Dulla Makabila buaaana!

Monday January 8 2018

 

By RHOBI CHACHA

UKIACHANA na Msaga Sumu, hakuna msanii mwingine wa muziki wa Singeli aliyeweza kuwateka mashabiki wa miondoko hiyo na hata wale wa miondoko mingine kama Dulla Makabila.

Ndio, kazi zake murua kuanzia Hujaulamba, Utatoa Hutoi na hata ule uliozaa jina la Makabila ni moja ya kazi zilizomtangaza sana mwimbaji huyo.

Mbali na kutoa vibao hivyo vikali na vinazoendelea kusumbua hewani, mkali huyo wa Singeli bwana ana mikasa kibao na Mwanaspoti limepiga stori naye na kufunguka mambo kadhaa ambayo mashabiki wake hawakuwa wakiyafahamu.

Mwimbaji huyo ambaye kwa sasa anajihusisha kimapenzi na mwigizaji wa filamu wa kike, Husna Idd ‘Sajenti’ mwenye watoto wawili, ambao Dulla amesema hajali sana ishu ya kipenzi chake hicho kuwa na watoto zaidi ya kuyafaidi mapenzi.

Katika kupiga mahojiano hayo, Dulla ameanza kwa kusema kwa kuwatahadharisha watu ambao wanamsema analelewa na Husna kwa vile eti  amezidiwa umri akitaka kauli hiyo ifutwe kabisa kwani yeye ni mchakarikaji na Mwanaume Mashine. Endelea naye...!

MWANASPOTI: Inasemekana wewe ni mtu wa mademu sana, hasa mashabiki zako?

DULLA: Sio kweli bana, hizo stori tu za kwenye kahawa, mi, najiheshimu sana!

MWANASPOTI: Kuna habari zinadai mnagombana sana na Husna kwa sababu ya wivu kwake kupindukia, hii imekaaje?

DULLA: Jamani bila ya wivu kwenye mapenzi hayanogi. Kama wivu hakuna mjue nyie mnadanganyana, lakini sifikii kupitiliza.

MWANASPOTI: Kwa siku huwa unaoga mara ngapi?

DULLA: Haahahaa..Inategemea mara mbili au tatu hasa joto likizidi, pia kuna wakati mwingine hata mara moja.

MWANASPOTI: Ulishawahi kulizwa kwenye mapenzi?

DULLA: Sana tu, tena usinikumbushe nikaanza kulia saahizi.

MWANASPOTI: Marafiki zako ni watu wa aina gani?

DULLA: Wanaopenda maendeleo na wenye kufikiri kwa upeo mkubwa sana.

MWANASPOTI: Chakula gani unapendelea kula ama hata kukipika mwenyewe?

DULLA: Ugali wa Dona kwa samaki wa kukaangwa, kwa mfano nikila mlo huo mapema, kutwa nzima nashindia kunywa maji tu hadi jioni.

MWANASPOTI: Unapokuwa na hasira cha kwanza unafanya nini?

DULLA: Mara nyingi napenda kuondoka eneo la tukio ili kuepusha shari.

MWANASPOTI: Mara ya mwisho kula chakula kwa mama lishe ni lini?

DULLA: Yaani mpaka sasa nakula tena napendaga ukoko wa wali, siwezi kuacha hiyo hata kama ni staa.

MWANASPOTI: Ukiwa nyumbani unapenda kulala wapi mbali na kitandani?

DULLA: Yaani mimi tabia yangu ni nyingine ni kupenda kulala kwenye korido ndio mchezo wangu.

MWANASPOTI: Kitu gani kimewahi kukuumiza maishani?

DULLA: Niliponyang’anywa maiki na kuzomewa kwa kuonekana sijui kuimba nilipopanda jukwaani kwa mara ya kwanza.

MWANASPOTI: Nini tutarajie mwaka 2018.

DULLA: Sina maneno mengi, mimi ni  vitendo, mtaona.