Huyu hamisa Mobetto ameliamsha kinoma

MBELE ya macho yako amesimama Hamisa Mobetto. Msichana mmoja laini, anayeishi kijanja jijini Dar es Salaam. Ana mvuto wa kipekee na mwonekano wa kuvutia na sura ya kuhamasisha.

Alianza kupamba video za wasanii. Akamvutia DJ Majizo ambaye baada ya kula vya ndani, akamzalia mtoto. Nani angeamini kama Mobetto ana mtoto. Urembo wake ulibaki vile vile.

Mvuto wake ukaongezeka madaradufu, akafanya video ya Salome. Timu mafisi wakaanza kummezea mate. Bosi wake, Diamond Platinumz naye akaanza kula bata, naye akapata zawadi ya mtoto.

Huyu ndiye Hamisa Mobetto. Yupo mjini ametulia. Ni vigumu kumwelezea kwa wepesi. Sura yake haiendani na matendo yake, mwili wake hauendani na uvumilivu wake kabisa, yaani amekaa kipekee kabisa.

Pamoja na kufanya mambo yake kwa siri, alisahau kuwa ‘Penzi ni kikohozi, kulificha huliwezi’. Aliimba mwanamuziki nyota wa Tanzania, Fresh Jumbe ambaye kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki nchini Japan.

Penzi la Hamisa na Diamond lilikuwa siri lakini uzao wa Abdul ulilifichua. Hakukuwa na namna.

Jumbe katika wimbo wake, alionyesha jinsi mapenzi yalivyokuwa hayana kificho na hasa ukichukulia suala zima la Mobeto na Diamond.

WALIKOANZIA

Kwa wasiojua, wanadhani Diamond alianza na Mobetto baada ya kumpata Zari, lakini ukweli wa mambo ni kuwa wawili hao walifahamiana kitambo. Mama Abdul na Diamond walianza kula vya ndani siku nyingi, kabla hata ya wadada wengi wa mjini hapa.

Wenza hao wamewahi kukiri kuwa tangu waanze uhusiano hadi sasa wana miaka kumi, japo walikuwa wanaachana na kurudiana.

“Mimi na Hamisa tulikutana tangu mwaka 2010, tukawa na uhusiano lakini haukudumu. Kipindi hicho nilikuwa sijakutana na Wema wala Zari,” aliwahi kunukuliwa Diamond, msanii bora zaidi wa Bongo Fleva kwa sasa.

“Kipindi nipo na zari alianza kunirequest (kuniomba) turudiane lakini nilimwambia nina familia tayari, tukaendelea, baada kama ya siku tatu habari zikaanza kusambaa mitandaoni Diamond anatembea na Hamisa,” alisimulia Diamond wakati akihojiwa na kituo kimoja cha Radio.

“Nashangaa watu wanaoniambia nimemwingilia Zari katika uhusiano wake, sijawaelewa na wajue tu mimi na Diamond tuko wapenzi zaidi ya miaka kumi sasa,” alisema Hamisa katika arobaini ya mtoto wake aliyezaa na Diamond.

Licha ya kuwa pamoja kwa muda mrefu, Hamisa amepitia vikwazo vingi katika penzi hilo na mmiliki huyo wa lebo ya WCB.

MIMBA YAKATALIWA

Hebu pata picha umepewa mimba halafu mwenye nayo kila akienda hadharani anasema siyo yake. Hakuna ushahidi. Mimba unayo wewe. Ushahidi unao wewe. Utawaaminishaje wengine?

Hamisa ambaye ni mwanamitindo na pia mwigizaji, alipata mtikisiko baada ya Diamond kuikana mimba yake kila alipoulizwa. Angefanyaje na wakati alikuwa na familia. Zari angemwelewa? Jamii ingemwelewa? Ni ngumu.

TUHUMA ZA SHILAWADU

Mwaka jana, wakati Hamisa alipokuwa amepata ujauzito wa Diamond ambaye wakati huo alikuwa kwenye mapenzi mazito na Zarina Hassan ‘Zari’, walikubaliana kufanya siri jambo hilo ili mwandani huyo wa Diamond asijue.

Mama Diamond (Sandra) naye alikuwa kwenye mpango mkakati huo wa kuficha siri ya ujauzito wa Hamisa. Alipojifungua katika Hospitali ya Maria Stopes, Bi Sandra, Dada wa Diamond anayefahamika kama Esma na mama yake Romjs walikwenda kumwona Hamisa, ndipo watangazaji wa kipindi cha Shilawadu waliwavizia na kuwapiga picha na vipande vya video na kuvirusha katika mitandao ya kijamii muda huo huo.

Hapo ndipo watu wakaanza kuamini Hamisa amezaa na Diamond. Baada ya habari hizo kutembea zilimfanya Zari athibitishie pasi na shaka kweli Hamisa amezaa na Diamond, ambaye siku zote wamekuwa wakishea kitanda kimoja.

BIFU NA MAMA DIAMOND

Madai ya kuwaita Shilawadu kurusha vipande vya video vilivyokuwa vikimwonyesha mama Diamond na ndugu zake wakiwa hospitali yalimkera mama Diamond, ambaye aliamini kuwa kitendo hicho kitakuwa kimefanywa na mwanadada huyo mwenye mvuto wa kipekee.

Kwa muda mrefu mashabiki wa Hamisa na mama Diamond walikuwa hawajui kiini cha ugomvi wao, lakini hivi karibuni mama huyo ameweka bayana kwa kusema kisa ni kuwaita Shilawadu waje wamrekodi na kurushwa katika mitandao ya kijamii.

KESI MAHAKAMANI

Baada ya Shilawadu kurusha hivyo vipande vya video, siku si nyingi vipande vingine vya video vikimwonyesha Hamisa akiwa na Diamond na mtoto wao kitandani vilizagaa mitandaoni na kuthibitisha pia Diamond alikubali majukumu ya mtoto wa mrembo huyo.

Mambo baadaye yalibadilika na kulazimisha kesi ya malezi ya mtoto huyo ifike Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo, Hamisa alifafanua haikuwa kesi bali ni utaratibu wa kisheria alioufata ili kutengeneza mazingira yatakayomsaidia mtoto wake kupata haki zake kama watoto wengine wa Diamond.

KIPIGO CHA MAMA DAI

Hamisa na Diamond ni kama vile wamerudiana kwani, sasa baba wa mtoto huyo ameonekana kuwa karibu na mwanaye, Abdul tofauti na siku za nyuma. Pengine ni kwa sababu Zari alimpa kibuti.

Hata hivyo, tangu wamerudiana, kumekuwa na maneno mengi yanayosemwa ikiwemo ya Mama Diamond kumkataa Hamisa na hata baadhi ya mashabiki kuwatolea maneno ya kejeli wawili hao.

Sasa ili kudhihirisha mama Diamond bado ana kinyongo na Hamisa, Mei 13, mwaka huu mara baada ya Hamisa pamoja na Diamond kutoka kwenye shoo ya msanii wa WCB, Marombosso (Mbosso) walirudi nyumbani kwao Madale usiku.

Mama Diamond naye alirudi nyumbani hapo na alilala katika chumba chake bila kujua Diamond yuko na Hamisa.

Kulipopambazuka alikwenda kwenye mishemishe zake na aliporejea ndipo alipoliamsha dude baada ya kushtukia mrembo huyo amelala nyumbani hapo.

Madai ya Bi Sandra kumchapa makonde Hamisa hadi kumvua wigi yakashika kasi mitandaoni, huku akikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari (Sio Mwanaspoti) kuwa ni kweli alimpiga Hamisa na hataki afike nyumbani kwake.

MAMA DIAMOND AMKANA

Hata hivyo, baada ya ishu hiyo kuzagaa sana mitandaoni, Bi Sandra ameibuka na kukanusha kumpiga mrembo huyo aliyepo kwenye mahusiano na mwanaye

Mama Diamond aliweka wazi jambo hilo kupita mtandao wa WCB na kusema, jambo hilo limekuzwa kutokana na watu kupenda kufuatilia mambo ya familia yake.

Alifafanua kuwa, mambo hayo yanayozungumzwa kuhusu kumpiga mwanamitindo huyo, lakini hafahamu yametoka wapi ilihali hakuna jambo kama hilo.