Ebitoke yeye na Ben Pol tu

Tuesday September 12 2017

 

MCHEKESHAJI Ebitoke bado amemng’ang’ania mfalme wa R&B nchini, Ben Pol akidai anaendelea kumtunzia usichana wake hadi atakapokuja kuolewa na mwimbaji huyo.

Ebitoke amekuwa akisema kila mara kwamba huwa anaumia roho anaposikia msichana anajitangaza kuwa ni mpenzi wa Ben Pol kwa madai kwamba lengo lake ni kuja kuolewa na kujenga familia na mkali huyo wa R&B.

Hata hivyo, Ben Pol mara kadhaa amekaririwa akisema, Ebitoke ambaye majina yake kamili ni Anna Exavery anafanya utani tu na alimwomba amtumie kutangaza kazi zake na anashukuru kuona amefanikiwa japo Ebitoke anasisitiza Ben ni wake.

“Lengo langu lipo pale pale kuomba Mungu anisaidie nije kuolewa na Ben Pol nampenda sana, naamini mambo yataenda vizuri na mipango huwa sipendi watu wajue, kuhusu suala la usichana wangu sipendi kuliongelea tena,” alisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 19 alisema moja ya mafanikio yake kisanii ni kumtegemea sana Mungu, kuwa na nidhamu, kujiheshimu na kujituma chini ya menejimenti inayomwongoza vyema na kwamba hatalewa sifa mpaka afike kule anakokutaka.