Mwanamuziki Sir Nature, Harmorapa kuamsha popo Idd Mosi katika jiji la Mwanza

Friday June 23 2017

 

By Mwandishi wetu

Mwanamuziki Juma Nature (Sir Nature) na Harmorapa watapamba tamasha la muziki Raha ya Rocky City lililopangwa kufanyika wakati wa sikukuu ya Eid El Fitr  kwenye Ukumbi wa Buzuruga Plaza, Mwanza.

Sir Nature na Harmorapa wanatamba na wimbo wa Kiboko ya Mabishoo, naye muandaaji nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, P-Funk atashiriki katika tamasha hilo lililoandaliwa na kituo cha redio nyota ya kanda ya Ziwa, 102.5 Lake FM.

Mkurugenzi  Mkuu wa 102.5 Lake FM, Doreen Noni amesema kuwa maandalizi ya tamasha hilo lililopangwa kuanza saa 12.00 jioni yamekamilika na mashabiki wa muziki wa kizazi kipya watarajie burudani safi kutoka kwa wasanii mbalimbali mbali ya Sir Nature na Harmorapa.

Doreen alisema kuwa Nature na Harmorapa watafanya onyesho la kwanza ‘live’ kutambulisha wimbo wa Kiboko ya Mabishoo kwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa muziki huo wa mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.

“Harmorapa pia atatambulisha nyimbo zake mbalimbali kama, Nundu, Usigawe Pasi wakati Nature atawakumbusha mashabiki wake wa zamani  kwa nyimbo nyota za zamani kama  Ugali, Hili Game, Utajiju, Naja, Hakuna Kulala, Inaniuma Sana, Ubinadamu Kazi, Kighetogheto na Mgambo.

“Tamasha hili ni sehemu  ya kuadhimisha sikukuu ya Eid El Fitr, tumeandaa burudani mbalimbali ambazo hazita wachosha mashabiki, lengo ni kuleta msisimko wa aina yake kwa mashabiki wa Kanda ya Ziwa,” alisema Doreen.

Wasanii wengine watakaotumbuiza katika tamasha hilo ni Jimmy Chansa, Future JNL, kundi la Lakezonia, Ngeta na Dogo D, Abu Mkali,  vile vile kutakua na makundi ya kudans TYT na MCB pia jopo la warembo lukuki kutoka 21plus models na Blackfox models.

Mbali na hayo, pia kutakuwa a burudani safi ya muziki kutoka Ma-DJ wa 102.5 Lake FM.  Ma DJ hao deejays hao ni DJ Ten Ten, DJ Jabir, DJ Basta na DJ Steve wa Mitindo.