Kilichomponza Eboue England kinamgharimu Babu Tale Bongo

DESEMBA mwaka jana ilivuma habari kumhusu staa wa soka, Emmanuel Eboue. Kwamba mtalaka wake, Aurelie Bertrand, raia wa Ubelgiji, alimkomba kila kitu na kisha mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast, akawa hohehahe.

Ikawa mshangao mkubwa; Eboue alikuwa akipokea mshahara wa Euro 2.5 milioni (Sh6.7 bilioni) kwa mwaka alipokuwa Arsenal, inakuwaje afilisike mpaka akose mahali pa kukaa na kulazimika kulala kwenye vibaraza vya marafiki?

Sh6.7 bilioni kwa mwaka ni sawa na kusema Eboue kila mwezi alikuwa akiingiza Sh558 milioni ambazo ukizikokotoa unapata Sh140 milioni kwa wiki. Mpunga wote huo uliokuwa ukifurika benki kwenye akaunti zake, eti akafilisika kabisa. Fedha hizo ni mshahara tu. Sijagusa matangazo na dili nyingine.

Kilichosababisha Eboue ahame kimaisha kutoka kijana staa wa soka tajiri hadi kuwa ombaomba asiye na makazi ni hukumu ya Jaji wa Wilaya, Edward Cross ambaye alisikiliza kesi ya mgogoro wa ndoa kati ya Eboue na Aurelie.

Eboue hakuhudhuria kesi yake iliyosikilizwa kwenye Mahakama Kuu ya Familia, London, England. Na kutokuwepo kwake mahakamani, kulisababisha kesi isikilizwe upande mmoja. Jaji Cross alitoa hukumu yenye kumpa Aurelie umiliki wa kila kitu mpaka jumba lake lililopo London.

Watu wengi, hasa Waafrika walionyesha hisia zao kuhusiana na masahibu hayo ya Eboue. Wengi walimlaumu Aurelie kuwa ni mwanamke katili, kwani alibeba kila kitu ambacho Eboue alikivujia jasho. Hakuzingatia hata nafasi yake kuwa ni baba wa watoto wake watatu.

Hata hivyo, ukweli ambao hausemwi ni kwamba kitendo cha kutohudhuria kesi mahakamani ni kosa kubwa la kiufundi. Maana yake kesi ilisikilizwa upande mmoja. Jaji alitoa hukumu pasipo kusikiliza utetezi wa Eboue.

Mahakama sio baraza la utesi. Mlalamikaji anapowasilisha malalamiko, mlalamikiwa hujulishwa na huitwa mahakamani ili shauri lisikilizwe pande mbili. Mlalamikiwa akikosekana, mahakama hugeuka baraza la utesi. Unatetwa na hata kusingiziwa kisha unahukumiwa bila kujitetea.

Majaji na mahakimu nao ni binadamu. Mlalamikiwa anapopewa wito wa mahakama kisha akawa hahudhurii kesi inapotajwa au kusikilizwa, huona kama amedharauliwa yeye na mahakama anayoifanyia kazi. Hivyo, Eboue alikosea kuichukulia poa mahakama.

JIULIZE KWA HISIA

Alipoondoka Arsenal na kujiunga Galatasaray ya Uturuki, mshahara wa Eboue ulikuwa pauni 1.5 milioni (Sh4.5 bilioni) kwa mwaka. Eboue anasema kuwa alipokuwa Uturuki, mapato yake jumla yalikuwa euro 8 milioni (Sh21 bilioni) kwa mwaka.

Fedha hizo ni sawa na kusema Eboue alikuwa akiingiza Sh1.75 bilioni kwa mwezi, Sh437.5 milioni kwa wiki, Sh62.5 milioni kila siku. Hizo fedha ni nyingi mno. Mke kasepa nazo. Mke waliyezaa watoto watatu.

Eboue anasema, katika euro 8 milioni (Sh21 bilioni), yeye alikuwa anabaki na Euro 1 milioni (Sh2.7 bilioni) na euro 7 milioni (Sh18.6 bilioni) alikuwa akimtumia mkewe. Yaani mke pamoja na kupokea Sh18.6 bilioni kila mwaka, amemtenda haya Eboue? Aisee, zimwi likujualo linaweza kukula likakumaliza kabisa!

Utaona kuwa kama Eboue angehudhuria mahakamani na kuonesha mchanganuo wa kile alichokuwa anavuna kwenye maisha yake ya soka na kiasi kikubwa alichokuwa anampa mkewe, pengine Jaji Cross asingetoa hukumu iliyommaliza.

Jaji Cross asingetoa hukumu pamoja na amri ya mahakama ya kumtaka Eboue aondoke mpaka kwenye nyumba yake. Zaidi, Eboue angekuwa karibu na kesi, angefanya haraka kukata rufaa kabla ya muda wa kisheria kupita.

Ni wazi Eboue si tu kwamba alikuwa hahudhurii mahakamani, bali alikuwa mbali na kesi, kwa hiyo akawa hajui chochote kilichokuwa kinaendelea. Wakati wa utekelezaji wa hukumu (writ of execution), ndiyo Eboue alishituka na kuanza kulia. Tayari akawa amechelewa. Ndiyo, ilikuwa too late!

KAMA EBOUE KAMA TALE

Hivi sasa Eboue anapunguza machungu ya kimaisha baada ya kupewa kazi ya kufundisha watoto kwenye kituo cha kulea vipaji cha klabu ya Galatasaray. Mshahara unaingia, mahali pa kukaa si tatizo tena.

Bongoland kwenye kitivo cha burudani kuna mtikisiko. Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambaye ni meneja wa supastaa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anakabiliwa na hatihati ya kupelekwa jela kama mfungwa wa madai (civil prisoner).

Hili la Babu Tale nalo liliibuka kama masihara. Akidaiwa kutumia kibiashara mawaidha ya Mhadhiri wa dini ya Kiislam, Shehe Hashim Mbonde, bila makubaliano halali. Mara hukumu ikatoka ikiagiza Tale amlipe Shehe Mbonde Sh250 milioni.

Wakati tukio hilo linashika moto, japo ulikuwa wa chinichini, nilizungumza na Tale, nikamuuliza kuhusu kesi hiyo, alinijibu: “Achana naye, tuzungumze yetu.” Hiyo ni kuonesha ni kiasi gani Tale alikuwa hajali kesi iliyokuwa ikimhusu.

Baada ya hukumu kutoka na mchakato wa utekelezaji wa hukumu kuanza, ndipo Tale alipotokeza na kueleza kuwa yeye hakuwa mhusika bali marehemu kaka yake, Abdul Taletale ‘Abdu Bonge’. Akasema aliitwa mahakamani hakwenda kwa sababu aliona kesi haimhusu.

Kesi ya msingi ni kampuni ya Tip Top Connection kutengeneza na kusambaza CD za mawaidha ya Shehe Mbonde kibiashara bila ridhaa yake. Tale anafahamika ni mmoja wa viongozi wa Tip Top. Akaitwa mahakamani hakwenda.

Maneno yake kwa usahihi wake, alipaswa kuyatoa mahakamani, kwamba yeye hahusiki na biashara ya CD za mawaidha ya Shehe Mbonde. Pengine angesema hayo mahakamani, angeweza kumshawishi hakimu kuona hakuwa na uhusika wowote.

MDHARAU MWIBA

Ngano ya Kiswahili ilinenwa “mdharau mwiba guu huota tende.” Tale alipuuza wito wa mahakama, kwa hiyo hoja za Shehe Mbonde ndizo pekee zilitamba mahakamani pasipo kupingwa au kupata utetezi wa Tale.

Kwa vile Tale alipuuzia wito wa mahakama, ni dhahiri alikuwa hajui kilichokuwa kikiendelea. Hivyo, hukumu ilipotoka ama hakujua au hakujishughulisha nayo. Asingepuuza pengine angewahi kukata rufaa kabla ya siku za kisheria za kuruhusu kukata rufaa hazijavuka. Ukiweka yote yaliyotokea kwenye kapu moja, jawabu ni moja tu kwamba Tale alisahau kuwa wito aliokuwa anaupuuza ulikuwa wa mahakama. Yeye alidhani anampuuza Shehe Mbonde, kumbe alikuwa anaipuuza mahakama. Ni sawa na Eboue; alijua kutokwenda mahakamani ni kumpuuza mkewe (mtalaka wake), Aurelie, kumbe alikuwa anaipuuza mahakama. Matokeo yake ni maumivu makali kwa Eboue. Ni somo kwamba mahakama si chombo cha kupuuzwa.

Tale alikamatwa kwa amri ya mahakama na kushikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam Jumatano iliyopita na kuachiwa Alhamisi. Sababu ya kumkamata ni utekelezaji wa mchakato wa kumpeleka gerezani kama mfungwa wa madai. Pamoja na kutoka Alhamisi, jambo la kufahamika ni hili kwamba Tale anatakiwa kulipa fedha Sh250 milioni zilizotajwa kwenye hukumu. Hata akifungwa bado sheria inasema deni halifutwi kwa kifungo na yote yasingemfika kama angeheshimu mahakama.