Diva afunguka penzi lake kwa Neymar

Muktasari:

  • David Lucca ukipenda mwite Davi ni mtoto wa Neymar aliyezaliwa Agosti 24, 2011. Hivyo anakaribia kutimiza umri wa miaka saba. Mrembo wa Kibrazil, Carolina Nogueira Dantas, 25, ndiye mama wa Davi. Hata hivyo, Carolina na Neymar si wapenzi tena, walishamwagana.

JUNI 28, mwaka huu, mmoja wa burudani za soka ulimwenguni, Neymar da Silva Santos Junior, ukipenda Neymar Jr au kifupi tu Neymar, alitupia picha kwenye akaunti yake ya Instagram, akiwa na mtoto wake wa kiume, David Lucca da Silva Santos.

David Lucca ukipenda mwite Davi ni mtoto wa Neymar aliyezaliwa Agosti 24, 2011. Hivyo anakaribia kutimiza umri wa miaka saba. Mrembo wa Kibrazil, Carolina Nogueira Dantas, 25, ndiye mama wa Davi. Hata hivyo, Carolina na Neymar si wapenzi tena, walishamwagana.

Neymar, 26, ni raia wa Brazil. Kutoka nchi hiyo mpaka Tanzania, Taifa lenye bendera ya rangi nne, ni maili 5,900. Inachukua saa 11 na dakika 34 hadi saa 12 angani kwa ndege isiyosinzia kama Boeing 737-8 Dreamliner ambayo Tanzania imeingiza juzi kati tu hapa kutoka Brazil moja kwa moja hadi kufika Tanzania.

Ndani ya Tanzania yenye maji ya Bahari ya Hindi, yupo mrembo mtangazaji wa Clouds FM, kipindi cha Ala za Roho, Diva Giselle Malinzi, zamani aliitwa Loveness kabla ya kuapa mahakamani ili kuondoa jina la Loveness kwenye vyeti na vitambulisho vyake kisha kutambulika rasmi kama Diva.

Basi Diva anateseka kwenye ulimwengu wa hisia za mapenzi. Anaota kuumiliki moyo wa Neymar. Anampenda sana janki huyo wa maji ya Bahari ya Atlantic. Kisa Neymar, Diva anasema kuna wakati hutamani angezaliwa Brazil, ingawa anajivunia kuwa Mtanzania.

Juni 29, mwaka huu, Diva kupitia akaunti yake ya Instagram, alitupia picha ya Neymar na Davi ambayo Neymar aliiposti Juni 28, kisha Diva akaandika maneno yafuatayo:

“Mpenzi Neymar, nitaolewa na wewe hata ndotoni. Na mwanao nitamlea hata ndotoni. Hicho ni kiwango cha mapenzi niliyonayo kwa ajili yako. Ni katika ndoto zangu.” Maneno hayo aliyachanganya Kiingereza na Kiswahili. Nimeyaweka kwa Kiswahili kilichonyooka.

Kwa maneno hayo, Diva anatamani nafasi ya Carolina aliyezaa na Neymar? Au ni utani tu ili kuwaburudisha wafuasi wake 1.9 milioni waliojiunga kwenye akaunti yake ya Instagram? Mazungumzo na Diva yanadhihirisha hakuna utani.

HISIA ZA NDANI KABISA

Nilipofanya mazungumzo na Diva kuhusu hisia zake kwa Neymar kama ni kweli au utani, alijibu: “Nazungumza upendo halisi, nampenda Neymar. He is my crush. Neymar is my lifetime crush.”

Diva anasema Neymar ni ‘crush’ wake. Kwa Kiswahili, crush humaanisha hisia zinazokua kadiri muda unavyosogea. Unampenda mtu, sasa jinsi unavyomtazama au kumfuatilia unajikuta hisia zinaongezeka na kumpenda zaidi. Hivyo, Diva anasema hisia zake kwa Neymar ni za maisha yake yote.

Kuhusu tafsiri ya maneno yake kwamba ataolewa na Neymar ndotoni na hata mtoto wake atamlea kwenye ndoto, Diva anafafanua: “Unakuwa na hisia za muda mrefu na unaona haziwi, kwa hiyo unakuwa huna cha kufanya zaidi ya kumbeba ndotoni.

“Katika maisha ya ndoto nipo tayari kwa chochote, angalau tu moyo wangu unaridhika kwa kuzingatia kuwa yupo hai. Kwa hili sifanyi utani, nampenda sana. Huwa natamani yote ninayofikiria kuhusu Neymar yatokee kuwa kweli.”

Kutokana na hisia ambazo Diva yupo nazo, huwa anafikiri kwamba kuna siku atakutana na Neymar na kuzungumza mapenzi au mambo tu ya kawaida? Diva anajibu: “Sijui, ila unajua maisha, kwenye maisha chochote kinaweza kutokea. Ila nahisi nikikutana na Neymar uso kwa uso naweza kuzimia au naweza kufa kwa presha.

“Ni kwa sababu nina hisia za juu sana kwake. Nahisi nitashindwa kujimudu au nitapagawa kabisa. Pamoja na hivyo nina matumaini kwamba siku moja nitaweza kuonana naye, ingawa siwezi kueleza hasa nini kitatokea.”

ALIANZA VIPI KUMPENDA

Diva anasema: “Nina rafiki yangu anaitwa Richard Wambura, ni mtoto wa Michael Wambura. Richard ndiye alinionyesha video ya Neymar YouTube kwa mara ya kwanza. Kuanzia hapo nikajihisi navutiwa naye. Hisia za kumpenda ziliongezeka hadi kufikia kumuona ndiye mwanaume wa ndoto zangu.”

Hisia za Diva zipo wazi sana. Anamsema Neymar mitandaoni na hata redioni akitangaza. Haidhaniwi kama kuna mwanaume ambaye anaweza kumvumilia mwanamke wake, ambaye anaonesha wazi kuwa anampenda mwanaume mwingine. Je, Diva ana mpenzi? Na kama anaye, huyo mpenzi wake anapokeaje hizo hisia zake kwa Neymar?

Diva: “Nina mpenzi. Tofauti ya wapenzi wangu waliopita na huyu wa sasa, yeye sio msanii wala mtu maarufu. Ni mtu mzima na ni mwelewa sana. Uzuri hata yeye anampenda Neymar. Anajua nampenda sana Neymar. Akiniona ninavyohangaika nikimuona Neymar yeye huwa ananicheka tu.”

Diva anasema kuwa mpenzi wake wa sasa hakerwi na hisia zake kwa Neymar kiasi kwamba, ikitokea siku anapanga safari ya kwenda nchi yoyote kwa ajili ya kukutana na Neymar, anaweza hata kumlipia nauli na kumgharamia kila kitu, maana itakuwa anakwenda kutimiza furaha yake, kwani mwanaume wake wa sasa hutaka kumwona anafurahi muda wote.

Ni hisia katika mapenzi ya kufikirika aliyonayo Diva kwa Neymar. Ikitokea Diva anakutana na Neymar, kisha inatokea Neymar naye anavutiwa na Diva, hivyo kuomba wawe wapenzi. Upi utakuwa uamuzi wa Diva ukizingatia ana mpenzi wake tayari?

Diva anajibu kuwa hatajiuliza mara mbili zaidi kuingia mapenzini na Neymar, kisha anaongeza: “Nitamuomba msamaha mpenzi wangu wa sasa, nitamwambia anisamehe sana, maana linapokuja suala la Neymar itabidi tu anisamehe sana.”

Brazil ilikuwa kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2018, zinazoendelea Russia kabla ya kutolewa hatua ya robo fainali na Ubelgiji kwa kufungwa mabao 2-1. Je, Diva hakufikiri kuwa ilikuwa nafasi nzuri kwake kwenda Russia ili angalau kutimiza ndoto zake za kukutana uso kwa uso na Neymar?

Anajibu: “Sikuwa na mpango wa kwenda Russia mwaka huu kwa sababu nimebanwa na kazi pamoja na biashara zangu. Hata hivyo, wakati mwingine nikipata nafasi nitakwenda kwenye nchi atakayokuwa anacheza, hata akiwa na klabu yake.

“Na ninachojua ni kwamba nikimwona naweza kushindwa kusema chochote. Naweza kuishia tu kumsalimia halafu nisiwe na neno lolote. Unajua ukimpenda sana mtu tena kwa hisia za muda mrefu, siku ukimwona unaweza kukosa neno la kumwambia.”

KUCHORA TATTOO YA NEYMAR

Diva anasema kuwa hivi karibuni atachora kifuani tattoo ya jina la Neymar ili kuonesha kuwa kweli anampenda mwanasoka huyo na anataka hilo liwe wazi kwa kila mtu, kwamba Neymar hana mbadala kwenye moyo wake.

Akielezea zaidi anavyoguswa na Neymar, Diva anasema, hufuatilia mechi ambazo Neymar anacheza na akichezewa rafu huwa anamia sana. “Mtu akitaka aniumize moyo ampige Neymar mtama, huwa nahisi moyo unavuja damu,” anasema Diva.

Anaendelea: “Najua Neymar huwa anajiangusha sana, lakini hata ninapomuona ameanguka, mimi moyo na mwili unauma, naishia tu kusema msiniumizie. Msimkate mitama. Nasema hivyo mwenyewe kwenye televisheni. Naumia sana Neymar akichezewa vibaya uwanjani.”

Diva anasema timu anayoshabikia ni ile anayochezea Neymar. Anaeleza: “Naipenda Timu ya Taifa ya Brazil. Klabu nilikuwa Barcelona wakati Neymar akichezea, ila tangu alipohamia PSG ya Ufaransa na mimi nimehama timu.

“Ni vile wanasema ulipo tupo, na mimi kwa Neymar popote alipo nipo. Akihama timu namfuata hukohuko. Neymar ndiye ananifanya nitazame mpira zaidi.”

Ukimwacha Neymar, kuna staa mwingine yeyote wa soka ambaye Diva anampenda? Jibu lake ni hili: “Kimapenzi ni Neymar tu. Nilimpenda Neymar nilipomwona tu mara ya kwanza. Wapo wengine nawapenda kama wachezaji tu lakini sio kimapenzi.

“Nampenda Memphis Depay, pia Jesse Lingard. Zamani nilikuwa nampenda sana Ronaldinho Gaucho. Kuna wachezaji wengi tu huwa nawapenda kwa jinsi wanavyocheza, ila Neymar nampenda kwa kila kitu, kama mchezaji na vile jinsi alivyo.”

ANAVUTIWA NA AJIBU

Kwa wachezaji wa Tanzania, Diva anavutiwa na nani? Haya hapa ni majibu yake: “Sio kimapenzi, ila navutiwa na jinsi anavyocheza. Napenda nidhamu yake na mtindo wake wa maisha, nampenda sana Ibrahim Ajibu wa Yanga.”

Kuna vitu vyovyote ambavyo Ajibu na Neymar wanafanana mpaka kumfanya Diva awapende wote? Anajibu: “Hapana, hawafanani. Neymar ni Neymar. Nampenda kwa kila kitu. Ila kwa Tanzania navutiwa na Ajibu anavyocheza na jinsi alivyo na nidhamu. Nilikuwa nampenda pia Jerry Tegete, alikuwa rafiki yangu ila sasa hivi ni Ajibu peke yake hapa Bongo.

“Ukiniambia niseme tofauti ya ninavyompenda Neymar na Ajibu ni kwamba Neymar nampenda kimapenzi kabisa. Nimeanguka kimapenzi kwake. Ajibu yeye nampenda kama shabiki. Hata kwenye kucheza hawafanani. Japokuwa Neymar anajiangusha sana uwanjani, lakini ni namba moja kwangu.”

MAPENZI YA KUJIWAZIA

Mwandishi mkubwa wa Marekani, Alice Walker amepata kusema kuwa, ulimwengu wa kufikirika ambao kila mmoja huuwazia ni mzuri sana na ukiupenda utagundua kwamba, ni ulimwengu huru na unaweza kupata kila kitu unachotamani ndani ya fikra zako lakini si kwenye dunia ya kawaida.

Ni kwa maana hiyo, Diva kwenye ulimwengu wa kufikirika anamuona Neymar ni mpenzi wake kabisa. Anamvuta kwenye ndoto zake, anawaza ndoa naye na hata kumzalia mtoto. Hisia hizo wapo nazo wengi. Wapo wanaogelea mapenzi wengine utajiri.

Yupo anayeiota nyumba fulani, mwingine kuna gari linamnyima usingizi, akikaa anawaza akiwa analiendesha. Msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’, aliwahi kuchanganyikiwa kwa penzi la bitozi wa Pop, Justin Bieber, lakini kwa sasa bila shaka mawazo hayo yamekwisha, kwani anaelekea kufunga ndoa na CEO wa E Media, Francis Ciza ‘Majay’.

Kwa Diva anaamini hisia zake kwa Neymar hazitokufa, zitadumu maisha yake yote na anaongeza kwamba anachotaka kufanya kwa sasa ni kuanza kujifunza Kireno kwa sababu ndiyo lugha anayozungumza Neymar ili siku wakikutana wazungumze na kuelewana.

“Nafikiria wapi nitakwenda kujifunza Kireno. Nafuatilia mahojiano na Neymar, mara nyingi hazungumzi Kiingereza. Kwa hiyo nitajifunza Kireno ili tukikutana tuzungumze na kuelewana,” anasema Diva na kuongeza:

“Natamani siku moja kwenye sherehe yake ya kuzaliwa nimpe zawadi ya ua kubwa jekundu. Ile Red Rose yenyewe kabisa. Katika ulimwengu wa ndoto natamani nimpe zawadi ya kumzalia mtoto japo mmoja.”