Jamaa vichwa sana lakini hawasemwi

Muktasari:

  • Ni kweli, Kibongobongo bado sana ila wapo wachache ambao wamefanya makubwa tofauti na wengi wanavyodhani.

INAWEZEKANA ni nadra kusikia katika tasnia ya muziki mameneja ambao wanaweza kusimamia na kutoa fedha na kuwa wabunifu ili wasanii wao wafanye vizuri na kuwa gumzo Bongo.

Ni kweli, Kibongobongo bado sana ila wapo wachache ambao wamefanya makubwa tofauti na wengi wanavyodhani.

Mwanaspoti linakuletea mameneja wa Bongo walioko juu kwa sasa.

CHAMBUSO

Aliwahi kuwa meneja wa kundi la Salam TMK, baada ya kuthibitisha kuachana na lebo ya Mkubwa na Wanawe iliyokuwa inasimamiwa na Mkubwa Fella. Kwa sasa anasimamia kazi za Aslay nje ya kundi la Ya Moto Band.

Usimamizi wake umemfanya Aslay awe juu kutokana na kazi zake zinazobamba kama Muhudumu, Pusha, , Angekuona, Mario, Hautegeki, Danga, Rudi, Tete, Natamba na huu wimbo mpya unaoitwa Koro.

Seven Mosha

Jina lake la kwenye Pasi ya kusafiria ni Christine Mosha, ni mzaliwa wa Nairobi Kenya, lakini akiwa na miaka minne wazazi wake walihamia mkoani Kilimanjaro, Tanzania.

Mwanadada huyo mfanyakazi wa zamani wa Kituo cha Redio cha Clouds FM na kisha akajiunga na MTV mwaka 2010 na baadaye Sony Music, aliamua kubadilisha jina na kujiita Seven Mosha.

Kwa sasa ndiye msimamizi wa lebo ya muziki ya Rockstar4000 na ni meneja wa Ali Kiba aliyefanya naye kazi kwa muda wa miaka sita mpaka sasa. Gazeti la Daily Nation linamtaja kama Malkia (Queen Of Comebacks), kutokana na kitendo cha kuwarudisha kwenye gemu Ali Kiba na project ya Mwana na Lady Jaydee na Ngoma ya Ndindindi baada ya kuwa wamepotea. Pia amewahi kumsimamia Barakah The Prince

SALLAM

Sallam Sharaf ni meneja wa Diamond na kitu ambacho huenda wengi hawajui, pia ni meneja wa mwanamuziki AY.

Ukiachana na Said Fella na Babu Tale kuwa mameneja wa Diamond, Sallam inaaminika ni mmoja wa watu muhimu katika menejimenti ya Diamond. Sifa yake kubwa ni kuweza kutengeneza ramani za hela zilizompaisha Diamond kimataifa.

MADEE

Ni kama mlezi na meneja wa Dogo Janja. Mbali na kumsimamia Dogo Janja, pia ni mwanamuziki wa Bongo Fleva kutoka kundi la Connection lenye makazi yake Manzese Tip Top.

Nyimbo baadhi zilizomfanya kuwa juu Dogo Janja chini ya usimamizi wa Madee ni Kidebe, my Life, Ukivaaje Utapendeza na Ngarenaro.

SAID FELLA

Ni meneja wa siku nyingi wa kundi la TMK Family pamoja na Mkubwa na Wanawe. Ameweza kusimamia kundi la TMK Family linaloundwa na Chege Chigunda na Mh Temba kwa kutoa nyimbo kali zilizoweza kuwashika mashabiki.

Fella ameendelea kuwasimamia wasanii hawa na kila mmoja akitoa nyimbo nje ya kundi la Wanaume Family ambazo pia zimefanya vizuri.