Msikie Beka anachosema kuhusu ngoma za Aslay

YAMOTO Band ni kama imepotea. Sasa wanaotamba ni Aslay na Beka Fleva kutokana na ngoma zao. Lakini, kwa sasa imefika hatua mashabiki wanawapambanisha wasanii hao, ambapo baadhi wanajiita timu Aslay na wengine timu Beka.

Mwanaspoti ilifanya mahojiano na Beka Fleva, ambapo alianza kwa kuzungumzia ushindani wake na Aslay ambao, unaofanywa na mashabiki wa muziki kisha akasema, mashabiki wengi wanakosea sana kufanya hivyo.

“Huwezi kumpangia shabiki kufanya jambo fulani, lakini sio vizuri kunipambanisha na Aslay, kwanza sisi ni ndugu na bado tunawasiliana na kuzungumza mambo mengi.

“Sina bifu na Aslay, sisi bado ni ndugu na pia watu wanaongea sana kwamba Aslay anavyofanya nyimbo nyingi, eti ananitisha mimi, kwa kifupi hanitishi sababu ndio utaratibu wake na mimi pia nina utaratibu wangu. Nafikiri watu wanaona kwa jinsi hali inavyokwenda,” anasisitiza ingawa amekiri muziki umekuwa na changamoto kubwa kwa sasa.

“Wakati tukiwa Ya Moto tulikuwa na nyimbo nyingi, lakini kwa sasa nipo peke yangu hivyo inanibidi nifanye kazi kwa bidii ili mashabiki wafurahi, inabidi pengine niachie ngoma nyingi kwa sababu nikienda kwenye shoo kuna changamoto kubwa ya kupafomu nyimbo zangu ni chache sana,” anaongeza msanii huyo, ambaye kama asingekuwa anaimba anakiri angekuwa mkulima wa mpunga.

ATARUDI YA MOTO?

“Binafsi sipo tayari kurudi tena, sababu kwanza kwa sasa nina uongozi mpya unaonisimamia pamoja hata na akina Aslay na wengine pia wana uongozi wao, sifikiri hilo linaweza kutokea. Kwa sasa ninasimamiwa na Siraji Issa, ambaye ndiye meneja wangu na John Sambila huyu ananisaidia sana katika masuala ya kifedha,” anaongeza

KUHUSU NYIMBO ZAKE.

“Nina nyimbo zaidi ya 19 mpaka sasa, zote nimetunga mwenyewe na hakuna ambayo kuna mtu kanisaidia kuandika ama kutia mkono,”

Pia aliongeza zaidi kuhusu video zake ambapo, anasema video ya Nibebe alifanyia Dar na Sikinai alifanyia mkoani Arusha.

SHOO AMBAYO HAWEZI KUSAHAU

“Kuna shoo siwezi kusahau ilikuwa Tanga kipindi hicho ndio tunawasha moto kweli kweli, nakumbuka ilikuwa Mwaka 2015, sasa kwenye huo ukumbi watu walijaa sana halafu viyoyozi vilikata aisee tupo tunapafomu pumzi ikawa inakata kabisa, halafu watu shangwe la kutosha.

“Ilitubidi tuombe kusimama kidogo ili tutoke nje kwenda kupata hewa ila nilikuwa najihisi kama nakufa halafu watu huku ndio hawana habari kabisa.”

PESA YAKE YA KWANZA ALIFANYIA NINI?

Beka anaendelea kufunguka kuwa pesa yake ya kwanza kabisa kuipata alituma nyumbani kwa ajili ya kukarabati nyumba yao.

“Nakumbuka ilikuwa 2.6 milioni ambapo nilipoipata tu, nilituma nyumbani ili warekebishe nyumba na mambo mengine ya kifamilia,”

KITU ANACHOJUTIA SANA

Beka anafunguka zaidi kuwa kitu anachojutia ni kuwahi kuyajua mapenzi jambo ambalo lilifanya kuharibu baadhi ya ndoto zake.

“Nakumbuka nikiwa nasoma kipindi hicho kuna msichana nilimpenda sana, lakini yeye alikuwa ananizingua nakumbuka alikuwa anaitwa Patricia,”

“Yaani yule demu alinipeleka sana, nakumbuka kuna muda nilikuwa najifelisha makusudi kabisa ili anione kwa jinsi ninavyomfikiria halafu nilikuwa najiona kabisa niko poa, lakini kwa sasa nagundua nilikuwa nafanya ujinga mkubwa katika maisha,”

ANACHOKUMBUKA YA MOTO

“Nimekumbuka sana kwa jinsi tulivyokuwa tunaishi, yaani muda mwingi ilikuwa ni furaha sana hasa kipindi tukiwa tunaenda kwenye shoo, lakini kwa sasa naenda kwenye shoo najikuta nipo peke yangu, nakumbuka sana,” anasema Beka, ambaye anamkubali Christian Bella na Vanessa Mdee.

MCHANGO WA DIAMOND.

Ukiachana na Mkubwa Fella, Beka pia anamtaja Diamond Platnumz kuwa anamchango mkubwa kwao. “Jamaa mara nyingi alikuwa anasisitiza tufanane na nyimbo zetu yaani tujitengenezee namna ya kuonekana wa thamani.

“Maana kwa jinsi tulivyokuwa hatukuwa tukifanana kabisa na nyimbo zetu, kila mara alikuwa anasisitiza hilo na pia alituunganisha kwenda kushuti nje kwa GodFather, kilikuwa kitu poa sana.

ALIINGIAJE YAMOTO?

Beka anafunguka kuwa kwa mara ya kwanza alikutana na Mkubwa Fella, Morogoro ambapo alimuoneshea kipaji chake cha kuimba na jamaa alipenda na kumpa namba ya simu kwa sababu kwa kipindi hicho bado alikuwa anasoma.

“Nilikuwa nawasiliana naye hadi nilipomaliza shule nilikuja Dar, nikaanza mazoezi Temeke ambako ndipo kuna kituo cha Mkubwa na Wanawe, baada ya hapo nikachukuliwa nikaanza kukaa hapo hapo.

“Mwaka 2013 ndipo kundi liliundwa na hapo ndipo tulianza kuonekana na kufahamika na wengi baada ya kutoa kazi ya kwanza ambayo iliitwa Ya Moto na huo wimbo ndio ukawa chanzo cha jina hilo la bendi.”