Jamani ndoa ya Prof Jay ilianzia mbali nyie

Tuesday July 11 2017

Mbuge wa Mikumi mkoani Morogoro, Joseph Haule
Mbuge wa Mikumi mkoani Morogoro, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, akimbusu Mke wake Grace Mgonjo baada ya kufunga pingu za maisha katika Kanisa la St Peter, Dar es Salaam juzi. Picha za mtandao
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akigonganisha glasi kutakiana afya njema na mke wa mbunge huyo, Grace Mgonjo.
By RHOBI CHACHA

MKONGWE wa muziki wa kizazi kipya aliye pia Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ wikiendi iliyopita aliachana na kambi la ukapera na kufunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi.

Mwanaharakati huyo, alifunga ndoa na rafikiye wa muda mrefu, Grace Mgonjo na kusindikizwa na sherehe bab’ kubwa iliyohudhuriwa na watu maarufu nchini wakiwamo waigizaji, waimbaji wenzake na wanasiasa.

Sasa kama hujui ni kwamba kabla ya Prof Jay kufunga ndoa alipitia hatua tatu tofauti na Mwanaspoti inakutajia hatua hizo kuonyesha wanandoa hao sio watu wa mchezo.

HATUA YA KWANZA

Kumbukumbu zinaonyesha miaka mitatu iliyopita katika mahojiano yake na Mbunge huyo wa Mikumi baadaye kuandika katika ukurasa wake wa Facebook aliainisha sababu za ndoa kushindwa kudumu.

Hata hivyo naye ameingia katika listi hiyo ya wanandoa, je atatekeleza sababu hizo alizotoa?

Katika ujumbe wake, Jay alisema watu hushindwa  kudumu katika ndoa na kuvunjikiwa miezi michache baada ya kuzifunga kwa kukosa umakini na kuzifanya ndoa zao maonyesho katika jamii.

“Ndoa hazidumu kwa sababu kabla ya kufunga ndoa watu wanakuwa obssesed na wedding ceremony imaginations, bila kujua ndoa inaenda mbali zaidi. Kuna ndoa na kuna harusi...Wengi mnapenda zaidi harusi na mnapowaza ndoa picha inayowajia ni suti kali, boonge la shela kutoka Uturuki, make ups za ukweli kwa bibi harusi kutoka Maznat Mikocheni, mashosti kuingia ukumbini na wimbo wa Alingo. Wanafiki kukomeshwa kwa jinsi pati yako itakavyokuwa kali pale Karimjee Hall.

Je, umewahi kuwaza mmeo au mkeo akiumwa miaka mitano mfululizo utaweza kumvumilia? Umewahi kuwaza Watoto watakapozaliwa na ulemavu utawa-care namna gani? Mtakapokosa watoto miaka sita  ya ndoa utahimili maneno ya mama mkwe na mawifi kwamba unawajazia choo cha kaka yao na huna kizazi? Ndoa ni zaidi ya sherehe ya harusi. Baada ya yale matarumbeta kuzimika usiku kifuatacho ni majukumu mazito na kiapo kisichovunjika. Achana na fantasy za kwaito, waza mbali kidoogo... Je, uko tayari kuwa mume au mke wa mtu mmoja tu au ma-ex watarejea kidogo kidogo kama hupati satisfaction ya kutosha kama ya ex wako? Huwa mnawaza hayo au mnawaza zawadi ya kamati itatoa Verossa ya kuanzia maisha? Sidhani... kabla ya kuoa au kuolewa jiulize, unatamani ndoa au ni tamaa ya sherehe ya harusi ili uonekane umeoa au kuolewa?”

Maana yake ni kwamba Jay alishajiandaa kwa hayo yote na tayari kukabiliana na changamoto za ndoa yake na Grace.

HATUA YA PILI

Katika hatua hii Profesa Jay, aliongea kabla ya kufunga ndoa na kusema yupo kwenye maandalizi ya kufunga ndoa.

“Very soon naingia kwenye maisha ndoa,” alisema. “Wakati naingia kwenye majukumu mapya haya hata mke wangu aliniruhusu hebu tumikia wananchi halafu baadae kila kitu kitakuwa sawa, very soon, very soon jiandaeni na kadi zangu.”

Aliongeza kwa kusema, haamini kama kuoa kunaweza kumsababishia msanii wa muziki kushuka na kupoteza baadhi ya mashabiki. Hii ina maana ni kwamba alishajipanga mapema na mwenza wake kuishi pamoja.

HATUA YA TATU

Baada ya kupitia hatua mbili za kwanza, kilichofuata ni jinsi kutikisa Jiji la Dar es Salaam baada ya kufuatiliwa na watu wengi. Kitendo cha kuweza kufanikisha kufunga ndoa na mpenzi wake huyo (Grace Mgonjo) lilikuwa bonge la bao.

Kabla ya ndoa hiyo iliyoibua shangwe kwa ndugu, jamaa na rafiki waliofurika  katika kanisa la Mtakatifu Joseph, Posta- Dar es Salaam, msafara wa kuelekea kanisani ulianzia nyumbani kwa Profesa Jay, Kimara-Temboni jijini Dar. Ndoa hiyo ilifuatiwa na sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City na waalikwa walikula, kunywa na kusaza, huku shughuli nzima ikipambwa na mastaa kibao wa Bongo fleva. Hilo lilikuwa jambo lililomfanya Prof Jay, kutamka kwa furaha kwa kutimiza ahadi yake kwa mchumba wake aliyetoka naye mbali katika safari ya milima na mabonde. “Namshukuru Mungu nimetimiza ahadi ya ndoa kwa mchumba wangu ambaye tumepitia mabonde na milima.”