Ishu ya Lulu Baba na Mama Kanumba kila mtu na lake

Muktasari:

  • Baba Kanumba anasema licha ya kifungo cha nje, anaiomba mamlaka husika kumwachia huru kabisa kwani adhabu aliyotumikia gerezani imetosha kwa msanii huyo, aliyekuwa mpenzi wa mwanae, Steven Kanumba.

IMESHATIMIA wiki sasa tangu mwigizaji maarufu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, aachiwe kutoka gerezani baada ya kubadilishiwa kifungo na sasa akitumikia kifungo cha nje. Hata hivyo, imefahamika anayechekelea kuachiwa kwa mwigizaji huyo ni Baba Kanumba, Charles Kusekwa.

Baba Kanumba anasema licha ya kifungo cha nje, anaiomba mamlaka husika kumwachia huru kabisa kwani adhabu aliyotumikia gerezani imetosha kwa msanii huyo, aliyekuwa mpenzi wa mwanae, Steven Kanumba.

Hata hivyo, msimamo wa Baba Kanumba unatofautiana na ule na mzazi mwenzake, Flora Mtegoa.

MSIKIE BABA KANUMBA

Akizungumza na Mwanaspoti Baba Kanumba anasema; “Unajua kila mtu ana mawazo yake, mimi naona ni sawa tu kubadilishiwa adhabu kwa Lulu, maana bado yupo kifungoni, sio kama kaachiwa huru, lakini kama ingezekana ningeiomba mamlaka husika wangemwachiwa tu huru.”

“Kwa mtazamo wangu, maana haya mambo ni mipango ya Mungu na kutokana na ushahidi wake jaji ameona hakukusudia kufanya hivyo, hivyo hakufanya makusudi huyu mtoto na tayari atakuwa ameshajutia kitendo alichokifanya maana hakudhamiria.”

“Pia namshauri mzazi mwenzangu (Mama Kanumba), najua ameumia ila angeachana nayo tu haya mambo, cha msingi ni kumwomba Mungu, apooze tu moyo kwani huyu binti (Lulu) ameshajuta na kujifunza, hivyo asilalamike sana,” alisema Baba Kanumba.

MAMA KANUMBA SASA

Hata hivyo, ushauri huu wa Baba Kanumba unapishana na ule wa Mama Kanumba ambaye mara baada ya kusikia Lulu kabadilishiwa kifungo akitolewa gerezani na kufungwa kifungo cha nje aliongeza na MCL Digital na kusema;

“Licha ya kuwa mimi sijamhukumu Lulu, lakini alipaswa kukaa hata mwaka mmoja ili roho yangu iliridhike, lakini ndio hivyo maskini hana haki.”

Mama Kanumba ni kama vile hajaridhika na kifungo cha Lulu hata alipohukumiwa miaka miwili na kuachiwa kwake ili atumikie kifungo cha nje kumezidi kumsononesha, japo maamuzi hayo yametokana na amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza, Lucas Mboje ndiye aliyenukuliwa akisisitiza adhabu ya Lulu ya kutumikia kifungo cha nje ni amri ya mahakama hiyo na mwigizaji huyo ameanza kutekeleza kwa kufanya usafi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Novemba 13, 2017 mara baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, kumhukumu Lulu kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia Steven Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, 2012, Baba Kanumba aliilalamikia hukumu hiyo.

Alidai ni ndogo wakati akihojiwa na Mwanaspoti katika mahojiano yaliyokuwa hivi;

Mwanaspoti: Shikamoo Baba

Baba Kanumba: Marahaba, Nani mwenzangu?

Mwanaspoti: Naitwa Rhobi wa Gazeti la Mwanaspoti.

Baba Kanumba: Mlikuwa na shida gani?

Mwanaspoti: Tulitaka kujua maoni yako baada ya mahakama kutoa hukumu kwa Lulu kuhukumiwa miaka miwili kwa kumuua mwenenu (Steven Kanumba) bila kukusudi.

Baba Kanumba: Kwa upande wangu hukumu hii kwa nini imekuwa ndogo? Haijanifurahisha hata kama mtu aliua bila kukusudia lakini mahakama imetoa kifungo cha miaka miwili, kama mtu kaua kuku.

Mwanaspoti: Baba kwa upande wako ulitaka mahakama itoe kifungo cha muda gani kukufurahisha?

Baba Kanumba: Nilitegemea mahakama ingetoa kifungo kuanzia miaka mitano, sita au saba na kuendelea.

Mwanaspoti: Kwa nini baba hujatokea kwenye hii kesi kuungana na mke wako mahakamani?

Baba Kanumba: Sikuja huko, nilimwachia mke wangu aendelee na kesi hiyo kutokana na kupunguza gharama zisizo za msingi, hivyo na hukumu yenyewe hiyo ni miaka miwili tu kama kaua kuku, si ningepoteza muda wangu tu hapo kulingana na mazingira ya kifo cha mtoto wangu.

Mwanaspoti: Asante Baba

Baba Kanumba: Nawashukuru.