Duh! hawa Wameishia kunawa tu

Muktasari:

Japo zipo tuzo za aina nyingi, za kitaifa na kimataifa, ukweli unabaki, kila moja inao uzito wake. Zipo pia tuzo zinazomzidishia msanii heshima na kuinogesha ‘brandi’ yake na zipo zile humpa mzuka msanii azidi kupambana.

LICHA ya rekodi za mauzo ya muziki wake pamoja na wingi wa idadi wa shoo apatazo msanii, ubora na mafaniko ya msanii yeyote hupimwa pia katika mizani ya tuzo mbalimbali anazoshinda.

Japo zipo tuzo za aina nyingi, za kitaifa na kimataifa, ukweli unabaki, kila moja inao uzito wake. Zipo pia tuzo zinazomzidishia msanii heshima na kuinogesha ‘brandi’ yake na zipo zile humpa mzuka msanii azidi kupambana.

Mwigizaji mwenye asili ya Kenya, Lupita Ny’ongo aliposhinda tuzo za Oscars, ghafla zilimpa ustaa na michongo ya kutokea kwenye filamu nyinginezo kubwa. Aidha brandi yake ilipanuka na kumfanya kuwa miongoni mwa waigizaji wanaovutia dili kubwa za biashara ya matangazo.

Kwenye sanaa ya muziki, kushinda Grammy Awards huwa ni habari nyingine kabisa. Tuzo hizi ndizo zinazotajwa kuwa zenye hadhi ya juu na heshima kuliko nyingine zozote chini ya jua.

Zikiwa pia ndio tuzo kongwe zaidi (ziliasisiwa Mei 1959), Grammy ziliadhimisha makala yake ya 60 mapema Januari. Ingawa tuzo hizi hutolewa kwa vigezo vya ubora na mafanikio ya kazi za mwanamuziki husika, wapo wasanii mastaa waliofanya vyema kwa miaka mingi ila hawakuwahi kubahatika kutunukiwa tuzo hizo licha ya michango yao mikubwa kwenye sanaa.

BOB MARLEY

Mwanaye Damian Marley alilitwaa tuzo hiyo kwa mara nyingine mwaka huu kwenye kitengo cha Albamu Bora ya Reggae.

Hata hivyo, wadau wengi wamekashifu wakisisitiza albamu ya ‘Chronixx’ ndiyo iliyokuwa bora zaidi. Lakini Damian akifurahia tuzo hiyo, alisema mtu aliyestahili zaidi kuipata ila hakubahatika ni babake, marehemu Bob Marley.

Licha ya Bob kuuza mamilioni ya albamu zake 10 maarufu zikiwamo ‘Redemption Song’, ‘Exodus’, ‘Get Up, Stand Up’, ‘The Wailing Wailers’ kote ulimwenguni, hakuwahi kutuzwa Grammy.

KATTY PERRY

Ni miogoni mwa wasanii wakubwa wanaotambulika kwa muziki wake wa aina ya ‘Pop Rock’.

Albamu yake ya mwaka 2010 ‘Teenage Dream’ ilivunja rekodi baada ya kuwa na nyimbo tano zilizokamata nafasi ya kwanza kwenye chati za BillBoards na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa kike kufikia hilo.

Albamu hiyo ndiyo iliyotarajiwa na wengi ingemshindia Grammy, lakini cha kushangaza alitoka kavu. Ameteuliwa mara 11 kuwania tuzo hizo ila mpaka kwenye hajabahatika kushinda.

NICKI MINAJ

Licha yake kuendelea kufanya vyema kwenye muziki wa Hip Hop kwa zaidi ya miaka minane, mwanadada, Nicki Minaj, hajawahi kufanikiwa kutuzwa Grammy.

Tangu mwaka 2011, Minaj kateuliwa mara 10 kuwania tuzo hizo kwenye vipengele mbalimbali, lakini kila wakati mambo humkaliwa vibay.

Nicki kauza mamilioni ya kopi za albamu yake huku ile ya ‘Pink Friday’ ambayo ni kati ya tatu alizofanya hadi kufikia sasa, ikimwekea rekodi ya kuuza zaidi ya kopi milioni moja.

TUPAC SHAKUR

Tupac Amaru Shakur anakumbukwa kama mmoja wa waasisi wa mtindo wa Hip Hop.

Kazi zake zilikuwa za uhakika na zilizomfanya kuwa milionea mapema kutokana na mauzo mazuri ya rekodi zake chungu nzima.

Katika taaluma yake ya muziki iliyodumu kwa miaka mitano, Tupac aliachia zaidi ya hiti 15, lakini hakuwahi kutuzwa Grammy licha ya kuteuliwa mara nne kuwania kwenye vipengele tofauti kabla ya kifo chake kutokea mwaka 1996.

NOTORIUS B.I.G

Alikuwa hasimu mkubwa wa Tupac. Wawili hawa waliuwasha moto wa ushindani wa fani hiyo na hadi kufikia vifo vyao vilivyosababishwa na tofauti ya makundi yao, walikuwa wamefanya kazi ya kutosha kuwashindia tuzo zozote zile.

Albamu mbili za Notorius ‘Ready To Die’ na ‘Life After Death’ ndizo zilizomweka kwenye chati na kusababisha kuteuliwa mara nne kwa tuzo hizo, ila hakuwahi kushinda.

SNOOP DOGG

Ni miongoni mwa wakongwe wa Hip Hop aliyerithi mikoba ya Notorius na Tupac lakini pia licha ya umaarufu wake uliotokana na ukubwa wa hiti zake nyingi hasa za miaka ya nyuma, Grammy haijawahi kumtambua. Aliteuliwa mara 15 kuwania tuzo hizo katika vipengele tofauti ila kwa zote kachemsha.

BRIAN MCKNIGHT

Mwanamuziki huyu wa R&B ametuliwa kuwania tuzo za Grammy mara 16 ila mpaka sasa hajawahi kushinda. Anashikilia rekodi ya kuteuliwa mara nyingi zaidi kwa tuzo hizi bila ya kushinda chochote, anafuatiwa na Snoop.

NAS

Ni rapa wa Marekani ambaye aliamua kupunguza kasi ya kufanya muziki baada ya kutesa kwa zaidi ya miongo miwili.

Nas hajawahi kushinda Grammy licha ya kuteuliwa kuwania mara 13. Mwaka 1994 ndio ambao alipewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kupitia albamu ya ‘Illmatic’ iliyofanya vizuri sana, ikawa yaleyale.

BUSTA RYMES

Huwezi kuwazungumiza ma-MC wa muda mrefu bila ya kumtaja Busta ambaye amedumu kwenye fani kwa zaidi ya miaka 25 sasa.

Ndiye rapa mwenye kasi zaidi katika michano na aliteuliwa mara 11 kuwania Grammy, lakini hakuna hata moja aliyobahatika kupata.

Uteuzi wake wa mara ya mwisho ulikuja mwaka 2012 kuwania vipenge vya Best Rap Performance na Best Rap Song kupitia wimbo wake wa ‘Look at Me Now’ na kama ilivyokuwa miaka ya awali aliishia kunawa tu kwani kula walikula wengine.