Dimpoz, siri nzima ya kuugua na matibabu yake Bondeni

KATIKA nyumba za ghorofa za Weom, eneo la Morning Side, Barabara la Shannon Ln kwenye Kitongoji cha mji wa kifahari wa Sand ton jijini Johannesburg, Afrika Kusini nakutana na msanii maarufu wa Bongo Flava, Omary Nyembo au Ommy Dimpoz.

Dimpoz hayupo vilevile kama unavyojaribu kutengeneza picha. Anaumwa. Hauhitaji akwambie kama anaumwa. Hapana. Anaumwa. Unamuona tu kwamba anaumwa. Sio Dimpoz yule ambaye unamfahamu. Mchangamfu na mwenye mambo mengi ya utani.

Wakati ukiendelea kuburudika na wimbo wake wa Yanje ambao, unatamba Tanzania na Afrika Mashariki na kati kwa jumla, fahamu kwamba mpaka sasa hali ya staa huyu aliyewahi kutamba na nyimbo za Nai Nai, Baadaye, sio nzuri.

Najua unamfahamu Dimpoz wa jukwaani, wa katika video, lakini zaidi wa mitandaoni, hasa Instagram. Dimpoz mwenye mbwembwe nyingi na picha zake za kitanashati. Huyu niliyekutana naye Sandton, Johannesburg alikuwa anachechemea akiwa ameinamisha kichwa chake chini.

Sauti yake inatoka kwa shida na wakati mwingine unalazimika kusubiri apumzike kidogo ili aendelee na mazungumzo naye. Wakati mwingine anatamani kucheka au kupumua kwa nguvu, lakini inashindikana. Anakumbana na maumivu makali.

Amevaa jaketi linaloziba kichwa chake kwa sababu mbili. Kwanza ni kwa sababu amekonda sana. Lakini, pili ni kwa sababu anaziba kidonda kirefu katika eneo la shingo ambacho kilitokana na operesheni kubwa iliyomlaza hospitalini akiwa ICU kwa siku tisa.

Nini Kilimsibu? Mara ya mwisho Dimpoz alionekana katika harusi ya Ali Kiba akiwa katika afya njema kabisa.

Hata hivyo, ndani yake kulikuwa na kitu kilichokuwa kinamsumbua kwa muda mrefu. Hakuna aliyefahamu sana zaidi ya rafiki yake Ali Kiba.

“Unajua brother Edo kwa muda mrefu nilikuwa nikila chakula sometimes kuna kitu kinakuja kinakwama hakiendi. Najaribu kutumia nguvu sana kumeza, lakini inashindikana. Mara tatu nimekwenda Muhimbili eti kisa nimekwamwa na kinyama kidogo tu wakati nakula,” anaanza kusimulia Dimpoz.

“Katika harusi ya Kiba pale Dar es Salaam ilinitokea asubuhi wakati nimeandaliwa chai. Tulikuwa mimi, Kiba na Gavana Joho (Hassan Joho, Gavana wa Jiji la Mombasa ambaye ni rafiki mkubwa wa Dimpoz na Kiba).

“Wakati nakunywa chai nikawa napata wakati mgumu sana. Gavana Joho akashtuka. Akauliza ni kitu gani kinanitokea. Kiba akamwambia ni tatizo fulani kubwa na linanitesa.”

“Gavana akasema kama ni hivyo basi kuna umuhimu niende Mombasa kwa madaktari anaowafahamu ambao, ni wataalamu sana wa masuala ya mwili wa binadamu. Ndani ya siku chache nikaenda Mombasa. Pale ndipo tatizo kubwa lilipoonekana.”

Wakati Dimpoz akiamini kwamba tatizo lake lilikuwa limefika mwisho katika mikono ya wataalamu zaidi pengine kuliko nyumbani alikotokea, hali haikuwa hivyo kabisa.

“Baada ya uchunguzi madaktari waligundua kwamba, tatizo langu ni kubwa na nilipaswa kwenda Afrika Kusini kwa wataalamu zaidi. Iligundulilka kuwa ndani ya koo langu mishipa imetanuka kiasi kwamba, haiwezi kupitisha kitu chochote kwa urahisi.”

“Hicho ndio kilikuwa chanzo cha kuja hapa Afrika Kusini. Nilikuja hapa nikionekana kama nina afya njema brother, lakini badaye kilichonitokea nilichungulia kifo. Namshukuru sana Mungu aisee.

“Nilipitia vipimo mbalimbali kabla ya operesheni, lakini madaktari walinishtua zaidi baada ya kuniambia kwamba operesheni yangu ilikuwa ngumu na nusu ilikuwa uhai huku nusu nyingine ikiwa ni kifo,” anasimulia Dimpoz.

Kwanini ilikuwa ngumu? Namuuliza Dimpoz ambaye amekuwa Afrika Kusini kwa mwezi mzima sasa na hajawahi kutoka nje zaidi ya kushinda ndani kutazama runinga na kunywa lundo la dawa alizoweka mezani karibu na kochi analokaa.

“Kilichotakikiwa katika operesheni ile madaktari waliniambia kwamba, kulikuwa na njia mbili za kunifanya nirudi katika hali ya kawaida. Kwanza ni kurekebisha mishipa ileile ya koo, lakini wakanionya kwamba baadaye hali ile ingeweza kujirudia.”

“Pili, wakaniambia njia nyingine ilikuwa ni kuhamisha njia ambayo ninaitumia katika kupitisha chakula. Hii ilionekana kuwa salama zaidi. Hata hivyo, ilikuwa operesheni ndefu sana. Awali, madaktari waliniambia ingechukua saa saba, lakini ikaja kuchukua saa 10.”

Dimpoz ananionyesha kidonda kikubwa kilichotokana na kuchanwa kwa tumbo lake kuanzia chini ya kifua hadi chini ya kitovu. Usitegemee kumuona Dimpoz aliye tumbo wazi kwa miaka mingi ijayo.

“Licha ya kunichana shingoni, lakini pia waliniachana sehemu kubwa ya tumbo kwa ajili ya kurekebisha. Kilichokuwa kinatakiwa kwanza ni kuhakikisha inapatikana njia ya muda ya kupitisha chakula wakati njia halisi inaondolewa. Lakini pia kuhakikisha njia mpya ya chakula inafanya kazi vema.”

Operesheni hii ilifanikiwa. Hata hivyo, kitu cha hatari zaidi ambacho kilimtokea Dimpoz ni kwamba alilazimika kukaa ICU (Chumba cha uangalizi maalumu) akiwa hajitambui kwa siku zaidi ya saba. Hakujua yupo ulimwengu gani. Anaamini kwamba ni Mungu ndio amemuokoa.

“Sikujitambua kwa zaidi ya siku saba. Nilikuwa nimewekewa nyaya katika kila kiungo changu. Nilikuwa napumulia mashine kusaidia mapafu yangu. Kila kitu kilitibuka na nilikuwa katika hali ya hatari,” anasimulia Dimpoz kwa sauti ya chini.

“Nilipozinduka sikujua nilikuwa wapi. Kwa jinsi ambavyo nilikuwa dhaifu sana, nilihisi kifo aisee. Jinsi ambavyo madaktari walivyonishughulikia nilikuwa naona kabisa , maisha yangu yapo hatarini sana,” anasema Dimpoz.

Matibabu yaKE NI KUFURU

“Bado anasikia maumivu makali katika mgongo wake kiasi kwamba anatembea kwa shida sana. Pia, anashindwa kugeuza shingo yake vizuri kutokana na mshono mkubwa uliopo katika shingo yake.

“Kwa sasa katika shingo yangu nahisi kama vile nimepigwa kabali. Siwezi kugeuka kwa haraka. Nasikia maumivu pia mgongoni. Nanyanyuka taratibu sana na siwezi kutembea katika hatua za haraka kama zamani,” anasema Dimpoz.

Operesheni ya Dimpoz ilikuwa kubwa. Ilifanywa chini ya wataalamu wakubwa wakiongozwa na daktari wa kike, Selvie kutoka nchi ya Romania ambaye kwa mujibu wa Dimpoz walimsaka kwa kutumia mtandao wa Internet kujua ni daktari bingwa wa maradhi gani.

“Wakati tupo Mombasa tulianza kumsaka kupitia mitandao daktari, ambaye atakuwa Afrika Kusini na atakuwa ni bingwa wa maradhi haya. Hapo ndipo tulipompata daktari huyu. Ameokoa maisha yangu kwa sababu ilikuwa ni operesheni ngumu lakini alikuwa anajua anachokifanya,” anasema Dimpoz.

Shukrani kwa Gavana Joho na timu yake ya menejimenti ya Rock Star inayoongozwa na Christina Moshi maarufu kama Seven, ambaye pia anamsimamia Ali Kiba. Dimpoz anataja dau kubwa ambalo limetumika kufanikiwa operesheni na makazi yake Johannesburg katika apartments za kifahari za Woems zilizopo Sandton. Inashangaza kwelikweli.

“Brother kila ukipiga hesabu ya pesa iliyotumika nadhani inafika dola za Marekani 60,000 (Sh.132 milioni). Kujuana na watu inasaidia sana brother. Hii operesheni imegharimu kiasi kikubwa cha pesa. Kitu cha muhimu ni afya tu,” anasema Dimpoz. Wakati tukiendelea na mazungumzo inaingia meseji katika simu yake kutoka kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye anaonyeshwa kushtushwa na afya ya Dimpoz baada ya kupata habari kutoka kwa watu wa karibu.

“Mimi napenda sana simu. Nina addiction na simu, lakini hauwezi kuamini nimeanza kushika jana tu. Kwa zaidi ya siku kumi nilikuwa sijashika simu yangu, kuumwa kubaya sana asikwambie mtu. Kuna siku baada ya kuzinduka nilizitazama sura za madktari nikaona kama vile wamekata tamaa na hali yangu.”

Licha ya ubishoo wa kutofuatilia mambo muhimu ndani ya nchi yake, lakini Dimpoz anakiri kwamba kwa sasa atakuwa anapiga kelele kuhakikisha Serikali inawezekeza zaidi katika masuala ya afya nchini Tanzania.

“Sasa hivi ndio nimejua umuhimu wa sekta ya afya. Serikali ina kazi kubwa ya kufanya aisee. Hawa jamaa wametuacha mbali sana. Nadhani kuna watu wengi wanakufa nchini kwetu kwa kukosa aina ya matibabu ambayo nimepewa hapa Afrika Kusini. Lakini pia kuna umuhimu wa watu kuwa na bima ya afya.

“Hospitali ambayo nililazwa ni ya kiwango cha juu. Walinivalisha nyaya nyingi katika kila kiungo cha mwili. Kama nikitikisika tu nikagusa kitu basi kuna kitu kinalia daktari au muuguzi ananikimbilia. Sasa mimi Mungu amenijalia kutibiwa hapo vipi huko vijijini inakuwaje brother? Unadhani kuna vifaa hivyo? Panadol tu shida.”

Nini kinafuata baada ya hapa? Dimpoz amepewa ofa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ambaye ni rafiki yake wa karibu kuwa atampatia mtu wa kumtazama kwa karibu zaidi akiwa Dar es salaam. Mtu ambaye ni bingwa wa masuala ya misuli. Kwa sasa damu yake haitembei vema kutokana na mwili wake kushtuka kwa kuwa, hakuzoea sana kulala kitandani kwa muda mrefu.

“Pamoja na ofa ya Makonda lakini nimefikiria kurudi kwanza Mombasa na kujiweka sawa kwa sababu kule hakutakuwa na bugudha kama Dar es salam. Baada ya hapo nikiwa fiti natarajia kutoa nyimbo tena. Unajua nilipania mwaka huu nitoe ngoma nyingi na kurudia kwa kasi baada ya Yanje kwenda vizuri. Tayari kuna nyimbo nimerekodi bado video tu. Tatizo ni hii operesheni lakini Mungu ndio ambaye anajua kila kitu,” anasema.

Katika kochi alilokaa, Dimpoz anatazamana na televisheni kubwa mbele yake. Kinachoendelea ni kutazama mechi za kombe la dunia tu zinazoendelea nchini Russia. Ni shabiki wa soka anayekera mitandaoni kwa ushabiki wake wa Manchester United.

“Timu za Afrika zinazingua sana ila naipa nafasi Brazil.”

Wakati tunafanya maongezi haya na Dimpoz ilikuwa siku ya Idd. Tunamaliza maongezi huku akiwatakia Idd njema mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla. Hasahau kujipiga kijembe kidogo.

“Sikuamini kwamba kuna siku ya Idd inafika wakati watu wanahangaika na mapilau wewe unahangaika na uji. Mungu mkubwa sana aisee.” Anamalizia kwa utani Dimpoz huku nikiagana naye.

Ananisindikiza kwa shida. Nafika mlangoni naondoka zangu kuelekea na maisha mengine mitaani.