Nafsi ya mtu mzima ndani ya Lulu mtoto

Muktasari:

  • Kama jina la wimbo unavyoweza kulitafsiri jina la wimbo kuwa “Majaribu na mataabiko”, Rapa wa Uingereza, Ramson Badbonez, anasema amekua huku akijihisi kama nafsi ya mtu mzima ilitegwa ndani ya kiwiliwili cha mtoto.

NAPENDA mstari wa kwanza wa wimbo “Trials and Tribulations”, unasikika: “Growing up I felt like an old soul trapped in a child’s body.”

Kama jina la wimbo unavyoweza kulitafsiri jina la wimbo kuwa “Majaribu na mataabiko”, Rapa wa Uingereza, Ramson Badbonez, anasema amekua huku akijihisi kama nafsi ya mtu mzima ilitegwa ndani ya kiwiliwili cha mtoto.

Aliyoyashuhudia na kuyakabili akiwa mtoto mdogo ndiyo ambayo yanamfanya Badbonez ajihisi alikuwa na nafsi ya mtu mzima tangu alipokuwa mtoto mdogo. Kwamba nafsi ya mtu mzima ilitegwa ndani ya mwili wake akiwa mtoto.

Elizabeth Michael ‘Lulu’ ni msanii aliyehitaji utambulisho ndani ya Bongoland. Jina lake ni kubwa. Kazi zake zimempa thamani na mikasa yake imemfanya awe gumzo lisiloisha kama tamthiliya ya Isidingo.

Mikasa ikawa sehemu ya maisha ya Lulu tangu akiwa na umri wa mtoto. Ni mikasa hiyo iliyozua janga. Matokeo ya jumla yakawa ni Lulu kuishi mahabusu kwa muda mrefu kabla ya kuachiwa kwa dhamana kisha kufungwa jela.

Mstari wa Badbonez unamhusu sana Lulu. Kwamba nafsi ya mtu mzima inaweza kuwemo kwenye mwili wa mtoto mdogo. Na ifahamike kuwa mazingira ya kimaisha, wingi wa vishawishi na tamaa, kwa pamoja ni chanzo cha baadhi ya watoto kumiliki nafsi za watu wazima.

Watoto wa kike na kiume wanaweza kuwa na nafsi za watu wazima kwa sababu za kimajukumu. Zipo familia nyingi tu, watoto wanaachwa yatima, hivyo inabidi waamue kujilea na hata kulea wadogo zao. Wapo watoto wanatumika vibaya na wazazi. Wanatumwa kutafuta fedha, matokeo yake wanageuka ombaomba au wanakuwa waathirika wa ajira za utotoni. Kuna watoto wa kike wanaelekezwa kwa wanaume wakubwa wapate pesa.

Vipo pia vishawishi vya kimapenzi. Kwa watoto wa kiume kesi ni chache, kwa wa kike ni nyingi. Wanaume watu wazima kuamua kuwashawishi watoto wa kike kwa hadaa za kila aina na matokeo yake kuwafanya kuwa wapenzi wao.

Katika makundi yote hayo, changamoto ya kimalezi haikwepeki. Kimsingi kuna watoto wanavaa nafsi za utu uzima kwa namna chanya. Hao ni mashujaa. Wengi nafsi za utu uzima huwaingia katika namna hasi na matokeo huwa mabaya.

UTU UZIMA WA LULU

Kabla Lulu hajalivaa janga la kuhusika na kifo cha aliyekuwa fundi wa filamu wa Bongo Movie, Steven Kanumba, tayari alishabainika kuwa na mwenendo wa ovyo. Kulewa hadi kuzimika akiwa katika mavazi tata klabu. Mara kuhusika kimapenzi na watu aliotakiwa kuwaita wajomba zake.Ikawa hadithi mwisho ikabainika ni kweli. Ukweli nao ukadhihirika wakati wa janga. Kwamba kumbe Kanumba naye akawa mpenzi wa Lulu. Hata mazingira ya kifo cha Kanumba ni ugomvi wake na Lulu. Ugomvi wenyewe ni wivu wa mapenzi.

Mahakama ilielezwa kuwa Kanumba alihisi Lulu si mwaminifu. Yaani Lulu si tu kwamba alikuwa ameingia kwenye mapenzi katika umri mdogo, bali alikwenda mbele zaidi na kuonesha vitendo vilivyomtia ‘wazimu’ Kanumba kuona mwenzake ni macho juu, hivyo wakaingia kwenye ugomvi uliosababisha roho iache mwili. Kimsingi tukio la Lulu na Kanumba lina mafundisho mengi ndani yake. Kwa wazazi kulea vizuri watoto wao. Kuwakinga na vitendo vitakavyowafanya wawe na nafsi za utu uzima wakiwa bado watoto. Ni darasa kuhusu kuwa na mzani kwenye wivu wa mapenzi. Inaelekeza wanaume kutambua kwamba, mtoto ni mtoto tu.

Inawezekana kumfanya mtoto kuwa mpenzi wako na ukadumu kwenye siri. Hata Kanumba na Lulu walifanya siri. Tatizo ni kuwa siri ilivuja vibaya. Mmoja akawa marehemu, mwenzake akaingia kwenye tuhuma za kuhusika na kifo chake.

Mwisho kabisa, hata Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu, alipokuwa anasoma hukumu ya Lulu, Novemba 13, mwaka jana, alisema kuwa Lulu alijinyima upendeleo wa kitoto kwa vitendo vyake. Kwamba alikuwa akiitwa mke na Kanumba naye aliitika. Wakati huo alikuwa na miaka 16 tu.

“Mshitakiwa amekiri mahakamani kuwa yeye na marehemu walikuwa wapenzi. Kama mtoto ana uwezo wa kufanya mambo ya kiutu uzima akafanikiwa basi tutegemee iko siku Mahakama hii atafanya mambo ya kitoto na kuombwa alindwe,” alisema Jaji Rumanyika.

KILIKUWA KIKOMBE

Kipindi hiki Lulu akiwa ametoka jela na kupangiwa kuendelea na adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili akiwa nje, kinatuleta kwenye muktadha kwamba tukio la Kanumba kwa namna lilivyostaajabisha, basi kilikuwa kikombe ambacho ilikuwa lazima Lulu akipitie. Mwanamuziki wa Injili nchini, Martha Mwaipaja, kuna wimbo wake anaimba majaribu ni kikombe ambacho mja aliyepangiwa lazima akipate. Hivyo, Lulu kwa namna Kanumba alivyokuwa, itoshe kusema kile kilikuwa kikombe na amekipitia.

Tukio la Lulu, pia hunikumbusha kisa cha binti mrembo mno, Maeghan Rice ambaye yupo anatumikia kifungo cha maisha jela kwenye Gereza la Arizona, Marekani, baada ya kukutwa na hatia ya kuua kwa kukusudia lakini bila maandalizi (second degree murder).

Maeghan akiwa na umri wa miaka 17, aliingia kwenye maisha yasiyofaa ambayo anayajutia leo. Ujumbe wake akiwa jela anasema: “I got involved with the wrong guy at a young age and I am paying the price.” Kiswahili: Nilijihusisha na mtu asiyefaa katika umri mdogo na sasa nalipia gharama.” Hiki alichokisema Maeghan ndiyo tafsiri ya methali; asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu.

Kama Maeghan, kilichomtokea Lulu ni matokeo ya kukutana na watu wasiofaa katika umri mdogo. Watu ambao badala ya kumuona mtoto, wao wakaona anakidhi maisha ya kikubwa. Lulu alianguka akiwa mdogo, sisemi analipa gharama, isipokuwa anakua ila katika mlango ambao si mzuri.

Tukio la Lulu kwa Kanumba, kwa lilivyotokea, lingeweza kumtokea mwanamke yeyote lakini bahati mbaya imekuwa Lulu, ambaye alikuwa mtoto. Utetezi wa Lulu mahakamani ni kuwa Kanumba alikuwa mwenye wivu wa kupindukia.

Binafsi nawezaje kupinga hilo la Kanumba na wivu? Mwaka 2011 niliandika makala (Ipo mitandaoni mpaka sasa), nikimshauri Kanumba kuhusu hulka zake za kupigana na wanawake. Usiku wa siku niliyoandika, Kanumba na swahiba yake, Vincent Kigosi ‘Ray’, walinipigia simu na kunishambulia.

Nilichomshauri Kanumba ni mlolongo wa matukio; aligombana na aliyekuwa girlfriend wake, Wema Sepetu. Ugomvi ukasababisha Wema avunje kioo gari la Kanumba. Kesi ilifika mpaka mahakamani. Kanumba aligombana na rafiki yake mwingine, Sylvia Shally, kesi ikafika polisi Oysterbay. Wakati huo alikuwa amegombana na msanii mwingine wa maigizo, Aunty Ezekiel, kisa kama mnavyojua.

Makala ilihusu maongezi na wanasaikolojia ambao walieleza aina ya matatizo kama aliyokuwa nayo Kanumba, sababu yake na suluhu. Kanumba hakupenda andiko, ndiyo maana yeye na Ray waliamua kunijibu kwenye simu, wakiwa pamoja.

Hata hivyo, nimekumbusha andiko hilo ili kuonesha kuwa Kanumba hakugombana na mmoja. Kifo chake hakikutokea alipogombana na Wema, Sylvia wala Aunty. Lilitokea kwa Lulu. Hapo inakupa tafsiri kuwa kilikuwa kikombe ambacho Lulu ilibidi akipitie.

Matukio ya Lulu na ukuaji wake wenye changamoto nyingi, ndiyo sababu ya kuwa na nafsi ya mtu uzima akiwa mtoto. Tumuombee amalize salama kifungo chake cha nje. Ni msanii mzuri, ana nyota. Bado anayo nafasi kubwa ya kuifaa sanaa na nchi yake.