Kagera Sugar yapiga hesabu kali kubaki VPL

Muktasari:

Timu hiyo iliyotoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi ikiwa Mjini Bukoba, ilianza vibaya Ligi Kuu, lakini kwa sasa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26.

KLABU ya Kagera Sugar imesema bado haijaridhika na pointi 26 walizonazo kwa sasa, hivyo wanazipigia hesabu kali mechi tano zilizobaki sawa na dakika 450 kuhakikisha wanapata ushindi ili timu isishuke daraja.

Timu hiyo iliyotoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi ikiwa Mjini Bukoba, ilianza vibaya Ligi Kuu, lakini kwa sasa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26.

Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Ally Jangalu alisema kuwa licha ya matokeo waliyonayo kwa sasa ya kutia moyo, lakini bado wanahitaji ushindi zaidi ili kujihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Alisema mkakati wao si kujiandaa na mchezo mmoja mmoja, isipokuwa wanapiga hesabu ya mechi tano zilizobaki kuhakikisha wanashinda zote ili kumaliza msimu wakiwa nafasi nzuri.

“Kidogo tunaanza kupumua, lakini bado kazi inaendelea, tunahitaji kushinda zaidi ili kujihakikishia kubaki kwenye ligi. Tukifanya makosa kidogo tunakwama,” alisema Jangalu.

Kocha huyo alisema kuwa siri ya mafanikio hadi sasa kwa timu hiyo ni kutokata tamaa na kujituma na kwamba malengo yao ni kuinusuru Kagera Sugar kutoshuka daraja.

“Kikubwa ni kupambana na kutokata tamaa, tutaendelea kupigana na kuwaelekeza vijana nini wafanye wawapo uwanjani na uzuri wachezaji wanaelewa,” alisema kocha huyo.

Kagera imebakisha mechi tano dhidi ya Mbeya City, Njombe Mji, Simba, Lipuli na Stand United na iwapo itafanikiwa kushinda mechi hizo itakuwa imejiondoa kwenye wasiwasi wa kushuka daraja.