Rich Mavoko asafiria nyota ya Diamond

Friday July 28 2017

 

By THOBIAS SEBASTIAN

MSANII wa kizazi kipya Rich Mavoko June 2, aliingia mkataba na lebo ya Wasafi na kuanza kufanya kazi chini ya lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platinamzi.

Tangu ajiunge na lebo hiyo, Mavoko ameachia nyimbo tatu mpaka sasa ambazo ni  ‘Imebaki Story’, ‘Kokoro’ aliyomshirikisha Diamond Platinamz na ‘Sheli’  ambao ni mpya aliomshirikisha Fid Q.

Kabla ya kujiunga na kundi hilo, Mavoko  ni kama alikuwa ameshapotea lakini tangu ajiunge na lebo hiyo mambo yamekuwa safi na amezidi kupanda chati kila kukicha.

Msanii huyo anayefanya vizuri kwa sasa chini ya lebo hiyo, awali alikuwa akifanya video zilizoonekana za kawaida, lakini ni kama lebo hii imempa shavu kwani  video zake tatu alizotoa hadi sasa, zote zinaonekana kali na zilizotumia pesa nyingi kuzitengeneza tofauti na zile alizotengeneza kabla ya kujiunga na Wasafi.

Hata hivyo, Mavoko ameweza pia kupenya katika biashara kwani hapo awali ilikuwa si rahisi nyimbo zake kuchezwa nje ya mipaka ya Tanzania, pamoja na kupata shoo nyingi, tofauti na sasa chini ya lebo hiyo, mambo yamebadilika na amekuwa akipata shoo nyingi na hata video zake  kupata nafasi ya kuchezwa kwenye vituo vya runinga vya nje ya nchi.

Msanii huyo pia anafanya vizuri mitandaoni nyimbo zake zikitazamwa na watu wengi. Mpaka sasa wimbo wa Imebaki Story’ umetazamwa na watu 3,696,036, Kokoro (2,734132) na hii ya sasa Sheli (170,000).