Harmonize sasa kaamua

Muktasari:

  • Ipo hivi. Staa huyo wa Aiyola na Show Me, ametumia katika akaunti yake picha ya kipimo cha Utra Sound’ ikionyesha kiumbe kilichopo tumboni mwa mwanamke

WIKI chache tu tangu amteme Jacquiline Wolper, mwimbaji mkali wa Bongofleva kutoka WCB, Harmonize amethibitisha kwa sasa ameamua kwelikweli.

Ipo hivi. Staa huyo wa Aiyola na Show Me, ametumia katika akaunti yake picha ya kipimo cha Utra Sound’ ikionyesha kiumbe kilichopo tumboni mwa mwanamke.

Kitendo hicho cha kuitumia akaunti yake ya Instagram kutupia picha hiyo imewamsha wengi na hasa maneno yaliyoisindikiza yaliyosomeka; “Mnh nawaza huu mchanganyiko wa damu ya Kimakonde na ya Kizungu sijui itatuletea mwana gani...hasa nikiona kakomwe hapo, kananistua…chonde mtoto chukua vyote kwangu ila kwenye rangi jitahidi uibe ya mama yako…Nikavimbe Mtwara..!!

Picha na ujumbe huo ulikuwa unathibitisha yale madai kwamba mwimbaji huyo amemtundika mimba Mzungu na kuwapa nafasi mashabiki wake kumjadili wakidasi kuwa, ameshindwa kujizuia na kumwanika mzungu wake.

Siku chache zilizopita iligundulika kuwa chanzo cha kutemana na Wolper, ilitokana na mzungu huyo anayedaiwa ana fedha zake, japo alikuwa akifanya siri na hata alipokuwa akiulizwa alikuwa akikanusha.

Hata hivyo, ikiwa hata haijafika mwezi ndio kama hivyo kaposti Utra Sound na kuandika maneno yenye kuashiria kuwa ni kweli lisemwalo lipo juu ya mimba yake kwa Mzungu.

Kwa wiki nzima sasa ishu yake ndiyo imekuwa habari ya jiji hasa eneo la Sinza, baadhi ya watu kumshambulia kwa maneno kwa nini anashindwa kuweka wazi au bado ana lengo la kurudi kwa Wolper.