Nakukumbusha tu hawa ndo wapiga pesa kupitia posti zao Instagram

Monday March 12 2018

 

IKIANZISHWA mwaka 2010 na kisha kununuliwa na Facebook kwa Dola 1 milioni mwaka 2012, Instagram imejipatia umaarufu mkubwa na kuwa mtandao wa kijamii wa kijanja unaowaingizia watu mkwanja kibao.

Kuna watu maarufu duniani wametumia kurasa zao za Instagram kupiga pesa kiulaini kutokana na posti zao wanazotuma kwenye mtandao huo.

Lebron James – Dola 120,000 kila posti

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, staa wa mpira wa kikapu, Lebron James ana zaidi ya wafuasti 35.8 milioni na hilo limekuwa mtaji kwake kutokana na kuvutia kampuni mbalimbali zinazohitaji kutumia mtaji wake wa watu aliokuwa nao kufanya matangazo ya kibiashara.

Kutokana na hilo, King James ameripotiwa kuchaji kila posti ya tangazo anayotuma kwenye ukurasa wake Dola 120,000.

Mtu mwingine maarufu anayechaji kwa kiwango kama hicho cha posti zake anazotuma kwenye mtandao huo wa Insta ni mrembo Gigi Hadid, ambaye anaripotiwa kuwa na wafuasi wanaozidi 38.8 milioni.

Cara Delevingne – Dola 150,000 kila posti

Amekuwa maarufu kutokana na kufanya vizuri kabisa kwenye filamu. Moja ya filamu zake maarufu ni ile ya Suicide Squad aliyocheza mwaka 2016 na tangu hapo amejitengenezea wafuasi wengi kwenye mtandao huo wa kijamii kufikia zaidi ya watu 41 milioni.

Kitendo hicho kimekuwa mtaji na kumfanya mrembo Cara kuchaji kila posti anayotuma kwenye ukurasa wake kuwa ni Dola 150,000. Ni miongoni mwa wasanii wanaopiga pesa ndefu kwa kupitia posti wanazotuma kwenye Instagram.

Kourtney Kardashian – Dola 250,000 kila posti

Mrembo matata kabisa kutoka kwenye familia ya Kardashian. Kourtney ameripotiwa kuwa na wafuasi wanaozidi 61.3 milioni kwenye ukurasa wake wa Instagram na jambo hilo limemfanya ajikusanyie dili kibao za kibiashara na kila posti sasa atakayoposti kwenye ukurasa huo anachaji Dola 250,000. Mrembo mwingine anayevuna pesa kama hiyo kuchaji Dola 250,000 kwa kila posti anayotuma kwenye ukurasa wake wa Instagram ni ndugu wa Kourtney, mrembo Khloe Kardashian, anayeripotiwa kuwa na wafuasi wengi wanaoanzia 73.5 milioni.

Kendall Jenner – Dola 370,000 kila posti

Mrembo Kendall Jenner ni mmoja watu wanaopiga pesa ndefu kupitia posti zao wanazotuma kwenye kurasa za Instagram. Akiwa na wafuasi wanaozidi 88.1 milioni jambo hilo limekuwa mtaji mkubwa kwa sababu limemfanya akaribishe dili nyingi za kibiashara na hivyo kila posti anayotuma kwenye ukurasa wake huo anachaji Dola 370,000.

Hiyo ni pesa anayovuna kiulaini. Staa mwingine anayepiga pesa ndefu ni Kylie Jenner, ambaye kila posti yake anayotuma kwenye ukurasa wake wa Instagram anachaji Dola 400,000 kutokana na kuwa na wafuasi wanaoanzia 105 milioni.

Kylie ana dili za kampuni kama nane tofauti zinazotangaza kupitia ukurasa huko.

Cristiano Ronaldo – Dola 500,000 kila posti

Ndiye mwanasoka pekee kwenye orodha ya mastaa wanaopiga pesa nyingi kwa kutumia Instagram.

Ronaldo na wafuasi wanaoanzia 121 milioni na jambo hilo limemfanya kuwa na mtaji mkubwa wa watu wanaomfanya azivute kampuni mbalimbali kuweka matangazo yao kwenye ukurasa huo. Ripoti zinafichua kwa kila posti anayotuma Ronaldo basi anachaji Dola 500,000.

Staa mwingine anayevuna kiasi kama hicho cha Dola 500,000 ni Kim Kardashian, mwenye wafuasi wanaoanzia 108 milioni kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kim amevutia kampuni zaidi ya nane zinazotangaza kupitia ukurasa wake huo wa Instagram.

Selena Gomez– Dola 550,000 kila posti

Umri wa Selena ni miaka 25, lakini mzigo wake wa pesa anazopiga ni wa maana kweli kweli.

Selena anawaongoza mastaa wote kwa kuvuna pesa nyingi kupitia posti zake anazotuma kwenye Instagram na mtaji wake wa wafuasi 134 unamfanya kuvutia kampuni nyingi kuwekeza kupitia staa huyo.

Kutokana na hilo, Selena kwa posti yoyote ya tangazo atakayotuma kwenye ukurasa wake wa Instagram, anachaji Dola 550,000.