JIACHIE: Vanessa Mdee na Jux ni mahaba tele

Friday January 5 2018

 

MASHABIKI wa muziki nchini ni vigeugeu sana na ni mara chache kuona wamekubali kitu kwa moyo mmoja.

Tabia yao hiyo imewafanya kupinga kila kitu hasa ndoa zinazofungwa na mastaa kwa madai kuwa ni za kutafuta kiki, lakini hali imekuwa tofauti kwa Vanessa Mdee na Jux ambao wamewashikia bango na kuwataka wafunge ndoa.

Wawili hao wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu licha ya hapa katikati penzi lao kugeuka kuwa la kisela na kuamua kutemana kwa muda.

Wakali hao wa Bongo Fleva walishindwa kuficha mahaba yao na kurudiana wakati wa shoo za Fiesta ambapo sasa wanatoka pamoja kama kawaida.

Sasa mashabiki wao hawataki kuwaona wakiachana na tena na wamewaambia wafunge ndoa haraka kama wenzao, Shilole na Uchebe walivyoamua kujifunga wiki chache tu zilizopita.

Wapendanao hao ambao kulikuwa na wasiwasi kama wamerudiana kweli, walionyesha mahaba mazito siku ya mwaka mpya ambapo walikwenda Kenya kufanya shoo.

Pia, hawakutaka kuficha lolote kwani ni kama walitaka ulimwengu mzima utambue kuwa wapo kwenye dimbwi la mapenzi ambalo haliwezi kukatika leo wala kesho kwa kutupia picha zao katika akaunti zao za mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Sasa mashabiki wao wametoa maoni wakiwaambia sasa hakuna kurudi nyuma na wahakikishe wanafunga ndoa.