Mastaa Simba, Yanga wapamba Kombe la Dunia

NYOTA wa zamani wa Simba na Yanga, Edibily Lunyamila, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Abass Kuka wamepamba uzinduzi wa kituo cha DSTV kurusha matangazo ya Kombe la Dunia moja kwa moja kwa lugha ya Kiswahili kutoka nchini Urusi.

Meneja matukio wa Multichoice Tanzania, Ronald Shelukindo alisema watakuwa na chaneli sita zitakazorusha mubashara mechi zote 64.

Kombe la Dunia ambalo litafanyia kwa mara ya kwanza, Ulaya ya Mashariki linatarajiwa kuanza rasmi Juni 14 kwa mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Urusi dhidi ya Saudi Arabia.

“Kila mchezo utakuwa Live (mubashara) kwa sababu tumetenga chaneli hadi sita ambazo zitahusika na kombe hilo la Dunia kwa lugha mbalimbali ikiwemo lugha yetu ya Kiswahili, tutarusha matangazo yetu kwenye kiwango cha juu (HD),” alisema Shelukindo.