Dude naye amlilia ticha

Tuesday June 12 2018

 

NI kweli kina nafsi itaonja mauti, lakini kifo hakizoeleki. Mkongwe wa sanaa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirika la Wasanii (SHIWATAS) Cassim Twalib ‘Teacher’ ameendelea kuwaliza wasanii aliowaibua, baada ya kufariki dunia wikiendi iliyopita.

Mmoja ya wasanii wanaomlilia mwasisi wa kundi la Splended lililowaibua wakali kibao wanaotamba kwa sasa nchini ni, Kulwa Kikumba ‘Dude’, ambaye alisema ameshtushwa na kifo Teacher na daima atamkumbuka kwa kumtoa mafichoni.

Dude alifichua alipotua Splended aliwakuta wasanii kama Dr Cheni, Billy, Mzee Kipara, Mama Haambiliki, Chekibud na kupokelewa na Ticha na kumpatia nafasi, hivyo ni vigumu kumsahau hata kama kufa ni sehemu ya maumbile ya binadamu.

Mkongwe huyo alifariki dunia Jumamosi kwenye Hospitali ya Amana akisumbuliwa na ugonjwa wa Moyo na kwenda kuzikwa katika Kijiji cha Mangesangi Bagamoyo.