Miaka mitatu ya kifo cha Banza Stone, familia yalia ukiwa

Muktasari:

  • Banza Stone alifariki dunia Julai 17, 2015 Ijumaa nyumbani kwao Sinza Vatican na kuzikwa julai 18,2015 katika makaburi ya Sinza Makaburini jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Hii ndiyo hali halisi! Ikiwa leo ni kumbukumbu ya miaka mitatu tangu kifo cha mwanamuziki Ramadhani Masanja 'Banza Stone' familia yake imedai wasanii wenzake wamepotea.

Banza Stone alifariki dunia Julai 17, 2015 Ijumaa nyumbani kwao Sinza Vatican na kuzikwa julai 18,2015 katika makaburi ya Sinza Makaburini jijini Dar es Salaam.

Tasnia ya Muziki wa Dansi

Banza Stone anakumbukwa kwa nyimbo zake Mtaji wa Maskini, Elimu ya Mjinga, 'Aungurumapo Simba, 'Kumekucha, Falsafa ya Maisha, ambazo hazichuji masikioni mwa mashabiki wa muziki wa dansi.

Kutokana na kifo cha staa huyo ni changamoto kubwa ambayo ilikuwa ikisababisha wengine kufanya kazi kwa bidii ili wamfikie au pengine wapite kiwango alichokuanacho cha uimbaji na sauti yake ya kuvutia, lakini hadi sasa hakuna aliyefanikiwa kuwa na sauti ya Banza.

Familia yake inasemaje?

MCL Digital leo ilifunga safari hadi nyumbani kwa Banza Stone na kuzungumza na kaka yake Hamisi Masanja alisema tunashukuru leo katika kumbukumbu ya ndugu yetu Banza Stone, tumeweza kusoma kisomo asubuhi na kwenda kaburini kwa ajili ya kurekebisha kaburi lake.

Hamisi aliiambia MCL Digital tangu Banza afariki changamoto wanazopata ni za kawaida, ila wanakumbuka mchango wake katika familia yao.

Hamisi hakuishia hapo alizungumzia suala la wasanii wenzake kutofanya mawasiliano na familia yake kama ilivyokuwa hapo mwanzo alipokuwa hai ndugu yao.

"Tangu Banza amefariki huu mwaka wa tatu hakuna mawasiliano na wasanii wenzie wale aliokuwa nao kwa ukaribu au viongozi wake wa bendi, imekuwa tofauti na alivyokuwa hai tulikuwa tunawasiliana mara kwa mara, hivyo nawaomba tu wazidi kumuombea dua, japo huenda wamebanwa na majukumu," alisema Hamis

Wasanii wazungumza

MCL Digital ilipata kuzungumza na baadhi ya wasanii kuhusiana na siku hii ya leo ya kumbukumbu ya Banza Stone:

Kiongozi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Luizer Mbutu alisema ni kweli leo ni kumbukumbu ya Banza Stone, mie kwa upande wangu nitamkumbuka kutokana na kuwa na vipaji vingi katika burudani, maana alikuwa anaimba, mtunzi, mpiga drum, mpiga tumba na mzuri kuimba nyimbo za kizungu.

“Banza atakumbukwa kwa kuimbaji wa nyimbo zake za jamii, hakuwa mpenzi wa kuimba nyimbo za mapenzi, yaani nyimbo zake ulikuwa ukisikiliza zinaendana na matukio" alisema Mbutu.

Akizungumzia suala la wasanii kutofanya mawasiliano na familia ya Banza, Luizer alisema ni kweli kabisa familia inavyosema mawasiliano hakuna kama alivyokuwepo hai, hii ni asilimia kubwa sisi watanzania sio Banza tu hata mimi siku Mungu akinichukua familia yangu hawatakuwa na mawasiliano na watu wangu wa karibu, sababu mimi ndio nilikuwa mzizi mkuu wa kiunganisho sasa sipo tena, hivyo ni kawaida tu," alisema Luizer.

Mwanamuziki Ramadhani Mhoza 'Rama Pentagone' alisema Banza Stone anamkumbuka kutokana na kuwa mwanaharakati kwani alikuwa haimbi nyimbo za mapenzi, alikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo za kuelimisha na maisha.

Pentagone alisema familia ya Banza haikuwa karibu na wanamuziki kama alivyokuwa marehemu mama yake Banza Stone, hivyo imekuwa ugumu wa kuwazoea baada ya kifo cha Banza.

"Kiufupi wao walikuwa wanajitenga ikachukua ugumu wanamuziki kuwazoea, ila mama alikuwa na ukaribu sana yaani ukisikia mila za kisukuma basi mama Banza alikuwa nazo,"alisema Pentagone