Miss kanda ya ziwa aduwaza mashabiki

AMEKATA mzizi wa fitina. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Sharon Headlam kuibuka kidedea kwenye shindano la Mrembo wa Kanda ya Ziwa ‘Miss Lake Zone 2018’ na kuamua kufanya maamuzi magumu ya kuchagua zawadi ya gari ambalo lilikataliwa na waandaaji wa Miss Tanzania.

Ilikuwa ni tofauti na walivyofikiria wadau ambao walijitokeza katika shindano hilo na wengi waliamini mshindi huyo ataondoka na gari lililonunuliwa kwa mara ya pili baada ya lile la awali kuwa na misukosuko.

Wadau mbalimbali walibaki na sintofahamu kwa maamuzi ya mrembo huyo kulichagua gari ambalo lilikataliwa mapema na waandaaji wa Miss Tanzania kwa madai ya kutokidhi vigezo.

Baada ya kutangazwa mshindi, aliruhusiwa kuchagua gari moja kati ya mawili, lile lililosemekana kuchakaa na jipya lililonunuliwa kuwa mbadala, mrembo huyo akalichagua lile ‘chakavu’ na kuwashangaza wengi.

Gari alilolichagua ni Toyota Passo lililotajwa kuwa na thamani ya Sh8 milioni.

Mshindi wa pili Miriam Mmari aliondoka na seti ya sofa na wa tatu Zuhura Abdul alizawadiwa seti ya runinga.

Msikie mwenyewe

Mrembo huyo anasema ameamua kulichagua gari hilo ambalo picha yake ilisambazwa mitandaoni na kujadiliwa kwa mapungufu yake, akisema msingi wa uamuzi wake, ndio zawadi ya kwanza iliyokuwa imetolewa.

Anasema hakujitokeza kushiriki shindano hilo ili apewe gari, isipokuwa alijiingiza kwenye ushindani ili kutimiza ndoto zake za kutwaa taji hilo na kufikia malengo yake kimaisha.

Amewataka wadau kukubaliana na maamuzi yake na zawadi ni zawadi cha msingi iwe halali na anashukuru kwa sapoti waliyompa hadi kufikia hatua ya kuitwa Miss Lake Zone.

“Nimechukua gari hili kutokana na ndio zawadi iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yangu, siwezi kuikataa kwa sababu ya maoni ya watu mitandaoni, lengo langu ni kupiga hatua kwenye mashindano haya,” anasema Headlam.

Wadau watofautiana

Baadhi ya wadau waliojitokeza kulishuhudia shindano hilo, walikuwa na maoni tofauti juu ya uamuzi wa mshindi huyo.

Wapo waliosema huenda mrembo huyo ameshawishiwa ili kulinda hadhi ya waandaaji huku wengine wakisapoti hatua aliyoichukua mwanadada huyo.

Rebeca Wiliam, mkazi wa Nyakato hapa Mwanza anasema anaamini mrembo huyo ameshawishiwa kuchukua gari lililokataliwa kwani hata alipoenda kuchagua alionekana kusitasita kabla ya maamuzi.

Anasema alimfuatilia vizuri na anaonekana kisaikolojia anapendelea gari jipya lililokuwa na rangi nyekundu, lakini anaamini kutokana na msukumo alioupata akaamua achukue lililochoka.

“Nilimchunguza vizuri, anaonekana akili ilikuwa kwa ile nyekundu, lakini akasita na kuingia kwenye lile la rangi ya bluu. Ni dalili alishawishiwa,”alisema.

Kwa upande wake, Emmanuel Laurence, alisema: “Nadhani ameamua sahihi tu, si mwenyewe ameridhika? Waliolikataa lile gari ni wale waandaaji wa Miss Tanzania, lakini yeye ameona linamfaa, namuunga mkono.”

Waandaaji wafunguka

Mkurugenzi wa Kampuni ya Jembe Ni Jembe iliyoandaa shindano hilo, Sebastian Ndege, alisema wanakubali kupokea changamoto hiyo ya zawadi ya gari na wamejifunza jambo.

“Tulipopata changamoto hiyo na kutokana na sapoti ya wakazi wa Mwanza kwa kampuni yetu, tukaamua kuingia tena sokoni kununua gari nyingine na kuyaweka yote na mhusika amechagua analolipenda,” alisema Ndege.

Ndege ameongeza changamoto hiyo inapaswa kuwa funzo hata kwa wengine kwani hawakutarajia kufikia hatua hiyo ya kununua gari mbili kwa wakati mmoja.

Hali ilivyokuwa

Katika shindano hilo, warembo 15 kutoka mikoa ya Mwanza, Geita na Mara walichuana vikali jukwaani na Sharon akawazidi wenzake.

Siku njema huonekana asubuhi, kuanzia alivyopanda jukwaani kwa mara ya kwanza, mlimbwende huyo alikuwa akishangiliwa mwanzo mwisho.

Sharon anayetokea Mwanza, aliingia Tano Bora akiwa na Yunis Donald, Zuhura, Miriam na Neema Charles, kisha akasonga Tatu Bora akiwa na Zuhura na Miriam kabla ya kuibuka na taji.

Kabla ya kumtangaza mshindi, Jaji Mkuu Basila Mwanuzi alisema vigezo vya ushindi ni urembo, ufahamu bora na utu.

“Tuna kazi ngumu ya kumpata mshindi, lakini tunaongozwa na kanuni hivyo ili uwe mshindi lazima uwe sifa za kibalozi, kiintelijensia, mwonekano na utu,” alisema Basila.

Mipango ya mshindi

Anasema mipango yake ni kushirikiana na serikali kutangaza vivutio vya ndani vya utalii.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kunitimizia ndoto. Nimejiamini na kutambua nachokifanya, pia nitashirikiana na serikali kuibua vipaji vya watu wa chini,” alisema.

Amewaomba wadau wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wao waendelee kumsapoti akiahidi kutowaangusha katika fainali za taifa za Miss Tanzania.

Wasanii wapagawisha

Wasanii mbalimbali walitumbuiza lakini waliobamba zaidi ni Barnaba na Dogo Janja waliofanya shoo ya kibabe. Wengine ni Irene Uwoya, Jaqueline Wolper na Irene Paul.