VIDEO: Wasanii wa Bongo Muvi wazikimbia fursa ZIFF

Tamasha la ZIFF linaloendelea katika viwanja vya Ngome  kongwe limekosa ushiriki kamili wa wasanii wa filamu za Kibongo, ambao kelele zao kubwa ni kukuza soko hilo.

Wasanii wa filamu hadi sasa, ambao wameonekana  katika viunga vya maeneo ya sinema ni Mzee Chilo, Gabo, Natasha na Claud.

Kutokuwepo kwa  wasanii wengi wa filamu  na hata balozi wao ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Saimon Mwakifamba, kunaleta hisia tofauti kwa wadau wa filamu ambao wamekuwa wakishauri Watanzania kulitumia tamasha la ZIFF kujifunza na kutanua mtandao wao badala ya kusubiri kualikwa.

“Wapo watengeneza filamu wengi wanakuja bila kualikwa,lengo lao ni kukuza mtandao wa mawasiliano na kuona fursa za soko” anasema Meneja wa Tamasha Daniel Nyalusi baada ya MCL Digital kumuuliza swali.

Alisema tamasha ni la kila mmoja lakini wapo watu wanatoka Haiti wanakuja kwa fedha zao na kuja kuona fursa ya soko na kusikia wengine wanafanyaje kazi zao.

Wasanii na watengeneza sinema wa Kenya, wamejitokeza kwa wingi na kazi zao wakitumia ZIFF kama sehemu ya kujitangaza.

Akizungumzia kuhusiana na wasanii wa filamu za kibongo  kutokuwepo kwa wingi  katika uzinduzi wa tamasha la Ziff lililozinduliwa julai 7,2018  Mkurugenzi wa ZIFF, Frabrizio Colombo amesema

“Tatizo kubwa hapa ni kwa wasanii wetu wengi wao wanasubiri sisi waandaaji tuwaombe waje kushiriki katika tamasha hili baada ya wao waje kuomba ama kuja kujifunza binafsi katika tamasha hili,’’ alisema.

“Nawalaumu kwa kuwa hawalichukulii tamasha hili kwa uzito,” alisema Frabrizio Colombo na kuongeza kuwa kama wangekuwepo labda wangeweza kupata elimu na kubadilishana mawazo na magwiji mbalimbali waliofika.

Hata hivyo Frabrizio  amesema wasanii wa filamu za kibongo  wanatakiwa kufika leo kwa ajili ni siku yao ya kuonyeshwa filamu za Kibongo na pia kesho kutwa ni  siku ya Swahili Day kuonyeshwa.

Kuna sinema kadhaa zilizoingia katika ushindani wa tamasha ingawa ipo siku kamili ya kuonesha sinema za Kiswahili na ushindani katika awamu hiyo hiyo.

Hata hivyo kwa upande wa msanii mkongwe wa filamu Cloud, amesema  Issa Musa 'Cloud' ameiambia MCL digital kuwa Wasanii wengi hawajajitokeza wa kibongo hawajajitokeza katika tamasha la ZIFF, sababu baadhi yao wapo Dar es Salaam na ushiriki wao katika Tamasha la ZIFF kwa mwaka huu ni tofauti.

Changamoto kubwa ni kwamba wasanii wengi hawajaelewa fursa zinazopatikana katika Tamasha la ZIFF.

Amesema wasanii wengi wanachukulia kwamba ili kushiriki Tamasha la ZIFF ni lazima upate tuzo, hilo si lengo. Lengo la kuja ZIFF ni kuja kujifunza kwavile Kuna wageni wengi kutoka nchi tofauti duniani wanahudhuria Tamasha hili.