Yaliyomkuta King Majuto asimulia kila kitu

TANGU saa 7 mchana juzi Ijumaa, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na maeneo ya jirani yalijazana mashabiki wake.

Hali hii ilizoelekea pale zinaposafiri ama kuwasili kwa klabu za Ligi Kuu ama ujio wa makocha au nyota wa kigeni kutoka nje ya nchi.

Kila mtu aliyekuwa eneo hilo alikuwa bize kuchungulia ili kujua kile alichokifuata uwanjani hapo na kweli bwana, majira ya saa 9 alasiri kila mmoja alituliza mtima wake.

Unajua nini? Wengi wao walifika uwanjani hapo ili kumpokea gwiji wa filamu na vichekesho nchini, King Majuto aliyekuwa akirejea kutoka India kwenye matibabu.

Siku moja, yaani Alhamisi walikatwa stimu baada ya kufika uwanjani hapo na kushindwa kumuona mkongwe huyo ambaye majina yake kamili ni Amri Athuman maarufu kama Mzee Majuto, baada ya safari yake kuahirishwa hadi hiyo Ijumaa.

Hata hivyo, bahati mbaya ni kwamba walishindwa kumuona Majuto anayetembea mwenyewe na pengine kupata nafasi ya kumpokea na kupiga naye picha za ukumbusho.

Majuto hakuwa katika hali nzuri na watu waliopokea waliharakisha kumuingiza kwenye gari la wagonjwa kabla ya kumkimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu na uangalizi baada ya kufanyiwa upasuaji nchini India.

TATIZO NINI?

Kama ambavyo Mwanaspoti liliwahi kufanya mahojiano naye miezi michache iliyopita, King Majuto alikuwa anasumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa Tezi Dume.

Licha ya kupatiwa huduma mara kwa mara hapa nchini, hali yake ilikuwa inashindwa kutengemaa na kuamriwa akapate matibabu ya kina nchini India na Mei 4 mwaka huu alisafirishwa kwenda Hospitali ya Apollo iliyopo jiji la New Delhi.

Majuto alisafishwa kwa msaada wa Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa miezi mitatu ya mateso ya maumivu makali kama alivyowahi kunukuliwa mwenyewe kwenye mahojiano ya mwisho na Mwanaspoti alipokuwa kalazwa Muhimbili.

ANGALAU SASA

Mzee Majuto mara alipowasili jijini Dar es Salaam alizungumza machache na wanahabari na kukiri kwamba kwa sasa angalau hali yake inampa matumaini kwani hajambo tofauti na alivyoondoka kwenda huko India.

Anasema kupelekwa kwake Muhimbili sio kama amezidiwa, bali ni kutaka kupumzishwa kutokana na uchovu wa safari na pia kuangaliwa vyema kabla ya kuruhusiwa kwenda kujiangalizia nyumbani.

Licha ya kusisitiza kuwa anaendelea vizuri, lakini hali yake ni wazi bado haijakaa njema kwani mara alipotua uwanjani alishindwa kutembea mwenyewe na kupewa kiti cha kutembelea na kupakizwa katika gari la wagonjwa la Muhimbili.

Majuto hakusita kumshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha safari na matibabu yake India, pia akiwashukuru Watanzania kwa ujumla na hasa mashabiki wake kwa jinsi walivyomuombea na kumfanikishia kumrejesha salama akiwa mzima wa afya.

Anasema anashukuru pia amepata huduma na matibabu mazuri kutoka kwa madaktari bingwa wa India na kukiri kama asingefanyiwa matibabu hayo basi angekuwa katika hali mbaya na huenda tungemkosa kama utani.

“Nawashukuru madaktari wa India kwa kunitibia vizuri, nimefanyiwa mambo mengi ambayo kama nisingefanyiwa hivyo basi huenda mngenikosa maana nilikuwa na hali mbaya sana,” anasema na kuongeza;

“Namshukuru Rais Magufuli kwa kuwezesha safari na matibabu yangu ya India, pia nawashukuru wote walioniombea nipone kwani Mungu amesikia dua zao njema, angalau sasa najisikia kuzaliwa upya,” alisema Majuto.

UAMUZI MGUMU

Hata hivyo katikati ya shukrani ya kupata kwake nafuu, Majuto akafichua jinsi alivyoamua kiume, japo anakiri mashabiki wake hawatafurahia.

Majuto anasema kuwa, Mungu akimjalia na kupona bado anafikiria kuachana kabisa na uigizaji ili apate muda mrefu wa kupumzika.

“Nawashukuru Watanzania wote kwa maombi yao, nawapenda sana ila naomba wazidi kuniombe ili nipone haraka na jambo langu la kuwaaambia ni kwamba nikipona nitaacha kuigiza,” anasema Majuto.

Majuto anasema anajua mashabiki wake watashtushwa na habari hizo za kuacha kwake kuigiza ila kutokana na kuugua kwa muda mrefu ameona hana jinsi zaidi ya kupumzika.

“Najua mashabiki wangu watashtushwa na habari hizi, ila sina namna waniache nipumzike kwani nimeitumikia sanaa hii kwa muda mrefu na ninapenda kuendelea, lakini kwa mateso niliyopata ya maradhi, acha nipumzike kwanza.”