Sholo Mwamba ameishika singeli

Muktasari:

  • Ukiachana na Man Fongo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na kibao chake cha ‘Hainaga Ushemeji’, Singeli Fleva imeshikwa na Sholo Mwamba.

SINGELI ndiyo habari ya mjini. Muziki fulani hivi wa kasi na wenye nakshi za kutosha. Una mastaa wake na mashabiki wake karibu nchi nzima kwa sasa.

Ukiachana na Man Fongo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na kibao chake cha ‘Hainaga Ushemeji’, Singeli Fleva imeshikwa na Sholo Mwamba.

Huyu ndiye mfalme halisi wa muziki huo unaokimbiza vilivyo kwa sasa. Anatamba na nyimbo zake kadhaa kama ‘Gheto’, ‘Ukinipa Sisemi’, ‘Panya’, ‘Mwaga Maji’ ‘Namba Moja,’ na nyingine kali.

Sholo ameishika zaidi Singeli kutokana na aina ya uimbaji wake pamoja na staili yake ya nywele ambayo huwezi kuikuta sehemu nyingi hapa nchini. Amesuka dredi halafu amenyoa staili flani hivi kama nusu kichwa. Jamaa anaonekana mtamu ile mbaya.

Mwanaspoti limepiga stori mbili tatu na Sholo Mwamba na kujibu maswali mbalimbali.

Mwanaspoti: Inasemekana unapenda sigara kubwa kuliko chakula, hii imekaaje?

Sholo Mwamba:Duu! Situmii sigara kubwa, ila kwenye suala la msosi ni kweli wakati mwingine huwa nasahau kula.

Mwanaspoti: Asubuhi huwa unakumbuka ndoto unazoota usiku?

Sholo Mwamba: Ni mara chache sana.

Mwanaspoti: Huwa una ratiba gani ukiamka asubuhi?

Sholo Mwamba: Baada ya kuamka huwa nafanya mazoezi kwanza kuweka viungo sawa kisha nahamia kwenye usafi maana si unajua usela siyo uchafu kisha mengine yanafuata.

Mwanaspoti: Unafikiri una kitu gani cha tofauti na mastaa wengine wa Bongo?

Sholo Mwamba: Mimi ni fundi wa kukaangiza, yaani niko tofauti na mastaa wengi wa kiume. Sina haja ya kuomba nipikiwe au kununua vyakula kama baadhi ya mastaa wanavyofanya.

Mwanaspoti: Starehe yako kubwa ukiwa nyumbani ni ipi?

Sholo Mwamba: Napenda kuandika mistari ya nyimbo na kutazama filamu.

Mwanaspoti: Unatuhumiwa kwamba umewatupa masela wako wa zamani baada ya kupata umaarufu, hii ina ukweli?

Sholo Mwamba: Hapana, sio kweli, siwezi kuwatupa wanangu kwa sababu nilikuwa nao kabla ya kutusua. Naanzaje kuwatenga, nikifanya hivyo nitaonekana kama nimesaliti kambi.

Mwanaspoti:Inasemekana unaogopa kutongoza mademu hasa wakali, hili nalo ni kweli?

Sholo Mwamba: Hahaha..., kweli mimi ni domo zege.

Mwanaspoti: Una mpango wa kuoa lini?

Sholo Mwamba: Mpango upo, ila kwa sasa nakomaa kukuza muziki wangu utusue zaidi.

Mwanaspoti: Vipi kuhusu tuhuma za ushirikina?

Sholo Mwamba: Ni kawaida katika muziki kupata tuhuma za ushirikina na hasa ukiwazidi wenzako, hivyo sishangai kuambiwa natumia ndumba.