Shilole aingia ukumbini na wimbo wa Mwanaume Mashine

Muktasari:

Harusi ilihudhuriwa na wanamuziki Diamond Platnumz, Hamornize, Wolper, Vanessa Mdee, Jux, Joketi, Dogo Janja na Irene Uwoya

Dar es Salaam. Hatimaye ile sherehe ya harusi ya msanii wa Bongo Fleva, Shilole na mume wake Ashrafu Uchebe iliyokuwa inasubiriwa kwa shauku kubwa  baada ya kufunga ndoa Desemba 6 mwaka jana,sasa imefanyika usiku wa kuamkia jana Hekima Gardern Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Katika Sherehe hiyo Shilole aliwashangaza watu waliohudhuria katika sherehe hiyo baada ya kuingia ukumbini na Muziki wa Singeli na wimbo wa 'Mwanaume Mashine".

Shilole alionekana kuufurahia huo wimbo kutokana na kuucheza kwa mbwembwe wakati anaingia ukumbini, hadi wakati mwingine alikuwa anajisahau kama yeye ni bi harusi kwa kuonyesha nyoga zake za kwenye Jukwaa, lakini watu wake wa karibu walimfuata na kumstua apunguze mapepe kidogo.

Wakati huo akifanya mbwembwe hizo ;mume wake Uchebe alikuwa akimfuatilia kwa nyuma huku akionyesha tabasamu na watu wa ukumbini walikuwa wakishangilia na kusema Uche mashine...Uchebe mashine.... hadi walipoenda kukaa kwenye sehemu yao waliyoandaliwa.

Mwanaspoti ilipata kuzungumza na Shilole kwanini amechagua wimbo wa Mwanaume Mashine kuingia nao ukumbini, alisema amependa kutokana na kufikisha ujumbe kwa wahusika.

"Unajua kwanza nilitaka niwe tofauti na baadhi wa watu wengine wanaoingiaga na nyimbo zinazofanana au za staili nyingine, na pia ni kutaka kufikisha ujumbe kwa wahusika ambao wanapenda kumchambua mume wangu Uchebe katika mitandao ya kijamii, hivyo wajue mwanaume siyo sura  wala kuendana, na mambo mengine wanayoyasemaga.

"Pili ni wimbo ambao naupenda unachezeka na kuchangamka na ukizingatia mie napenda sana Singeli"alisema Shilole.

 Sherehe hiyo ya harusi ilihudhuriwa na mastaa mbalimbali kama Diamond Platnumz, Hamornize, Wolper, Vanessa Mdee, Jux, Joketi, Dogo Janja na Irene Uwoyo pamoja na watu wengine wengi.