HE! Bongo Fleva wanaoa bana

Muktasari:

Wasanii wengi wa muziki huo ulipoanza, walikuwa wahuni. Walikuwa ni watu wa bata mpaka aibu. Walikesha kwenye kumbi za starehe. Walitembea na wake za watu. Walilewa umaarufu.

NANI asiyekumbuka namna Bongo Fleva ilivyoanza kwa kuhesabika ni muziki wa kihuni? Muziki huo ulipigwa vita, watu walisema umesheheni kundi la wahuni. Unadhani ilikuwa uongo? Hapana, ilikuwa kweli.

Wasanii wengi wa muziki huo ulipoanza, walikuwa wahuni. Walikuwa ni watu wa bata mpaka aibu. Walikesha kwenye kumbi za starehe. Walitembea na wake za watu. Walilewa umaarufu.

Unaambiwa miaka ya tisini Bongo Fleva ilikuwa muziki wa kihuni. Baadhi ya wazazi waliogopa watoto wao kuingia katika muziki huo kwa hofu ya kuwapoteza. Hata wasomi walikwepa kujihusisha na muziki huo sababu ulionekana ni muziki wa vijana walioshindwa maadili. Ilisikitisha sana.

Ila ilipofika miaka ya 2000, jamii ikapata mtazamo tofauti. Wadau wa muziki wakaanza kuamini labda kulikuwa na wahuni wachache ndio waliofanya uhuni, ila muziki huo haukuwa wa kihuni.

Ubunifu, mabadiliko katika muziki huo na hata mavazi vikachochea kufuta imani ya watu waliokuwa wakiamini kuwa muziki huo ni uhuni. Ghafla wasanii wa Bongo Fleva wakaanza kuheshimika. Leo hii kina Sugu na Profesa Jay wako bungeni. Akina Mwana FA na AY wapo kwenye taasisi kubwa za kibiashara.

Pamoja na mabadiliko hayo, bado wapo baadhi ya wanawake ambao hadi sasa wanaamini kuwa muziki huo ni wa kihuni, hivyo kushindwa kuolewa na wanamuziki hao, wakidhani ni wahuni waliojaa uongo, utapeli na wasioweza kuishi katika ndoa.

Nani kasema? Siku hizi Bongo Fleva wanaoa bhana. Tena wanafunga ndoa zinazoacha gumzo nchi zima. Achana na yule Mfalme wao ambaye mpaka sasa amekuwa akipita huku na kule, wasanii wengine wa muziki huo kwa sasa wanaoa.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya wanawake walioolewa na wasanii wa Bongo Fleva na wanafurahia maisha yao ya ndoa. Yaani wanawake hawa wameondoa ile hofu ya kwamba muziki huo ni wa kihuni.

Amina-Ali Kiba

Amina Khalef Ahmed. Ndivyo anavyofahamika kule kwao Mombasa, Kenya. Ni mke halali wa Ali Kiba ambaye amefunga naye ndoa majuzi tu, Aprili 19.

Mrembo huyu mwenye staha zake, amethibitisha wanamuziki wa Bongo Fleva si wahuni, ni kutokana na uamuzi wa kukubali kuolewa na mwanaume wa tasnia hiyo.

Harusi ya Kiba ilikuwa gumzo maana ilirushwa mubashara na kipindi cha Sinema Zetu cha Azam TV, mitaani unaambiwa akina mama na wasichana karibu wote walikesha wakitazama.

Kazi imekuwa ngumu sasa kwani karibu kila mwanamke anayeolewa, naye anataka kurembwa kama Amina wa Ali Kiba.

Uwoya-Dogo Janja

Anaitwa Irene Uwoya. Ni maarufu zaidi huko kwenye filamu. Uwoya ambaye ni miongoni mwa warembo waliotokana na shindano la Miss Tanzania mwaka 2006, alifunga ndoa na Dogo Janja Oktoba mwaka jana.

Nani asiyemfahamu Dogo Janja ambaye siku hizi anajiita Janjaroo? Ni yule dogo fulani aliyekulia pale Manzese Tip Top kwa Madee. Ni mwanamuziki wa Bongo Fleva.

Uwoya ameingia katika orodha ya wanawake walioamua kuachana na fikra potofu kuwa wanaume wanaoimba muziki wa Bongo Fleva ni wahuni.

Waheeda-Mr Blue

Huyu ni mke wa mwanamuziki mwingine nguli wa Bongo Fleva, Mr. Blue ‘Mzee wa Mbwa Koko’. Nyota huyo aliyeanza muziki akiwa kijana mdogo wa kati ya miaka 12 na 15, alifunga ndoa na Waheeda Aprili 14, 2016. Unaambiwa mapenzi yao ni moto. Waheeda naye ameingia katika orodha ya kuthibitisha kuwa wanaume wanaoimba muziki wa Bongo Fleva si wahuni.

Helga-Mwana FA

Mwaka 2008 Mwana FA alitikisa nchi na kibao chake cha ‘Bado Nipo Nipo’. Kilikuwa gumzo nchi nzima. Katika kibao hicho aliimba kuwa hataoa mapema kutokana na changamoto zilizopo kwenye ndoa.

Alisema atasubiri sana.

Hakika mwaka FA ni mtu wa maneno yake. Ni hadi ilipopita miaka minane baadaye ndiyo alikubali kuwa nyakati zimefika na anastahili kuwa mume wa mtu. Alifunga ndoa na Mrembo Helga Juni 5, 2016. Inasisimua sana.

Sasa Helga naye ameingia katika orodha ya kuthubutu kujilipua kwa kuolewa na mwanaume anayeimba Bongo Fleva kwa kuweka mbali hisia potofu za baadhi ya watu kuwa wanamuziki hao wanakuwa ni wahuni.

Aisha-Luteni Karama

Aisha ni mke wa mwanamuziki mkongwe katika muziki wa Bongo Fleva Luteni Karama. Walifunga ndoa Mei 15, 2016 na mpaka sasa wanaishi pamoja. Aisha naye ameingia katika orodha ya wanawake wanaoamini kuwa wanaume wanaoimba muziki wa Bongo Fleva si wahuni.

Sabrah-Tunda Man

Sabra ni mke wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Tunda Man. Wawili hao walifunga ndoa Oktoba 15, 2016. Kabla ya hapo walikuwa wapenzi kwa muda mrefu hadi walipooana kwa ndoa hiyo inayoendelea kuthibitisha kuwa Bongo Fleva wanaoa vizuri tu.

Bado tu yule mfalme wao ambaye pamoja na kuwa na watoto zaidi ya wawili, bado hajaoa.

Remmy-AY

Inasemekana kule Rwanda asilimia zaidi ya 80 ya wanawake wa huko ni warembo. Yaani wanatofautiana kidogo. Kwamba huyu amemzidi yule kwa kitu fulani kidogo tu, lakini wote bomba.

Sasa nyota wa Bongo Fleva, AY hakutaka kuwa nyuma. Aliingia kwenye ardhi hiyo ya Rais Paul Kagame na kujiopolea mke matata.

Ni Remmy na walifunga ndoa yao Februari 10 mwaka huu. Remmy amethibitisha kuwa wanamuziki wa Bongo Fleva si wahuni kwa kukubali kuolewa na mwanamuziki wa tasnia hiyo, tena akitokea nchi jirani.

Veronica-Stamina

Pamoja na kuimba Kibamia akishirikiana na Roma Mkatoliki, bado Stamina naye amesafisha jina la muziki huo. Stamina alifunga ndoa na Veronica Peter, Mei 5 na kuongeza orodha ya wasanii wa muziki huo walioaga ukapera. Kwenye ndoa hiyo, Patroni wake alikuwa Roma wanayeunda naye Kundi la Rostam na mwaka jana ndio waliishika Fiesta nchi nzima. Wazee wa Kibamia.

Nancy-Roma

Nancy ni mke wa Mwana Bongo Fleva mwingine, Roma. Wawili hao walifunga ndoa Aprili 9, 2016 na kuthibitisha kuwa wanamuziki wa Bongo Fleva si wahuni. Nancy na Roma wamebarikiwa mtoto aitwaye, Ivan. Roma amemwandikia mwanaye nyimbo mbili; mmoja ulikuwa maalumu kwa Siku ya Kuzaliwa na unaitwa ‘Ivan’ huku mwingine ukiwa ni ule wa 2030.