VIDEO: Hatma ya kesi ya Wema, hukumu Ijumaa

Muktasari:

  • Wema na mwenzake wanakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya katika Mahakama hiyo, na kwamba walitakiwa kusomewa hukumu hiyo leo, lakini  imesogenzwa mbele hadi Julai 20, mwaka huu kutokana na Hakimu anayesikiliza shauri hilo kuwa bado hajakamilisha kuandika Hukumu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Ijumaa ya wiki hii kutoa hukumu dhidi ya Miss Tanzania mwaka 2006, Sepetu na wafanyakazi wake wawili.
Wema na mwenzake wanakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya katika Mahakama hiyo, na kwamba walitakiwa kusomewa hukumu hiyo leo, lakini  imesogenzwa mbele hadi Julai 20, mwaka huu kutokana na Hakimu anayesikiliza shauri hilo kuwa bado hajakamilisha kuandika Hukumu.
Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati kesi hiyo lilipokuja kwa ajili ya hukumu.
"Naomba mniwie radhi, kuna vitu vichache bado sijaviweka katika hukumu yangu, hivyo naomba kuiahirisha hadi Julai 20, ili niweze kuvikamilisha" alisema Hakimu Simba.
Hakimu Simba, alisema licha ya kuandaa hukumu, bado kuna vitu anavipitia ili kujiridhisha na kesi hiyo kabla ya kutoa hukumu.
Awali, Wakili wa Serikali, Costantine Kakula alidai mahakamani hapo kesi hiyo imekuja kwa ajili ya hukumu na wao wako tayari kusikiliza hukumu.
Hukumu hiyo, inatarajia kutolewa Julai 20, mwaka huu, baada ya mawakili wa upande wa utetezi, Albert Msando na wa upande wa mashtaka Costantine Kakula kuwasilisha hoja za majumuisho katika kesi hiyo za kushawishi mahakama iwaone wa shtakiwa hao wana hatia ama hawana hatia.
Tayari mashahidi watano wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao  ambapo mahakama iliwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na hivyo kuwaamuru kujitetea.
Hata hivyo, tayari Wema na wafanyakazi wake, Angelina Msigwa (23) na Matrida Abas (19) nao wameshajitete na kufunga ushahidi wao.
Katika utetezi wake mahakamani hapo, Wema, alikubali kuwa nyumbani kwake palikutwa na msokoto unaodhaniwa kuwa ni bangi jikoni, vipisi ambavyo hajui nini katika chumba cha kuhifadhia nguo zake mapochi na viatu na kiberiti katika chumba wanacholala wanamuziki wawili Jodarn na Mila .
Akiongozwa na wakili Msando kujitetea, Wema alieleza kuwa yeye hajui vitu hivyo ni vyanani  kwa sababu yeye ni msanii wa filamu na nyumbani kwake wanaingia watu tofauti tofauti pia huwa anafanya pati na kualika watu katika nyama choma na chakula cha mchana.
Hivyo hawezi kujua vitu hivyo ni vya nani na kwamba watu wengine huwa wanaingia jikoni kwake na maeneo mengine isipokuwa katika chumba chake cha kulala kwa kuwa huwa anafunga.
Wema alidai kuwa polisi walikagua katika chumba chake cha kulala lakini hawakupata kitu.
Alibainisha kuwa nyumbani kwake walikuwa wanaishi yeye, wafanyakazi wake wawili, wadogo zake wawili,  Agray Philemon na Fanuel Evalast na vijana wawilï wanamuziki Milaji na Jordan.
Alidai kuwa Februari 3, 2017 aliitwa polisi wakaripoti polisi kati saa tano asubuhi kwa idhinï ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
"Siku hiyo tulifika polisi saa tano asubuhi na wenzangu watano tukasubiri hadi saa 10 jioni, ulipofika muda huo alifika Makonda na kutuita mmoja mmoja katika chumba ambapo alikuwepo na Afande Siro" Alieleza Wema.
Alidai kuwa wakiwa humo aliulizwa kama anatumia dawa ya kulevya ama kuuza  na kwamba aliwajibu hapana.
Aliendelea kudai kuwa baada ya mahojiano hayo walpelekwa mahabusu ambapo walikaa kwa siku saba na kwamba kati ya siku hizo, Februari 5, 2017 Jumapili polisi, akiwamo afande Mery,OCCID Denis, Hassani walimpeleka kwake kufanya upekuzi.
Wema alibainisha kuwa wakiwa njiani hawakuongea chochote na afande Mery safari yote walikuwa kimya tu.
Wema aliongeza kuwa yeye alitoa sampuli ya mkojo polisi na kwamba alimkabidhi afande Mery na kwamba yeye hana lolote la kueleza mahakama.
Akihojiwa na wakili wa serikali, Costantine Kakula, kuwa nitakuwa sahihi nikisema hivyo vitu vilikutwa nyumbani kwako.
Wema alijibu kuwa inasemekana.
Wakili Kakula alimuuliza Wema ulishuhudia jinsi hivyo vitu vikipatikana.
Wema alijibu kuwa ndiyo nilikuwepo.
Wakili Kakula aliuliza  hao watu unaoishi nao ulikwishawahi kuwaona wanavuta bangi.
Wema alijibu kuwa hapana sijawahi kuwaona wanavuta bangi.
Kwa upande wa wafanyakazi wa Wema, Angelina na Matrida wao walieleza kuwa wakati askari walipoenda kufanya upekuzi kwa Wema wao walikuwa wamekaa nje.
Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa  na Matrida Seleman Abbas.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.
Inadaiwa kuwa Februari 4, 2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio  washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februari Mosi, 2017 katika  eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya Bangi.