Madame Wema Sepetu atoa neno zito aisee

Friday December 1 2017

 

By RHOBI CHACHA

YAWEZEKANA ni hizi habari zilizozuka hivi karibuni za kuwa, ana mpango wa kuhama CHADEMA na kurudi CCM alikokuwa mwanzo.

Au ni habari nyingine zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa, aliwekwa kwenye mapumziko kutokana na kupata ujauzito ambao unamsumbua.

Pia, pengine zile timu za mitandaoni zinazomshambulia na kwa sasa kuna habari kuwa amerudiana na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond waliyewahi kutoka pamoja.

Lakini, ukweli anaujua mwenyewe staa wa Bongo Movie, Wema Sepetu. Mlimbwende huyo kupitia katika akaunti yake ya Instagram juzi ametupia ujumbe mzito juu ya maisha yake ya sasa na pindi atakapoaga dunia.

Miss Tanzania (2006), anaonekana kuandika ujumbe huo kwa hisia kali huku akimwomba Mungu amwepushe na mitandao ya kijamii.

UJUMBE WENYEWE

“Ipo siku nitakufa, hakuna anayeishi milele, sijui mtaendelea kunisema kwa kejeli na kunitukana matusi ya nguoni au ndo itakuwa, “Maskini ya Mungu, dada wa watu alikuwa hivi na vile, Mungu ailaze roho yake mahali pema?.

“Kuna muda mwingine huwa natamani Allah Subhannah wata’allah (Mwenyezi Mungu Baba) anichukue tu, ya dunia ni mengi sana.

“Kuna muda mwingine namkufuru Mwenyezi Mungu na kutamani labda hata nisingekuwepo, ila acha niendelee kumtegemea yeye, kila jambo hutokea kwa sababu, hili nalo litapita,” aliandika na kuongeza.

“I think I need a time off Social Media (Nafikiri nahitaji muda kuwa nje ya mitandao ya kijamii), kwa mara nyingine tena, siwezi jamani,” alihitimisha andiko lake hilo.

Lakini, Mwanaspoti lilijaribu kuzungumza naye kuhusu kutaka kufahamu habari mbalimbali zinazosikika pamoja na hii ya kurudi CCM na alisema hayuko kwenye hali nzuri hivyo atazungumza wakati mwingine.