Cheki Ramadhan ilivyowabamba mastaa Bongo

MFUNGO wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaendelea mdogo mdogo na leo ni chungu cha nane kwa Waislamu wote nchini wanaotimiza moja ya nguzo muhimu za dini hiyo.

Mwezi wa Ramadhan ni nguzo ya nne kati ya nguzo tano za Uislam na ni mwezi wa toba, waumini hufunga kwa kujinyima kipindi chote cha mwezi ili kumrudia Mola wao sambamba na kujikita katika kutenda mema na hasa kutoa kwa wingi kwa lengo la kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.

Ni kipindi chenye utulivu mkubwa. Kila mwenye hofu ya Allah SW hutulia na kufanya toba. Hii sio kwa wachache, bali kwa wote.

Hivyo basi Mwanaspoti linakuletea orodha ya baadhi ya mastaa wa Kibongo walivyoukaribisha mwezi kwa aina tofauti.

RIYAMA ALLY

“Mwezi huu nimeupokea vizuri kabisa na huwa naupenda sana kutokana na asilimia kubwa ya watu kubadilika kimavazi na hata kuzidisha ibada. Napenda huu ungekuwa kwa miezi yote 12, ingependeza kabisa.”

WEMA SEPETU

“Nimeupokea vizuri huu mwezi na nimejaaliwa kufunga, hivyo nawakumbusha tu Waislamu wenzangu huu mwezi ni lazima kufunga endapo Mwenyezi Mungu ametupa uzima na afya njema. Tunafanya mambo mengi ndani ya miezi 11, tunashindwaje kufunga mwezi mmoja?”

GABO

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kufanga mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan. Nimeupokea vizuri na napenda kuwaambia Waislamu wenzangu tusiishie kufanya mema mwezi huu, inabidi tuendelee kwa miezi yote, kwani kujistiri, kuswali na kutubu haitakiwi mwezi huu tu.”

LAVALAVA

“Mwezi huu wa Ramadhan nashukuru nimeupokea salama kabisa na nafunga maana ni moja ya nguzo ya Kiislamu, hivyo nawatakia kila la kheri Waislamu wote na wasio Waislamu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan. Nawakumbusha tu kufunga na ibada ni muhimu sana.”

SNURA

“Mwezi huu wa Ramadhan nimeupokea vizuri sana na nafunga kama kawaida yangu kila mwaka, ila nawashauri wasanii wenzangu na hata wasio wasanii tujaribu kujiheshimu kimavazi na hata kimaongezi ili kuweza kulinda swaumu zetu. Pia isiwe kwa mwezi huu tu bali hata miezi mingine tufanye hivyo.”

MWANA FA

“Mimi ni mtoto wa Kiislamu na nashukuru sana nimeupokea vyema mwezi wa Ramadhan kwani ni mwezi ambao huwa nausubiri kwa hamu kila mwaka.

Waislamu wenzangu tujitahidi kufunga na kufuata maadili mema na hata kwa wenzetu wa dini nyingine, wajaribu kutuepushia vishawishi vya hapa na pale ili tusiharibu swaumu ya mtu. Pia tusiache kuswali kwa sisi Waislamu tunaofunga na hata wasiofunga.”