Dalili 5 mumeo anatoka na shoga yako

Sunday June 24 2018

 

By Kalunde Jamal

NAWAKARIBISHA tena mashabiki na mashoga zangu kwenye Kijiwe cha Anti K, ambapo kama kawaida tunapasha mambo yetu yaleee. Ndio! Hayo hayo kwani ulidhani hapa tunazungumzia Kombe la Dunia kule Russia, hapa ni mapenzi tu kwani, maisha bila malovee kamwe hayaendi shoga.

Sasa wiki hii hebu tuzungumzie kidogo hawa mashoga zetu. Si unajua adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe? Sasa kuna mashoga zetu hawa ni mabingwa wa kudanga, lakini wanavuka viwango sasa wanadanga hadi kwa shemeji zao.

Kwa kuwa haya mambo yameshika kasi sana, nimeona niwape mchongo kidogo tu wa jinsi ya kutambua kama shoga yako kaingia anga za mumewe. Jamani hawa mashostito wadangaji wanatupa stress hatari halafu wengine unakuta ni mafundi kwelikweli hapo ndio balaa lenyewe.

Mawasiliano hayakatiki

Kuna vitu vinaonekana vya kawaida sana kwa marafiki walioshibana, lakini shogaangu kwenye mapenzi usiruhusu sana hilo. Kamwe usiruhusu mpenzi wako kuzoeana na rafiki yako kiasi cha kupigiana simu, kuchati na wakati mwingine kukutana kabisa. Yaani kuna mashoga wanajua kudanga bana, kabla bwana hajaamka kashatuma sms: Shem umeamkaje, siku njema ubarikiwe sana.

Aaah! Shoga hapa itakula kwako mapemaa, ni lazima haya mambo uyafanye mwenyewe na ukiacha hili likaota mizizi basi bwana huna.

Anamponda Sana

Kuna wanaume wanajua mipango bana asikwambie mtu, yaani akishamdanga tu rafiki yako anaanza kwa kumponda ili kukuzuga kwamba, hata hisia naye hana kabisa.

Kila wakati anamzungumzia vibaya na wakati mwingine kukupiga marufuku kufuatana naye.

Hatua hiyo itakufanya upumbazike akili na hisia hivyo, kuanza kujiweka mbali na shoga yako ili kumridhisha bwana, kumbe hapo ndio anapata nafasi ya kula bata.

Wanakutana bila kukutaarifu

Hivi utajisikiaje kama ukiwa kwenye mizunguko yako mjini kisha ukaingia sehemu kupata angalau soda ili ukate kiu kisha, ukamkuta mzee ametulizana na shoga yako wanapata kinywaji? Tukio hilo limetokea huku si mpenzi wako wala shostito wako aliyekupigia ama kutuma hata sms kukwambia kuwa, wamekutana kwa bahati mbaya sehemu fulani hivyo wako hapo! Hapa ni lazima taa ya hatari iwake ma utaumizwa shoga.

Namba yake kichwani

Akipigiwa simu na rafiki yako anaijua namba yake, lakini hajisevu kwenye simu. Kwa kawaida wanaume ni ngumu kushika namba za simu kichwani ukilinganisha na wanawake, lakini mumeo au mpenzi wako anaijua ya rafiki yako akiiona inaita anakwambia fulani anapiga.

Urafiki unapungua

Ukiona shoga yako anapunguza urafiki kwako na badala yake anauhamishia kwa shemeji yake kuwa makini. Wewe ndiyo umewakutanisha iweje ampende mtu ambaye hana mahusiano naye wala alikuwa hamfahamu hapo kabla.

Wengine huvuka mipaka na kujifanya anamjua sana hata katika mazungumzo ya kawaida.

“Shemeji hapendi kabisa kula pweza, hata kuogelea sio hobi yake. Ngoja nikamchagulie nyama anayopenda kula ninaijua”.

Kwa leo sina la zaidi shoga, lakini ngoja nikuache na take away kidogo kwamba, usipende kusimulia mambo yako na mpenzi wako kwani, wengine wakisikia mambo flani ndio ugonjwa wao.