Sherehe ya Banda ilinoga kinoma

NDO kashachukua chake bana. Nyota wa kimataifa wa Taifa Stars na Baroka FC ya Ligi Kuu Afrika Kusini, Abdi Banda, amemalizia shughuli yake ya sherehe ya harusi na mkewe Zabibu Kiba katika ukumbi wa Tanga Beach Resort.

Awali sherehe ya harusi ya wawili hao kwa upande wa mwanamke ilifanyikia jijini Dar es Salaam na baada ya hapo ikahamia Tanga upande wa kiumeni.

MAMBO YALIANZA HIVI

Asubuhi kabla ya maandalizi ya shughuli yenyewe, nyota huyo alikwenda kutembelea kituo chake cha Banda Football Academy na kuwapa hamasa chipukizi walioko katika kituo hicho kwa lengo la kufanya vyema kwenye safari yao ya kisoka.

Hata hivyo, huko hakukaa sana na akahamia kwenye maandalizi ya ukumbini kwa ajili ya sherehe hiyo iliyowaacha atu vinywa wazi kwani maandalizi yake yalikuwa babu kubwa.

MAMA BANDA AFUNGUA SHEREHE, KIBA AAMSHA SHANGWE

Mama mzazi wa Banda, Bi Mwanahawa Mwalimu, ndiye aliyefungua sherehe kwa kuanza kuingia ukumbini kisha akafuatiwa na wageni wengine upande wa bibi harusi.

Bi Mwanahawa aliingia ukumbini hapo akionekana mwenye furaha na asiye na wasiwasi wowote huku akionyesha madaha yake. Baada ya kuingia, alifuatiwa na wazazi wa Zainab na kubwa zaidi ni baada ya kaka zake bi Harusi, Abdu na Ali Kiba, kuingia ukumbini hapo na kuamsha shangwe kwa wageni waalikwa wote waliojitokeza katika ukumbi huo.

ZABIBU ATOA CHOZI UKUMBINI

Kama ilivyo kawaida, upande wa kiume ndio huwa wa kwanza kutambulisha ndugu na jamaa zake. Ndivyo ilivyokuwa katika sherehe hiyo baada ya Banda kutoa utambulisho huo kwa mama yake na baba yake mdogo. Baba yake mzazi alishindwa kuhudhuria sherehe hiyo kutokana na kuwa na udhuru.

Ndipo ikaja upande wa pili, Zainab aliposimama na kutambulisha ndugu zake, hata hivyo mara tu alivyomtambulisha mama yake, alishindwa kujizuia na kujikuta akitokwa na machozi ya furaha, kabla ya Ali Kiba kumpokea na kuendelea na utambulisho huku akidai, kulia ni kawaida ya mdogo wake huyo, hivyo ameamua kumalizia alipoishia kama kaka wa kwanza.

KAMATI YAONGOZWA NA WAZIRI

Sio mchezo. Unafikiri ni nini kinaharibika hapo. Kama tunavyojua, waziri ni msimamizi mkuu wa wizara husika ndani ya serikali yoyote kumsaidia Rais majukumu yake. Sasa fikiria usimamizi wa waziri kwenye shughuli kama hii. Utapenda.

Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye ni mama mdogo wa Abdi Banda, ndiye aliyekuwa akiongoza wanakamati wa shughuli hiyo na alihakikisha kila meza inameremeta kwa chakula na vinywaji.

Mambo yalikwenda kama kama yalivyopangwa kwani hakuna meza iliyokosa chakula na vinywaji vilikuwa vya kila aina na watu walikunywa kwa wingi.

CHAKULA USHINDWE MWENYEWE TU

Si unajua Tanga kwa misosi ndio kwenyewe. Sasa unafikiria nini kwenye mambo kama hayo? Usipime unaambiwa. Kwa waliokuwepo huko, walifaidi hadi kusaza.

Kama ilivyozoeleka katika sherehe nyingi, huwa kuna muda maalumu wa chakula na mara nyingi huwa ni katikati au mwishoni mwa shereh. Sasa unaambiwa kwenye sherehe ya Banda, hayo mambo hayakuwepo, chakula kililiwa mwanzo mwisho, yaani watu walikuwa wanakula huku ratiba nyingine zikiendelea.

WAGENI WAPIGA SALUTI

Wageni wote waliojitokeza ukumbini hapo walionekana kuipiga saluti sherehe hiyo kwani walikula mpaka wakasaza.

Mmoja ya wageni waalikwa aliyejitambulisha kwa Jina la Abdul Juma, Mkazi wa Barabara ya Tatu, jijini hapa alisema katika sherehe hiyo hakuna kupeleka neno la ovyo nje ya ukumbi.

“Kwa hiki kilichotokea hapa kiukweli hata kama kulikuwa na watu wamekuja kwa ajili ya kuangalia wapi wamekosea, wameumbuka, vyakula watu wamekula na kurudia na vinywaji bado vipo kama hivi na wote wamevipa kisogo, hili sio jambo dogo,” alisema.

VIONGOZI WA SERIKALI NDANI

Viongozi wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawakumwacha Bi Ummy peke yake katika shughuli ya mtoto wake, bali nao walijitokeza ukumbini hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela na wabunge Dadi Rajabu (Muheza), Kassim Magige, Mbunge wa Viti Maalumu (Arusha) nao walikuwepo.

Pia walikuwepo Wakuu wa Wilaya Godwin Gondwe (Handeni), Thomas Mwilapa (Tanga), Sele Boss ambaye ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga na Zainab Abdallah (Pangani). Pia walikuwepo madiwani pamoja na wafanyakazi wastaafu wa Serikali.

KIBA AMWAGA NASAHA KWA WANANDOA

Ikiwa ni miezi michache tu imepita tangu Ali Kiba afunge ndoa iliyokuwa ya kifahari, msanii huyo aligeuka kuwa mtoa nasaha kwa wanandoa katika sherehe hiyo.

Alifanya hivyo ikiwa ni baada ya kusimamia shughuli nzima ya ndoa hiyo iliyofungwa jijini Dar es Salaam.

Katika nasaha zake hiyo, Kiba aliwaambia wanandoa hao ndoa ni neno dogo sana lakini lina maana kubwa pale utakapoanza kulichanganua, kabla ya kumgeukia mdogo wake na kumwambia anapohisi amekosea asisite kuomba samahani, hata ikitokea siku wamegombana wasikubali wakalala bila kuombana msamaha.

“Msije mkafanya hivyo hata siku moja, mmegombana asubuhi basi hadi inafika jioni mnakuwa bado hamjamaliza tatizo, haipendezi na Zabibu unapojua umekosea jitahidi kuwa mpole na kumwomba msamaha mumeo,” alisema.

Kiba alikumbushia enzi ambayo walikuwa wakimtengeneza mdogo wao katika msingi bora wa dini na kumkumbusha kwa kumwambia hayo ndio matunda yake.

“Tulipokuwa tunakuambia usitembee kichwa wazi inawezekana ulikuwa unaona kama tunakosea, lakini naamini leo ndio unaona matunda, hakuna mwanamume anayetaka kula embe lenye vumbi tena la juu juu, lazima atake embe la kulitafuta kwenye matawi,” alisema.

Kauli yake inaonekana kuendana na alichofanya yeye kwani baada ya awali kuhusishwa na wanawake wengi kimapenzi, baadaye aliamua kwenda kumuoa Bi Amina kule Mombasa, Kenya, hivyo hilo lilikuwa kama ni fumbo pia kwa upande wa wanawake aliotembea nao.

Kiba alimalizia kwa kuwasihi wanandoa hao wote kuheshimiana na kuwatakia kila la kheri katika maisha yao.

“Maisha ya ndoa ni baraka kutoka kwa mwenyezi Mungu, hivyo mnapaswa kuilinda baraka hii,” alisema.

MPOTO AKOSHA WAGENI, AMWAGIWA NOTI

Sherehe yoyote lazima iwe na burudani. Sasa unaambiwa katika sherehe hiyo, ilialikwa bendi ya kutumbuiza wageni ikipiga live na kuvutia wengi ukumbini hapo.

Kubwa zaidi ni msanii Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ alipoanza kuimba wimbo wake mpya wa Ndoa alioufanya na msanii Hermonise, kwani alikuwa akitoa maneno yenye mashiko na kuwafanya watu wote kwenye sherehe kuangua vicheko.

Mpoto alisema anatambua Kiba kaongea maneno mazuri kwa wanandoa lakini yeye kupitia wimbo huo atakuwa anatoa maneno yanayoishi.

Baada ya kuona anaimba lakini hatunzwi, yeye mwenyewe akiwa mbele ya ukumbi alianza kuwataja viongozi kwa majina na kuwataka wamtunze.

“Naona hamnitunzi eeh sasa naanza kutaja kwa majina na sitaki mniangushe, lakini hizi mtakazonitunza hapa zinabidi ziwe nyingi kuliko ile hela tuliyokubaliana,” alisema msanii huyo kwa kutania.

Pia Mpoto alishindwa kuficha hisia zake kwa Kiba na kujikuta akisema ni kati ya wasanii wanaoelewa nini wanakifanya katika muziki.

“Nisiwe mnafki, kiukweli Kiba ni msanii ambaye anaelewa nini anakifanya katika tasnia hii na napenda kumpongeza kwa hilo,” alisema.

Wasanii wengine waliokuwepo ukumbini hapo ni Abdu Kiba, Mwana Fa na Lulu Diva.

ULINZI USIPIME AISEE

Katika harusi nyingine huwa kunakuwa na wale wazamiaji, lakini kwa Banda hiyo haikuwepo.

Hata kama ulikuwa unataka kufanya tukio baya, ilikuwa ni ngumu kutokana na ulinzi uliokuwa umeimarishwa kuanzia getini mpaka ndani.

Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania walikuwa kila kona katika ukumbi huo na hivyo kuimarisha usalama. Mbali ya Polisi hao pia walikuwapo wana usalama wengine kibao tu.

APEWA ZAWADI NZITO

Wakurugenzi wa Mkwabi Super Market, wamempa ofa kali mchezaji huyo baada ya kumwambia atakuwa huru kufanya manunuzi ya bure katika duka lao.

Zawadi hiyo ilitangazwa na MC kuwa mchezaji huyo amepewa zawadi hiyo kwenda kufanya shopingi hiyo muda wowote kuanzia sasa.

MAISHA MAPYA YANAANZIA SAUZI

Baada ya Shughuli kumalizika Mwanaspoti lilibahatika kufanya mahojiano ya dakika chache na Banda kutaka kufahamu kama anaondoka na mke wake au anamuacha.

Banda alisema anatakiwa arudi Afrika Kusini kujiunga na wenzake, hivyo ataondoka na mkewe ili kuanza maisha mapya.

“Ligi kule imeshaanza na kuna mechi Jumatatu, kwa hiyo inabidi nirejee ili nijaribu kuiwahi mechi ya Jumatano kule na wenzangu na ndio maana nataka niondoke na mke wangu,” alisema.

Banda aliongeza ataondoka na ndege kwenda Dar es Salaam (Jumapili), baada ya hapo ataunganisha na mkewe kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya maisha mapya.