Kijasho kimemtoka

Tuesday October 10 2017

 

ELIZABETH Michael ‘Lulu’ amefichua hakuna urahisi katika kuyafikia mafanikio kwani lazima kupitia mitihani mingi na amekiri kijasho kimemtoka kuishinda mitihani aliyokumbana nayo hadi kufikia alipo sasa.

Lulu alisema watu wamekuwa wepesi kukosoa mafanikio ya wenzao bila kujua namna wahusika walivyotaabika kufika walipo na kutolea mfano waigizaji wa filamu nchini na changamoto walizonazo.

“Mwanadamu anahitaji kushinda mitihani ndipo afanikiwe, hii ipo katika nyanja mbalimbali za kimaisha. Ni lazima mtu ujipime ndipo utaweza kusonga mbele,” alisema msanii huyo.

“Hata kwa upande wetu wa filamu, kwa muda mrefu tumekosa kitu cha kutupima na kutupatia motisha kama wasanii, kwa muda mrefu tumekosa kuwa na tuzo Bongo.”

Lulu aliyasema hayo wakati akitangazwa kuwa Balozi wa Tamasha la Sinema Zetu International Film litakaloonyeshwa kwa mara ya kwanza kupitia runinga kwa kushindanisha kazi za wasanii watakaopatiwa tuzo.

Baadhi ya wadau wa filamu wamepongeza ujio wa tamasha hilo kwani kwa muda mrefu filamu zilikuwa hazina tuzo za hadhi hiyo mbali na ile ya Zanzibar International Film Festival (ZIFF) tu ambayo hutolewa kila mwaka.