KWA SAM WA UKWELI; Bora Wali-Tembele kuliko walimwengu

Sunday June 10 2018

 

By LUQMAN MALOTO

KAMA yalivyo maneno ya mwandishi galacha wa Uingereza, William Shakespeare, kuhusu kifo, ndivyo imekuwa ikithibitika miaka yote. Shakespeare aliishi muhula wa pili ya Karne ya 17 na kufariki dunia muongo wa pili, Karne ya 18. Shakespeare alipata kuandika: “Nothing can we call our own but death and that small model of the barren earth which serves as paste and cover to our bones.”

Tafsiri yangu: Hakuna tunachoweza kuita cha kwetu ila kifo na muundo wa kipande kidogo cha ardhi ambacho hutumika kama hifadhi na kufunika mifupa yetu. Kwa kifupi Shakespeare alimaanisha kuwa binadamu hana anachoweza kujivunia ni mali yake, isipokuwa kifo na kaburi. Muundo wa kipande kidogo cha ardhi ambacho hutumika kama hifadhi na kufunika mifupa ni kaburi.

Kusadiki maneno ya Shakespeare; mwanamuziki wa kizazi kipya, Salum Mohammed ‘Sam wa Ukweli’, hivi sasa ameshapokea yale ambayo ni mali yake. Ameshafariki dunia na tayari ameshazikwa. Hivi sasa yumo ndani ya kaburi. Kifo ni shule. Mafundisho yenye kupatikana kwenye Uislam, husemwa shule ni mawaidha. Ni tafsiri ileile kwamba kila binadamu anapofikwa na mauti, huacha elimu kubwa kwa waliobaki, ama kwa sehemu anayofahamika au kwa jamii kubwa kulingana na ukuu wake. Kipindi hiki Sam Wa Ukweli akiwa ameshafunga macho na kuipisha dunia, familia yake na jamii yote ya watu wake wa karibu wanayo mengi wamejifunza, vilevile jumuiya ya mashabiki wake na wapenda muziki kwa jumla.

Sam amelazwa kwenye kipande cha ardhi kinachofunika mifupa. Hiyo ndiyo mali yake ya pili baada ya kifo. Mengine yote ya dunia, aliyochuma au kuyapenda si mali yake. Asante Shakespeare kwa kutuachia hekima hii.

MANENO YANAVYOISHI

Sam ana nyimbo nzuri sana. Hizo si zake tena. Watabaki wakizifaidi walimwengu. Ndani ya kaburi hakuna wimbo aliozikwa nao, hana redio iliyoambatana naye. Hata angewekewa ‘music system’ kaburini, asingepata uwezo wa kuamka ili awashe na kusikiliza muziki wake mzuri. Sam kaacha mke na mtoto. Hao si wake tena. Ni mali ya walimwengu. Mungu akimkuza mwanaye, anaweza kuwafaa sana walimwengu, yeye hataona matunda. Duniani atasemwa tu aliacha mtoto mwema. Mke naye, Mungu akimwezesha ataolewa. Hata asipoolewa, yeye Sam hana matumizi naye tena. Hiyo ndiyo hali halisi; ukifanikiwa kumiliki nyumba, magari na mali nyingine zote, ukishakufa, watakaofaidika ni wengine. Watu wanaendelea kutumia simu, kompyuta, tablets za Apple, vilevile wakitembelea iTunes kusikiliza na kupakua nyimbo zake. Steve Jobs mwenye Apple yake alishalala. Apple si mali yake tena.

Kuna jamii kubwa inatengeneza fedha nyingi kupitia Apple, wakati Jobs hana habari tena. Akili zake nyingi hazina matumizi tena. Hata angezikwa na kampuni zake zote, Job asingezifanyia kitu. Je, hata baada ya mifano hiyo, bado unaweza kuthubutu kumpinga Shakespeare kuwa binadamu vitu pekee anavyoweza kuita vya kwake ni kifo na kaburi? Rejea mwaka 2010, Sam akiwa kijana mwenye matumaini makubwa ya kufanikiwa kimuziki, akaachia wimbo Sina Raha. Mpishi wa kazi hiyo ni mtayarishaji Kisaka Michael wa Emotion Records. Wimbo ukawa mkubwa na mpaka leo unaendelea kuishi.

Sam ameondoka duniani akiwa hajaweza kutoa kazi nyingine iliyofunika Sina Raha. Mwaka 2011, alitoa mzigo mwingine mkubwa, Hata Kwetu Wapo, lakini haukuweza kufua dafu kwa Sina Raha, ingawa ulizidi kumuweka pazuri kwenye anga za muziki.

NILITAKA TUFIKE

Nilitaka tufike kwenye Hata Kwetu Wapo ili kusoma kwa ukaribu hisia za Sam. Ndani ya wimbo huo, Sam anafikisha ujumbe jinsi ambavyo watu wasivyopenda mafanikio yake, wengine ni wakubwa lakini anatamba kwamba kwake watasubiri.

Ni wimbo uliokuwa na ujumbe kuwahusu wale ambao waliamini asingefanikiwa, kwani tayari alikuwa ameshapiga hatua nyingi mbele. Ajabu ya walimwengu ni kwamba baada ya wimbo huo Hata Kwetu Wapo, Sam hakupata kutoa wimbo uliobamba tena kwa kiasi kikubwa.

Hesabu Samaki, Kisiki hadi ngoma mpya aliyoachia Januari mwaka huu, yenye kuitwa Milele. Zote ziligonga ukuta. Ni hapo unakutana na Sam mwenye kulia na ushirikina. Sam alitoka kutamba kuwa watu wengi kwake watasubiri, sasa akawa analia kuwa uchawi upo, akimaanisha anguko lake kwenye muziki ni mafanikio ya watu waliomroga.

Sam alifanya mahojiano na vyombo vingi na kuzungumzia uchawi. Mojawapo alizungumzia kuinuka kwake kimaisha kulisababisha kundi kubwa la familia na marafiki watake awasadie. Alisema uwezo wake ulikuwa mdogo. Matokeo yake wale alioshindwa kuwasaidia hawakufurahia na walikusudia kumkwamisha. Kumkwamisha huko ni kupitia njia za kishirikina. Na ukiyasoma maisha ya Sam unapata taswira ya kijana, ambaye alikuwa anajiona anapitia mapambano makali yasiyoonekana kwenye ulimwengu wa kawaida. Hata wakati akituacha na kuingia kaburini, ameacha simulizi hiyo.

BORA WALI NYAMA

Ni msemo ambao upo mitaani, bora wali-nyama kuliko wali-mwengu. Sam aliuchukua na kuufanya wimbo ambao aliamini ungekuwa mali yake, kumbe ni mali ya walimwengu ambao yeye amewaimba na kusema afadhali wali-tembele, tena bora wali-nyama.

Steven Joseph ‘Jobiso’ ni mtayarishaji, vilevile mmiliki wa studio ya A Sound. Jobiso ambaye miaka ya nyuma alifahamika zaidi kama Small Jobiso kutokana na umahiri wake wa kudansi, ndiye mtengenezaji wa wimbo Walimwengu ambao ni wa mwisho kuimbwa na Sam Wa Ukweli. Jobiso anasema, wimbo ulirekodiwa Jumamosi ya Juni 2, mwaka huu. Sam aliimba wimbo huo akiwa hayupo sawa kiafya. Jumatatu Sam alirejea studio na hakuondoka. Akawa analala palepale studio kungoja wimbo ukamilike matengenezo. Jumatano (Juni 6) mchana, wimbo ulikamilika na Sam alipata nafasi ya kuusikiliza na kuridhika nao. Baada ya hapo alikabidhiwa wimbo wake kwenye ‘flash disc’. Alipopewa wimbo, Sam kwa vile alikuwa anaumwa na hakuwa na nguvu, aliomba apumzike kidogo ili akijisikia mwili umepata nguvu aweze kuondoka. Haikuwa hivyo, Sam hakupata nguvu, bali alizidiwa zaidi na kupelekwa hospitali ambako mauti yalimfika.

Wimbo wake, aliusikiliza, akaridhika nao, akapewa flash disc yenye wimbo. Bila shaka alikuwa na mpango mkubwa na wimbo huo. Hata hivyo, kuonesha kwamba wimbo haukuwa mali yake, hakuondoka nao studio kurudi nao nyumbani. Sasa walimwengu wanausikiliza, wanaburudika kwa ujumbe na sauti yake tamu. Binadamu mali yake ni kifo na kaburi!

Ndani ya Walimwengu; Sam ni yuleyule anayezungumza uchawi. Anatwambia alirogwa, ila inakuwa ni vigumu yeye kueleweka kwa sababu watu wametekwa na imani za wazungu na kuacha imani za mababu. Anamaanisha watu wangeshika misingi ya mababu, wangeelewa kuwa alirogwa.

Sam anaimba; alikuwa hoi kitandani, waliomuona hawakuamini. Kuna ambao hawakujua anasumbuliwa na nini, wengine walivumisha anaumwa Ukimwi, wapo marafiki hawakutaka hata kumwona. Hawakujua kuna mazingara na uchawi. Binadamu moyoni huwezi kujua, walimwengu wana siri hawafai.

Maneno ya wimbo huo, yanatuleta kwa Jobiso ambaye alikuwa na Sam mpaka alipofariki dunia, kwamba msanii huyo aliwaambia anaumwa ukimwi wa kurogwa na kila alipokwenda hospitali dawa hazikumsaidia. Sam aliamini alirogwa na Walimwengu, ndiyo maana ameimba bora wali-nyama, akaongeza bora wali-tembele kuliko Walimwengu.