi, likibeba dhumuni moja, huku tukisimama pamoja kupitia kaulimbiu ya Kuunganishwa na Muziki," alisema Yusuf.