Magufuli ainogesha Fiesta Dar

ASLAY NA NANDY

USIKU wa kuamkia Jumapili huku Dar es Salaam ilikuwa si mchezo hapo kwenye viwanja vya Leaders. Fiesta ilinoga ile mbaya manake.

Tamasha hilo ambalo, awali lilitangazwa kumalizika saa saba kamili usiku, lakini baadaye  ilitangazwa kibali kimepatikana hadi saa kumi na moja alfajiri.

Lakini ilipofika saa kumi na moja alfajiri, wakati msanii Chege Chigunda ‘Mtoto wa mama Saidi’ akiwa jukwaani anaimba wimbo wa ‘Mwanayumba’ alisimamishwa na watangazaji wa Clouds FM, B Dozen na Adam Mchovu na kuwatangazia mashabiki kuwa, wamepokea simu kutoka kwa Rais John Pombe Magufuli, kuwa anataka Tamasha la Fiesta liendelee hadi saa 12 asubuhi wakati yeye anaenda kanisani apishane na watu barabarani wakiwa wanatoka katika tamasha hilo.

Mashabiki kuambiwa muda umeongezwa wakalipuka kwa shangwe.

WASANII UBUNIFU

Wasanii wengi walikuwa wanaumiza kichwa kuongeza ubunifu ili kuhamasisha mashabiki. Na walipatia. Mtu kama Ben Pol kwa kuingia na muigizaji anayejulikana kwa jina la Tausi akiwa amevaa shela nyeupe na Ben Pol akiwa amevaa suti nyeupe wakisindikizwa na wimbo unaoitwa ‘Nimekuchagua wewe’ wa mwanamuziki wa  siku nyingi Bob Rudala. Alipagawisha.

Baadaye akabadilisha na kuchomekea zingine, mara Paaap! mchekeshaji Ebitoke akatinga jukwaani na kuanza kurushiana maneno na Tausi akidai kuwa Ben Pol ni mpenzi wake, yaani ilikuwa kama maigizo.

Kwa upande wa Jux, yeye alipanda na Vanessa Mdee na kuimba wimbo wa mwanamuziki Bushoke aliomshirikisha K-lynn ‘Nalia kwa furaha’ na walikuwa wanapokezana lakini Vanessa alikuwa anaigiza kama  hamtaki Jux.

Jux alimpandisha pia Kassim Mganga ili amsaidie kumbembeleza Vanessa aweze kumsamehe ndipo alipoimba wimbo wake ‘Haiwezekani’ alikuwa anamwambia Vanessa haiwezekani amuache Jux.

Aliona haitoshi Jux akampandisha Q Chifu na kuanza kumuimbia Vanessa wimbo wa ‘Nikilala naota’ hapo ndipo Vanessa akatamka kuwa kamsamehe Jux na wamerudiana rasmi ila asirudie tena na kuamsha hoi hoi.

Pia msanii Barnaba hakuwa nyuma na ubunifu wake wa kuingia jukwaani akiimba wimbo wa Fally Ipupa, Eloko oyo na baadaye akampandisha Isha Mashauzi na wimbo wake ‘Nimpe Nani’wakaanza kuimba  kwa pamoja kitu ambacho baadhi yao wengi hawakutarajia taarabu kuimbwa katika shoo hiyo.

Mbali na hao wanamuziki wengine ni Roma na Stamina wao waliingia wakiwa wamevaa jezi nyingi wakawa wanavua moja moja kwa kubishana huku wakiimba wimbo wao wa ‘huku ama kule’.

ZA KALE ZILINOGA

Mashabiki nao hawakuwa nyuma kuonyesha kuwa kiingilio chao hakijaenda bure, pale walipoonyesha  kufurahia  nyimbo za zamani zilizokuwa zinapigwa na dj pindi wanamuziki wakishuka jukwaani.

AFANDE SELE ANALIPA

Nani amekwambia Afande Sele amechuja? Kwenye Fiesta alishangiliwa kinoma. Alikamua vizuri na kulitawala jukwaa huku mashabiki wakimfuatia kwa maneno ya wimbo wa Mtazamo.

ASLAY  NA MAVOKO VIPI?

Aslay alipanda jukwaani saa nane ambapo aliimba wimbo wake wa ‘Pusha’ hajaumaliza akaanza kuuchambua wimbo wake mpya wa  ‘Koro’ unaowahusu wanawake.

Baada ya hapo akawaita wenzake aliokuwa nao Yamoto, akaanza kuelezea habari za Yamoto kuwa itarudi mara wakaanza kuimba nyimbo za bendi hiyo hadi aliposhuka.

Kwa upande wa Rich Mavoko, yeye alipanda jukwaani na kuimba wimbo wake wa ‘Kokolo’ aliomshirikisha Diamond, mara akaimba wimbo wa Hamornize wa ‘Show me’ na wimbo wake mpya wa Rudi kaimba ubeti mmoja tu.

Hapo mashabiki ndio wakaanza kuwaambia waimbe nyimbo zao lakini haikufanyika hivyo.

Wanamuziki wote waliopafomu walishangiliwa ila hawa walishangiliwa zaidi na mashabiki ambao ni Chege,Temba,Afande Sele,Mr.Blue,Ali Kiba, Weusi, Barnaba, Darasa, Dogo Janja na Madee.