Patrick azikwa akiacha somo kubwa kwa wazazi

Muktasari:

  • Msiba wa mtoto Patrick umekuwa na msisimko mkubwa kutokana na kufuatiliwa na maelfu ya watu. Sio tu kwa sababu ya sintofahamu kutoka kwa wazazi wake na malumbano yanayoendelea huko mitandaoni.

MENGI yamezungumzwa kiasi cha watu kuingiwa hofu kuhusu ni vipi itakuwa safari ya mwisho ya kumsindikiza mtoto, Patrick Peter Zakaria.

Msiba wa mtoto Patrick umekuwa na msisimko mkubwa kutokana na kufuatiliwa na maelfu ya watu. Sio tu kwa sababu ya sintofahamu kutoka kwa wazazi wake na malumbano yanayoendelea huko mitandaoni.

Yeye mwenyewe akiwa na miaka saba tu, tayari alikuwa ni staa mkubwa hapa Bongo.

Huko kwenye mitandao ya kijamii na hasa Instagram, hakuna asiyemjua mtoto Patrick. Nyota yake ilishaanza kung’aa mapema tu.

Hata hivyo, hatimaye safari wa mwisho ya Patrick katika nyumba yake ya milele ikahitimishwa jana pale kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambako mazishi yake yalifanyika.

Huzuni na vilio vilitanda kila kona wakati jeneza lenye mwili wake likishushwa kaburi kuashiria mwisho wa enzi za Patrick hapa duniani. Patrick alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu jijini Nairobi, Kenya na mwili wake uliwasili nchini juzi Ijumaa kisha kwenda kuhifadhiwa katika Hospital ya Aga Khan.

Hapa Mwanaspoti linakuletea hatua kwa hatua kwenye shughuli nzima na mambo yaliyojiri nyuma ya pazia.

Si unajua awali kulizuka utata mkubwa kuhusu nani baba halali wa Patrick kati ya mtangazaji wa Cloud Tv, Casto Dickson na Peter Zakaria, ambaye aliibuka na kueleza ndiye baba halisi wa Patrick.

Pia, alitoa vilelezo kibao vikionyesha alifunga ndoa na mama wa Patrick, Muna Love, ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika baba wa mtoto ni Casto na sio Peter.

MUNA AUMWA GHAFLA

Mwili wa Patrick uliwasili nyumbani kwa baba yake Peter, Mwananyamala saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya taratibu za kuagwa. Ndugu na jamaa wa Peter walihakikisha kila kitu kinakwenda sawa na shughuli ya kuaga ikafanyika kwa amani.

Hata hivyo, Muna ambaye awali alipinga msiba wa mwanaye kuwekwa nyumbani kwa Peter, hakuonekana kwenye tukio hilo.

Baadaye ikaelezwa aliugua ghafla wakati akiwa kwenye harakati za kuandaa mwili huo. Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu kupumzishwa kwenye Hospitali ya Agha Khan kwa muda.

Mbali na Muna hata mastaa wa Bongo Movie akiwemo Steve Nyerere ambaye awali alionekana kuwa mstari wa mbele kwenye msiba huo, hawakuonekana kwenye tukio hilo la kuagwa kwa Patrick nyumbani kwa baba yake.

HALI ILIVYOKUWA LEADERS

Baada ya shughuli ya kuagwa kumalizika nyumbani kwa Peter, ikawa zamu wa viwanja vya Leaders ambako, Muna aliibuka na kuungana na ndugu na jamaa katika kumuaga mtoto wake.

Mastaa wa Bongo Movie ambao waliingia mitini kushiriki tukio hilo nyumbani kwa Peter, walijitokeza kwa wingi viwanjani hapo. Steve aliwaongoza wasanii wenzake akiwemo Wema Sepetu, Mayasa, Anti Ezekiel, Shilole a.k.a Shishi Baby, Yusuf Mlela, Dude, Hemed PhD, Thea, Batuli na Cath ambao walishiriki kikamilifu kumuaga Patrick.

Gari iliyobeba mwili wa Patrick iliingia kwenye viwanja hivyo saa 12:15 na kusababisha vilio na kwikwi kila kona ya uwanja huo.

Hata hivyo, uwanjani hapo mambo yalionekana kutulia na Muna na Peter walionekana kuweka tofauti pembeni na kuungana pamoja kushiriki tukio hilo kwa kuketi pamoja kwenye meza kuu na kumaliza kabisa ile sintofahamu ya awali kwa muda.

PETER AFUNGUKA TENA

Katika ibada ya kuaga mwili huo, Peter alizungumza na waombolezaji na alirejea tena kusisitiza Patrick ni mtoto wake halali. Pia, alisema Muna bado ni mke wake halali, kauli ambayo iliwafanya waombolezaji kupiga shangwe za furaha.

“Nimepata nguvu ya kuzungumza na naomba niweke wazi tena hii ni familia yangu na nilimtolea mahari mke wangu Muna, lakini kuna watu wanampoteza kwa kumdanganya.

“Niwaeleze ukweli, sipendi kabisa kuingiliwa kwenye masuala ya familia yangu. Hata kama Patrick akifungua macho sasa ataeleza ukweli na siku zote alikuwa akiniita baba na alikuwa akinifanyia maombi,” alisema Peter kauli ambayo ilionekana kuwachoma waombolezaji.

MSIKIE NABII TRIZA

Kama unadhani shughuli ya kumuaga Patrick ilikuwa ya kawaida basi utakuwa umepitwa kwani, mama wa kiroho wa kijana huyo Nabii Trisa, alitua moja kwa moja akitokea Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki tukio hilo.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Nabii Triza alisema Patrick alikuwa kijana mnyenyekevu na aliyemfahamu na kujitoa kwa Mwenyezi Mungu.

“Patrick alikuwa analijua neno kuliko hata wazazi wake, ni kijana aliyejitoa sana katika kumwomba Mungu, lakini hakuna mtu ambaye mwenye uchungu kama baba yake au mama yake,” alisema.

Wakati akiendelea kuhubiri neno, Nabii Triza aliwataka wazazi wa Patrick, Muna na Peter kusahau yaliyopita na kuanza ukurasa mpya wa maisha. Pia, aliwataka kuacha kusikiliza maneno ya kwenye mitandao ya kijamii.

“Nimeangalia kwenye mitandao na kuona watu wanajaribu kuleta mtafaruku ndani ya familia, mimi ni mama wa kiroho wa Patrick ndiyo maana nimesimama hapa na kuhubiri upendo. Nawaomba muanze ukurasa mpya na msisikilize lolote nje ya haya ninayosema,” alisema.

RAFIKI ALIZA WATU

Patrick kama ilivyo kwa watoto wengine, ana marafiki zake na mmoja wapo ni Abraham, ambaye alisimama kumuaga mwenzake lakini, kauli aliyoitoa iliongeza simanzi na huzuni kwa waombolezaji.

Abraham aliandika shairi fupi akielezea jinsi walivyoishi na Patrick na alisema walikuwa kama vipepeo wakicheza pamoja lakini mmoja ameondoka na kukatisha furaha hiyo.

“Tulikuwa kama vipepeo, tulicheza na kufurahi pamoja lakini leo umeondoka na kuniacha peke yangu, naamini upo sehemu salama,” alisema Abraham ambaye naye alikuwa na maonekano wa kitanashati kama alivyo Patrick.

KEYSHA, MASANJA WAFUNGUKA

Unambuka staa wa kike wa Kundi la Tip Top Connection, Khadija Shaban (Keysha), ambaye kwa sasa ni mwanasiasa, naye aliungana na waombolezaji kwenye msiba huo.

Keysha alisema kuondoka kwa Patrick ni mipango ya Mungu kuwakumbusha wanadamu anamchukua mtu yeyote na muda wowote.

“Mimi ni shabiki wa Patrick, nimekuja kumsindikiza kijana huyu lakini wazazi muwe na amani na upendo na hata mtoto huko alipo anawaombea muwe na amani,” alisema Keysha.

Kwa upande wake, Masanja Mkandamizaji aliwataka watu kujifunza kupitia msiba huo kwani, kila mmoja anatakiwa kujindaa kwani, hakuna anayejua siku yake.

“Tunaweza kuokoka na bado tukapitia magumu na biblia inasema Mungu pekee ndiye aliyepewa mamlaka ya kumhukumu binadamu. Tumieni nafasi hii Muna na Peter kujenga palipobomoka,” alisema.

Naye malkia wa Bongo Movie, Wema Sepetu ambaye alikuwa rafiki wa karibu na Muna, alikiri anajua rafiki yake anapitia wakati mgumu kwa sasa kwa kumpoteza mtoto wake.

“Kama nisingemjua Muna nisingemjua Patrick, najua uchungu aliokuwa nao rafiki yangu licha ya kuwa sijabahatika kupata mtoto, lakini maumivu nayajua,” alisema.