Nyamayao: Naipenda sana nchi yangu, naitangaza

Muktasari:

Anasema ukiacha mambo binafsi, lakini kwa kuigiza ndani na nje ya nchi ameweza kuitangaza Tanzania, mavazi ya nyumbani na zaidi lugha ya Kiswahili akiamini ni kati ya bidhaa muhimu kwa sasa katika ajira za kimataifa kwa vijana wengi.

HAPPINESS Stanilaus ‘Nyamayao’ ambaye ni miongoni mwa waigizaji nyota katika tasnia ya filamu nchini, anasema kipaji chake kimemsaidia kujua mambo mengi ya ulimwengu huu na pia kumwongezea uzalendo kwa Tanzania.

Anasema ukiacha mambo binafsi, lakini kwa kuigiza ndani na nje ya nchi ameweza kuitangaza Tanzania, mavazi ya nyumbani na zaidi lugha ya Kiswahili akiamini ni kati ya bidhaa muhimu kwa sasa katika ajira za kimataifa kwa vijana wengi.

“Tunapokuwa nje ya Tanzania upendo unaongezeka wa kuipigania nchi, nimekuwa nikifanya hivyo kule China,” alisema na kuongeza yupo nchini kwa sasa katika likizo fupi, pia kwa ajili ya kazi maalumu ya kuingiza sauti katika tamthilia mpya.

Nyamayao anajivunia nafasi yake ya uigizaji kuwa imempatia ajira nyingine kwa njia ya kuigiza kwa sauti tu, pia msanii huyo anasema wakiwa nje wanajitahidi sana kuvaa mavazi ya Kiafrika kwa ajili ya kutangaza utamaduni Tanzania.