Mpango mzima harusi ya Lulu

HABARI ya mjini ni harusi itakayotingisha nchi ya mwigizaji wa filiamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’anayedaiwa kutaka kufunga ndoa na mmiliki wa Redio EFM, Francis Shiza ‘DJ Majizo.’

Taarifa za kuwepo kwa ndoa hiyo zilienea baada ya mkuu mwenye Jiji lake la Dar es Salaam, Paul Makonda kuthibitisha kwenye mitandao atakuwa mwenyekiti wa shughuli hiyo ambayo itafanyika hivi karibuni.

Katika akaunti yake ya Instagram Makonda aliandika: Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi ya Bw. Majizo na Bi.

Elizabeth Michael (Lulu) nimeupitisha wimbo huu wa Mrisho Mpoto na Harmonize kuwa wimbo rasmi wa harusi yao, kuhusu tarehe za harusi endelea kufuatilia 92.5 Dodoma.”

Baada ya taarifa hiyo, wenye maneno yao wakaanza kuyasambaza. Wengine wakidai ni kiki lakini wengine wakidai habari ndio hiyo.

Mtu wa pili kuthibitisha habari hizo ni mtu wake wa karibu kabisa na Lulu, Makhsein Awadhi ‘Dk. Cheni’. Naye aliposti picha ya Majizo na Lulu wakiwa pamoja na kuandika kuna mtu mwenye swali?

Kama haitoshi baadaye akaposti picha yake na kuandika kuwa “Naitwa Dk. Cheni ni MC wa siku hiyo inayosubiriwa sijui ya nani vile mh,”akamtagi Makonda.

Unadhani Majizo alikaa kimya?

“La hasha aliposti picha inayoonyesha 95.5 Morogoro, na kuandika: “Tupo hewani kuanzia sasa hivi, namba yenu ya bahati ni 95.5 FM… Hatudaiani #ByBwanaharusi cc Mwenyekiti wa kamati kuu.” Akamtagi Paul Makonda.

Hata Mwanaspoti nalo halikukaa kimya, likamvutia waya, Lucresia Karugila huyu ni mama mzazi wa Lulu ili athibitishe au akanushe uwepo wa iyena hiyo.

“Mbona una haraka? Siku ikifika itawekwa wazi kwa kila mtu, kwa sasa siko tayari kuzungumza hilo, ila ni kweli Majizo ni mkwe wangu.”

Imebainika taarifa za Lulu kufunga ndoa na Majizo hazikuanza kusikika leo. Umbea ulianza kuzagaa tangu mwaka jana na Lulu alithibitisha wakati akikakunusha taarifa za kuachana kwao.

Hata hivyo, haikufanyika. Sababu kubwa ikitajwa ni kesi iliyokuwa ikimkabili staa huyo wa filamu.

Ndoa ya kwanza

Pia, inadaiwa mipango ya Lulu kutaka kufunga ndoa ilianza tangu mwaka 2012 lakini Mungu hakupenda ikayeyuka.

Mwaka huo, kulikuwa na taarifa za Lulu kuvishwa pete ya uchumba na msanii mwenzake, Steven Kanumba na kufikia kutambulishwa ukweni, lakini Lulu alipoulizwa hakuwa akitoa ushirikiano hadi alipokutwa na sakata la kumuua Kanumba bila kukusudia.

Kwa vile Kanumba alikuwa hatajwi katika ishu hiyo, ndipo ikafunguka kwa wadau kumbe mwanaume aliyetaka kumuoa ndiye huyo.

Habari za Lulu kutaka kuolewa hajziwahi kukoma, mwaka 2013 Lulu alipata mchumba wa kuziba pengo la Kanumba aliyejukana kwa jina la Lusekelo Samson ‘Seki’wa Mwanza. Kwa bahati mbaya naye alifariki.

Baada kifo hicho, Lulu alijiondoa katika mitandao hususan ule wa Instagram, baada ya kushambuliwa kwa matusi akihusishwa na kifo cha Seki.

Mwaka mzima Lulu alikuwa kimya.

Ulipoingia mwaka 2015 ikaanza kusikika tena kuwa Lulu amepata mchumba.

Tena ni mfanyabihashara maarufu wa jijini Dar es Salaam.

Katika mitandao ya kijamii umbeya ulisema mfanyabiashara huyo anataka kufunga ndoa na Lulu.

Mwaka 2016, ikagundulika kuwa mfanyabiashara huyo ni Majizo aliyetoka kuachana na Hamisa Mobetto na uhusiano wao ulianza tangu mwaka 2015.

Mwaka 2016, umbeya ukazidi kudai kuwa Majizo alishamlipa mahari kwa siri na hakutaka mambo ya vyombo vya habari.

Ndipo mwaka 2017 zilipozuka habari za Lulu kuachana na Majizo.

Mwanaspoti lilizungumza na Lulu na alikuwa na haya ya kusema: “Najua wapo watu wanatamani niachane na Majizo, lakini watapigwa na butwaa maana siku zinakaribia na karibu tarehe ya ndoa yangu itatangazwa.

“Kwa uwezo wa Mungu, hapo ndipo waliotamani tuachane wataziba midomo, maana natarajiwa kuwa mke halali hivi karibuni.’’

Lulu ni nani?

Akiwa na umri wa miaka saba tu, alionwa na Dk. Cheni kupitia bonanza la kuibua vipaji lililoandaliwa na nyota huyo aliyekuwa akiigiza katika Kundi la Kaole.

Dk. Cheni ndiye aliyempeleka Lulu kuigiza katika Kundi la Sanaa la Kaole ambako nyota yake ya uigizaji ikaanza kung’aa fasta.

Alionyesha uwezo mkubwa wa kuvaa uhalisia wa nafasi anazopewa kuigiza, jambo lililomtengenezea mashabiki wengi.

Jina la Lulu

Mbali na uigizaji, Lulu pia amewahi kujihusisha na utangazaji kwenye Kipindi cha Watoto cha Runinga ya ITV mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Jina la Lulu alipewa na msanii mwingine wa zamani wa Kaole, Chiki Mchome ambaye mbali na kumtaka alitumie katika filamu yake, alimsihi alitumie kibiashara kwani litamfungulia milango ya neema siku za usoni.

Walimwengu wanasubiri kuona nini kitafanyika na zaidi kumwona Lulu akiingia maisha mapya.