Fani anayeyatamani makali na kazi ya AY

Khalfan Ali Rashid maarufu kwa kwa jina la ‘Fani’

Muktasari:

  • Hivyo ndivyo ilivyo kwa msanii Khalfan Ali Rashid maarufu kwa kwa jina la ‘Fani’ ambaye ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva kutoka Zanzibar, aliye na ndoto za kuwa mwanamuziki wa kimataifa, lakini akitoa burudani yake kwa ladha ya nyumbani.

INAJULIKANA wazi burudani ni suala la muhimu katika maisha ya kila siku.

Vilevile ni ajira kwa vijana wengi huku kundi kubwa likitamani kuingia katika fani hiyo kwa ajili ya kusaka mafanikio ya kimaisha.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa msanii Khalfan Ali Rashid maarufu kwa kwa jina la ‘Fani’ ambaye ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva kutoka Zanzibar, aliye na ndoto za kuwa mwanamuziki wa kimataifa, lakini akitoa burudani yake kwa ladha ya nyumbani.

Fani ni miongoni wa wasanii chipukizi wanaokuja kwa kasi, wakionyesha bidii katika fani hiyo ya muziki kwani kwa upande wake anaichukulia kama ajira iliyobeba matarajio ya kumfikisha mbali kimaisha.

Chipukizi huyu aliyeweza kwenda sambamba na Aslay katika Tamasha la Ziff lililofanyika Zanzibar hivi karibuni, alithibitisha kauli ya ‘Mcheza kwao hutunzwa’ kwani alisababisha jukwaa la Ziff kuchangamka zaidi pindi alipopanda jukwaani.

Kwa kifupi kwa wakazi wa Zanzibar, Fani, ndiye msanii mmoja anayewawakilisha vema katika Muziki wa Bongo Fleva.

Fani alianza muziki mwaka 2004 wakati huo akiwa na umri wa miaka 10 akisoma darasa la pili pale Shule ya Mwera Zanzibar, ila wimbo wake wa kwanza kurekodi ni ‘Kisa cha Mama ‘ alioutoa akiwa darasa la saba ambapo alibaini kuwa na mapenzi makubwa ya kuwa mwanamuziki wa kimataifa.

Anasema wimbo huo unaelezea tukio la kweli lililomkuta mama yake aliyepata ulemavu wa macho kutokana na kipigo cha mumewe huku akiwa na ujauzito wa miezi saba.

“Mama aliolewa na mwanajeshi, akapata ujauzito akawa anaomba hela ya matumizi, sasa kama unavyowajua wajawazito, wakapishana kauli na baba ambaye alipaniki na kumpiga mateke ya tumbo, hata ule ujauzito uliharibika na mama akapata upofu,” alisema Fani.

Licha ya muziki, Fani pia ana ndoto ya kuwa mtayarishaji wa muziki akitamani kuwasaidia wasanii wachanga akiwa na kumbukumbu kuwa hata yeye alianza kama wao.

Msanii huyo anasema anatamani kufuata na kufikia mafanikio ya baadhi ya wasanii akiwamo AY na Diamond Platnumz.

Fani anayependa zaidi miondoko ya Bongo Fleva , anaeleza kuwa muziki huo umemfundisha mengi na kumkutanisha na wasanii maarufu ambao hakutarajia kukutana nao, akibainisha kwamba hiyo imemwezesha sasa mlango wake wa mafanikio kuanza kufunguka.

Anasema kuwa msanii yeyote ili afanikiwe kimuziki, ni lazima awe na vionjo tofauti na kutumia ubunifu ambao wasanii wengi hushindwa kuutumia na anayeweza hilo atakuwa na fursa kubwa ya kukubalika kitaifa na kimataifa.

Fani aliwataja baadhi ya wanamuziki waliotumia ubunifu hatimaye kufikia walipo sasa kuwa ni pamoja na AY, Ali Kiba na Diamond.

Hadi sasa ana nyimbo tano; Sangoma, Naumwa, I love U, Tukikutana na Nimerogwa.

Nyimbo alizoshirikishwa ni ‘Unavimba Unaringa ‘ ameimba na Chid Yobo, ‘Nani Super Staa’ alioshirikishwa na Nassir Vanilla.

Fani anabainisha kuwa wimbo uliomfanya atambulike ni Sangoma ambao aliutoa mwaka 2012 na kumpata Tuzo ya Mwanamuziki Bora Zanzibar.

Atamani kolabo na AY

“Naheshimu kazi ya kila msanii aliyenitangulia na hata anayekuja nyuma yangu, ila natamani sana kufanya kazi na AY,” alisema.

Matarajio yake kimuziki

Kuhusu matarajio yake kimuziki, Fani anasema ni kutambulika kimataifa na kuwasaidia vijana wenzake wenye vipaji kama chake na pia kumiliki studio yake binafsi.

Pia, Fani anasema soko lake la muziki limeegemea Zanzibar kuliko Bara kutokana na kuwa mzaliwa wa visiwani humo, lakini amepania sasa alikamate na soko la Bara.

Wito kwa wasanii

Msanii huyo anawataka wasanii kufanya kazi badala ya kuingia kwenye ugomvi na vituko vya hapa na pale visivyokuwa na maana badala yake kushirikiana kuitangaza Tanzania kimataifa.

Anasema wasanii wengi wa muziki wamekuwa wakilewa umaarufu na kusahau kuelimisha jamii au kuburudisha, hivyo wakijikuta wanaangukia kwenye tabia zisizofaa ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya.

Aliwatoa hofu wanaodhani kuwa wanaofanya muziki ni wahuni akisema ni moja ya ajira kubwa kwa vijana wengi wenye vipaji ambao hujipatia ujira na mafanikio zaidi.

Fani anatoa ushauri kwa wanaohitaji kuwa mwanamuziki kufanya bidii katika fani ya muziki, badala ya kukata tamaa akiwataka kutumia fursa walizonazo na kuongeza juhudi katika kusaka mafanikio na kukuza muziki unazidi kukubalika nchini.

Anawaomba wadau wote wa muziki kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta mafanikio nchini kwani nchi zinazoendelea hufanikiwa kwa ushirikiano baina yao na kuleta mafanikio katika nchi yao .

“Wivu ni muhimu katika maendeleo, lakini tusijizoeshe. Ukiona mtu amefanikiwa mpongeze au mdadisi ujue katumia njia ipi kufanikiwa ili nawe pia upate kufanikiwa kama yeye,”alisema Fani. Mwanaspoti linamtakia kila la heri Fani katika kazi yake yamuziki.