Rayvanny kaamua kufunguka WCB

Muktasari:

  • Amesema kuwa ndani ya label hiyo huwa wanafanya mambo kwa maelewano na kwamba, hawajawahi kufikia hatua ya kupishana kauli.

HUKO WCB hakuna jambo dogo kila kitu kinawekwa kwenye mstari ili kuhakikisha mambo yanasonga. Staa wa kundi hilo mwenye sauti matata, Rayvanny amefichua kuwa hajawahi kutofautiana na mabosi zake akiwemo Diamond.

Amesema kuwa ndani ya label hiyo huwa wanafanya mambo kwa maelewano na kwamba, hawajawahi kufikia hatua ya kupishana kauli.

Akichonga na Mwanaspoti jana, Rayvanny amesema mara nyingi yanapotokea mambo huyafanya kuwa ya kawaida ingawa kuna mengine huonyesha kutopendezwa nayo.

“Nikikosea lazima anikoromee, lakini kunikoromea hajawahi kwa sababu Diamond sio mtu wa kufokafoka, lakini kitu akikukataza unajua hiki kitu hajakipenda. Lazima ujiongeze ili mambo yaende sawa,” Rayvanny.

Rayvanny na Diamond wameshafanya ngoma kibao pamoja ikiwemo Salome, pia wamekutana katika ngoma ‘Zilipendwa’ ambayo iliwakutanisha wasanii wote walio chini ya WCB.

Aidha, Rayvanny amekanusha uvumi kuwa ndani ya WCB anayependwa zaidi ni msanii mwenzake, Hamornize.

“Habari hizo sio za kweli tena zipuuzieni kabisa, Diamond anawapenda wasanii wake wote katika lebo ya WBC hana ubaguzi,” alisema.