Baba wa Meghan aibuka, atema shombo

Prince Harry na Meghan Markle wameshakamilisha shughuli na sasa wamejichimbia kula bata tu. Lakini, huku nyuma wazushi bado wanaendelea kufuatilia nyendo za wazazi wa Meghan hasa baba yake, Thomas Markle.

Mzee Merkle ameonyesha kukerwa kwa jinsi anavyofuatiliwa na vyombo vya habari wakati tayari ameshatimiza jukumu la kumuozesha binti yake tena kwenye familia ya kifalme.

Juzi, Markle aliamua kuvunja ukimya na kufunguka baada ya kusambazwa kwa picha akipiga bia na washkaji zake kisha zikarushwa katika mitandao.

“Sielewi kwanini wanafuatilia maisha yangu, nimeshaozesha binti yangu basi kazi imeisha. Tulikuwa tunakunywa kwa raha zetu, sasa mtu anakuja kupiga picha halafu azisambaze, niwaambie wazi mimi sio maarufu kama wanadhani. Binti yangu ndio maarufu hivyo, kama mnataka habari mfuateni yeye,” alisema.

Katy Perry avunja ukimya gauni la Meghan

Wakati watu wakiendelea kuwamwagia sifa Prince Harry na Meghan, Katy Perry amekuja na mtazamo tofauti kabisa unaambiwa.

Katy ameweka wazi kuwa hajavutiwa na gauni la Meghan na halina hadhi ya kuvaliwa na mwanamke wa familia ya kifalme.

Katy alilinganisha gauni hilo na lile alilovaa Kate mwaka 2011 wakati akiolewa na Prince William na kudai kuwa hilo lilikuwa bora zaidi.

“Nahisi lilihitaji marekebisho zaidi kwa jinsi lilivyokuwa, halikustahili kuvaliwa na mwanamke ndani ya familia ya kifalme,” alitema shombo.

Inadaiwa kuwa Meghan alinunua mwenyewe gauni hilo lililotengenezwa na mbuninifu Clare Waight Keller.