TP Mazembe yatinga fainali kibabe

Muktasari:

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Baptist Jijini hapa, TP Mazembe ikicheza kwa kujiamini, iliweza kuibuka na ushindi huo na kufanikiwa kutinga fainali.

JUZI Jumatano Farudume walijikuta katika wakati mgumu baada ya kukutana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa TP Mazembe kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mbuzi.

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Baptist Jijini hapa, TP Mazembe ikicheza kwa kujiamini, iliweza kuibuka na ushindi huo na kufanikiwa kutinga fainali.

Katika mpambano huo, TP Mazembe walipata bao la kuongoza katika dakika ya 39 kupitia kwa Jafari Khamis akimalizia krosi safi ya Juma Ahmad na kuwachanganya wapinzani wao.

Licha ya Farudume kupambana kiume kipindi cha pili kutaka kusawazisha bao hilo, walijikuta wakidundwa tena la pili lililowekwa kimiani na Ramadhan Ramadhan katika dakika ya 78.

Kwa matokeo hayo, TP Mazembe watamsubiri mshindi kati ya Jiwe Kuu FC na Kitangiri Shooters kukipiga hatua ya fainali, ambapo bingwa ataondoka na mbuzi wawili na kombe.

Mratibu wa ligi hiyo, Goodluck Charles alisema Fainali inatarajiwa kupigwa Jumapili ya wiki hii na tayari zawadi zimeshaandaliwa na wanamsubiri mshindi tu.

“Kila kitu kiko sawa, kinachosubiriwa tu ni fainali hiyo kupigwa na bingwa achukue mbuzi wake,” alisema mratibu huyo.