Dada wa Diamond yamemkuta unaambiwa

DADA wa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz anayefahamika kama Esma Khan ‘Esma Platnumz’ amekanusha taarifa za kutiwa mbaroni kwa kosa la kuuza vipodozi feki na vilivyopigwa marufuku.

Mwanadada huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kaka yake, alisema taarifa za kukamatwa sio za kweli bali watu wanasambaza habari hizo kwa lengo la kutaka kumuharibia bihashara yake.

Hata hivyo, licha ya kukana, Mwanaspoti limebaini kuwa mjasiriamali huyo aliwekwa rumande kwenye kituo cha polisi Mabatini kilichopo Kijitonyama na alifunguliwa kesi kwenye jalada namba KJM/RB/4427/2018 kwa kosa la KUKUTWA NA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU.

Ilielezwa kuwa Esma ametiwa mbaroni baada ya kunaswa na wakaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) akiuza vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye duka lake iliyopo Sinza, Afrika Sana.

Kwa mujibu wa habari za kishushushu ndani ya kituo hicho, maofisa hao walikuwa kwenye msako wa operesheni maalum wa wafanyabiashara wanaoendelea kuuza vipodozi hivyo. Taarifa hizo zilieleza kuwa, Esma alikamatwa na wakaguzi hao saa 9:00 alasiri, na baada ya taarifa hizo kumfikia mama Diamond alifika kituoni hapo akiambatana na watu wengine akiwemo, Petit Man ambaye ni mume wa Esma.