Jay Z na mkewe wana pesa balaa

Tuesday November 14 2017

 

KATIKA orodha ya wanamuziki wenye pesa nyingi iliyotolewa na Jarida la Forbes mwanzoni mwa mwaka 2014, Jay Z, alishika nafasi ya 12 akiwa amejiingizia Dola 60 milioni.

Wakati Jay Z akitamba katika nafasi hiyo, mke wake, Beyonce yeye alishika nafasi ya pili akiwa na pato lililofikia Dola 115 milioni.

Jay Z na Beyonce ni mume na mke matajiri ambao wameweza kuutumia vizuri muziki katika kuvuna fedha za maana.

Kama unadhani Jay Z ameporomoka basi sahau kwani hiyo ilikuwa ni pato la muziki na ilikuwa kwa kipindi kifupi cha mwaka 2014 ambao ripoti za jumla zinaonyesha aliufunga akiwa njema.

Katika jarida hilo hilo katika ripoti yake ya kuanzia Januari hadi Mei 2015, Jay Z aliingia Tano Bora ya wasanii wa Hip Hop wenye fedha nyingi. Kundi hilo linaitwa Hip Hop Cash Kings.

Wakati huo, Jay Z alishika nafasi ya tatu akiwa na pato linalofikia Dola 550 milioni, lakini takwimu za mwaka huu zilizotolewa tena na Forbes, zinaonyesha Jay Z ana pato linalofikia Dola 810 milioni na kuwa namba mbili nyuma ya P Diddy, anayeripotiwa kuwa na pato la Dola 820 milioni.

Jay Z, ambaye jina lake halisi ni Shawn Corey Carter, alizaliwa Desemba 4, 1969 katika Jiji la New York, Marekani. Jay Z ambaye ni rapa, pia ni mjasiriamali aliyewekeza katika vyanzo mbalimbali huku asili hasa ya kipato chake ikitajwa kuwa ni shughuli yake ya muziki.