Coleen kwa Rooney kama uji na mgonjwa

Muktasari:

Baada ya kuibuka tetesi kwamba ndoa yao imevunjika, Coleen amejitokeza hadharani akiwa na pete ya ndoa.

London, England. Coleen Rooney amevunja ukimya kuhusu ndoa yake na mwanasoka nguli wa timu ya Everton, Wayne Rooney.
Baada ya kuibuka tetesi kwamba ndoa yao imevunjika, Coleen amejitokeza hadharani akiwa na pete ya ndoa.
Pia, mwanamitindo huyo aliweka picha ya familia kwenye mtandao wa Facebook wakiwa na nyuso za furaha.
Coleen mwenye miaka 31, amempa nafasi ya pili nahodha huyo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England baada ya kukutwa na mwanamke mwingine.
“Wayne ni baba bora, lakini hawezi kufanya mambo yote mazuri, wakati mwingine anakosea kama binadamu,” alisema Coleen ambaye alianza uhusiano na nyota huyo tangu wakiwa na umri mdogo.
Coleen amewajibu wabaya wake kwa kutoa sababu za kuonekana hana pete ya ndoa katika siku za karibuni.
Mrembo huyo alisema ndoa yao ipo imara, lakini hawezi kuvaa pete ya ndoa mara kwa mara kutokana na mazingira.
“Siwezi kuwa navaa pete ya ndoa mara kwa mara kwa  mfano huwa navua ninapokuwa katika mazoezi ya viungo “gym”, alisema mama huyo wa watoto watatu wa kiume
Kai (8), Klay, (4) na Kit mwenye miezi 22.
Coleen anayetarajia kujifungua mtoto wa nne alisema ndoa yao imekuwa ikiandamwa na matukio baada ya Rooney kuchepuka na mfanyabiashara Laura Simpson wakati mrembo huyo akiwa Dubai kwa mapumziko.
Nguli huyo alikutwa ndani ya gari ya Laura akiwa amelewa baada ya kuponda raha usiku. Hata hivyo muda mfupi baadaye Rooney na Laura walikanusha kuwa na uhusiano.