Prince Dully katisha bana

Friday November 10 2017

 

By RHOBI CHACHA

ASIKWAMBIE mtu, mtoto wa tatu wa Diamond Platinumz, Abdul (Dylan) amekuwa maarufu pengine kuliko hata ndugu zake wengine waliozaliwa na Zari.

Prince Dully ambaye amezaliwa Agosti 8, 2017 baada ya uhusiano wa siri kati ya Diamond na Hamisa Mabetto tangu kuzaliwa kwake amekuwa gumzo hata kama mwenyewe bado hajajua kinachoendelea duniani dhidi yake.

Sio kuwafunika ndugu zake tu, Dully ambaye mashabiki wanapenda kulitumia jina alilopewa na mama yake yaani Abdul kuliko lile la baba yake Dylan,  amewakimbiza hata watoto wengine na mastaa kibao wa Kibongo. Dogo huyo juzi Jumatano alitimiza miezi mitatu tangu kuzaliwa kwake anaenda sambamba na umaarufu wa wazazi wake hasa kwenye mitandao ya kijamii na

Mwanaspoti inakuletea mambo kadhaa yaliyosababisha mtoto huyo kuwa staa ghafla akienda sambamba na wazazi wake.

KABLA YA KUZALIWA

Ikumbukwe kuwa kwa muda mrefu Diamond alikuwa akitoka kimapenzi na muuza nyago huyo wa video za muziki, japo walikuwa wakifanya siri.

Inaelezwa kuwa licha ya kutoka na mademu wengine, Diamond kwa Hamisa ilikuwa ni kama mate na ulimi na tetesi za kuendelea kula bata zilianza mapema na hata mwanadada huyo alipoonekana yu mjamzito Diamond alitajwa.

Hivyo mimba ya kichanga hicho ilianza kuwa gumzo na kujadiliwa kuliko hata watoto wawili wa Diamond aliozaa na Mganda, Zarinah Hassan a.k.a Zari.

UTATA WAIBUKA

Katika jambo zuri kama hilo hasa kwa staa kama Hamisa, wapo ambao hawakufurahishwa nalo. Wakaibuka watu na kuzusha mwenye baba kila kukicha na wengine walikuwa wanamuhisi ni Diamond huku wengine wakisema eti mimba hiyo haikuwa ya Diamond.

Yakaandikwa mambo mengi na kuwafanya wazazi, ndugu na marafiki wa msanii huyo kubaki njia panda. Wakati hayo yakitokea, Diamond na ndugu zake waliziba masikio.

Matashititi ya Hamisa yakaendelea na zaidi ya yote alianza kujiita Mama Dee, hapo watu ndio wakaanza kufunguka kuwa mimba itakuwa ni ya Diamond.

HAMISA ALIPOJIFUNGUA

Wakati huo minon’gono ikiendelea kuwa mtoto ni wa Diamond huku familia ya Diamond na Diamond mwenyewe wakiendelea kukataa kuwa hawahusiki na mtoto huyo.

Lakini siku mtoto alivyozaliwa, Mama Diamond, Bi Sandra, dada wa msanii huyo, Esma na mama wa DJ Romjs ambaye ni mdogo wa mama Diamond, walienda hospitalini kinyemela kumuona mtoto wa Hamisa.

Huku wakiwa hawajui shilawadu kama wanawafuatilia kila kukicha, ndipo wakanaswa na kurushwa katika mitandao lakini bado walikuwa wakipigiwa simu wanaendelea kukata kuwa Diamond hausiki na mtoto wa Hamisa.

VIDEO YAWAUMBUA

Mama Diamond baada ya kukataa kuwa mtoto sio wao na kujikuta picha zao wakiwasili hospitali zimeonekana, walijitetea kuwa walienda hospitali kumuona Hamisa kama mtu wao wa karibu.

Majibu hayo hayakumpendeza Hamisa, ambapo siku mbili zilizofuata Hamisa akavujisha video na picha akiwa na Diamond kitandani.

DIAMOND AKIRI

Tetesi ziliendelea hata alipojifungua mtoto huyo na hazikupita siku nyingi kila kitu kilikuwa hadharani baada ya Diamond kuvunja ukimya akikiri kwamba ni kweli yeye ndiye mhusika wa mtoto aliyejifungua Hamisa.

Kujitokeza kwa Diamond kukiri kuzaa na Hamisa ndipo kulikozaa ustaa wa Dully kwani vurugu za kuitangaza mimba hiyo ilivyokuwa hazikuwa za kitoto kwa Hamisa japo alikuwa anamficha baba wa mtoto.Hapa ndio alipoanza kuzungumziwa sana Dully hadi kufikia hatua ya kuundwa timu za mashambulizi kwa Hamisa juu ya mtoto wake na Zari juu ya Diamond kuzaa na Hamisa.

AROBAINI YA DULLY

Ikafika siku ya 40 ya Dully, lakini Hamisa aliamua kuifanya kimya kimya na hata ilipofika siku ya pili baadhi ya watu walijua wataweza iona sura ya Dully katika mitandao, lakini haikuwa hivyo hadi baba yake alipoionyesha siku ya  kuweka wazi ndio akaanza kuposti sura ya mtoto huyo.

Dully alizidi kupata umaarufu baada ya watu kugundua kuwa, katika 40 yake amehudhuria babu yake ambaye ni baba wa Diamond, kitu ambacho tangu Diamond apate watoto wake wale wawili Tiffah na Nillan, baba mzazi wa staa huyo hakuwahi kuhudhuria katika 40 zao.

AKICHAFUA INSTAGRAM

Mara baada ya 40 ya kichanga hicho kufanyika, Dully alifunguliwa ukurasa wake wa Instagram na kwa siku moja tu akawa na followers ‘wafuasi’ kibao. Jambo hilo lilimfanya awe gumzo kwani aliwafunika hata baadhi ya mastaa.

Na katika ukurasa wake huo wa Instagram, umekuwa kila wakati anabadilishiwa wasifu na jina. Kuna wakati anasomeka Abdul Diamond, mara Abdul Plutnum na wakati mwingine anaweka jina la Dylan alilolitoa Diamond.

Mbwembwe hizo hazikuishia hapo mara amposti Diamond na kusema ‘True my father’ hadi watu wakaanza kusema mtoto kaanza kuwa na akili ya kuandika akiwa na ametimiza 40, kumbe muandikaji wa yote hayo ni mama mtu, Hamisa.

HAMISA vs ZARI

Ukurasa huo wa Dully ulisababisha kuibuka kwa vijembe baada ya Hamisa

kupitia ukurasa huo  wa mtoto wake kumuomba urafiki Tiffah na hapo ndipo Zari alipocharuka na kusema hataki watoto wake kufuatwa fuatwa na kuwekwa karibu na mtoto wa Hamisa. Kazi ikaanza kwa wawili hao kurushiana maneno.