Azam FC yamfunga kitanzi Mwadini Ally

MATAJIRI wa klabu ya Azam FC, hawataki kulaza damu kabisa katika suala la usajili hasa baada ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, kwani tayari wameishamfunga kipa wao, Mwadini Ally kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kipa huyo msimu huu ameonyesha kiwango cha hali ya juu katika mechi 10 alizocheza na kuibuka mchezaji bora wa mwezi Machi ndani ya kikosi hicho, hii ikiwa ni baada ya kipa wao chaguo la kwanza, Razak Abalora kuwa nje kutokana na adhabu baada ya kufungiwa na Bodi ya ligi ya Shirikisho la soka Tanzania Bara (TPBL).

Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando alithibitisha ndani ya siku mbili zijazo, watakuwa wamemalizana kila kitu na kipa huyo kwani mpaka sasa pande zote mbili tayari zimeshafikia mwafaka.

“Mazungumzo baina ya uongozi wa timu na kipa Mwadini, yamefika mwisho na kilichobakia sasa ni kufanya kwa vitendo kwa maana ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja,” alisema meneja huyo.

Alizungumzia pia ishu ya kuvunja mkataba na mchezaji wao Mghana, Bernard Arthur ni uamuzi wa mchezaji mwenyewe baada ya kutathmini kazi yake na kuona haikuwa na manufaa kwa klabu na sasa klabu inajipanga kwa ajili ya msimu ujao na tayari wameanza na kipa wao huyo.